Friday, June 7, 2013

Lishe bora duniani ipewe kipaombele

Utapia mlo ni tatizo ambalo linakumba sehemu nyingi duniani
Utapia mlo husababisha asilimia 45 ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kote duniani. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la matabibu la Lancet.
Utafiti huo unasema kuwa , lishe duni husababisha vifo vya watoto milioni 3.1 walio chini ya umri wa miaka mitano kila mwaka
Kikundi cha kimataifa kilidurusu sababu mbali mbali zinazochangia kuwepo utapia mlo miongoni mwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Wanasema kuwa siku za kwanza miamoja za maisha ya mtoto, huwa muhimu sana kwa maisha ya mtoto yule.
Utapia mlo ambao kwa upande mmoja unamaanisha kuwa uzani wa juu kupita kiasi au kukosa lishe bora, pia ina athari zake kiuchumi.
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, utapia mlo hugharimu dunia dola trilioni 3.5 hadi trilioni miatano kwa kila mtu upande wa matibabu na kazi.
''Upande wa afya ya uzazi na afya ya watoto, hali inaweza kuiamarishwa, matokeo mazuri yanaweza kukuza kizazi sababu ambayo inatupasa kushirikiana kuchukua nafasi hii nzuri,'' alisema daktari Richard Horton
Kikundi cha madaktari kilichoongozwa na Profesa Robert Black, kilidurusu utafiti kuhusu utapia mlo kwa watoto na akina mama wajawazito katika nchi maskini duniani tangu mwaka 2008.
Wataalamu hao pia walidurusu uimarishaji wa mipango ya kitaifa na kimataifa kuhusu lishe bora kwa watoto na akina mama wajawazito.
Aidha wanasema kuwa licha ya hatua kupigwa katika miaka ya hivi karibuni, wanakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni 165, walikumbwa na utapia mlo pamoja na kudumaa.
Watoto 900,000, wanaweza kuokolewa katika nchi 34 ikiwa viwango vya lishe bora vinaweza kuboreshwa hadi asilimia 90 ya dunia nzima
Watafiti wanaonya kuwa Nchi hazitaweza kujiondoa kwa umaskini ikiwa dunia haiwezi kuweka swala la lishe bora kuwa kipaombele duniani.
Daktari Richard Horton, mhariri mkuu wa jarida la Lancet, alisema kuwa ikiwa viwango vya lishe bora vinaweza kuboreshwa , matokeo yake mazuri yanaweza kufaidi kikazi kijacho.
Wataalamu wanaofanya kazi katika nchi zinazokuwa wanakutaka wikendi hii mjini London, kwa mkutano unaoandaliwa na serikali za Uingereza na Brazil.
Mkutano huu utafuatwa na mkutano mwingine wa kila mwaka wa nchi zilizostawi kiuchumi duniani za G8.
Kampeini inayohamasisha chakula cha kutosha kwa kuchangisha dola bilioni moja kila mwaka kama pesa za ziada za msaada kuweza kutumika kwa miradi ya lishe bora ifikapo mwaka 2015.

Wasomali Afrika.K walaani mashambulizi



Watu wa jamii ya wasomali nchini Afrika Kusini, wameandamana hadi bunge la la kitaifa mjini Cape Town kupinga mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni nchini humo.
Raia wawili wasomali, wameuawa mwezi huu na serikali ya Somalia imeiomba Afrika Kusini kuchukua hatua zaidi kuweza kuwalinda raia wake.
Takriban watu 200 waliandamana wakibeba mambango yaliyoandikwa: ''kila mtu ni raia wa kigeni katika sehemu fulani ya dunia''
Waandishi wa habari wanasema kuwa mashambulizi dhidi ya waafrika wasio raia wa Afrika Kusini yameanza kutekelezwa katika siku za hivi karibuni.
Baadhi ya waandamanaji waliwashtumu maafisa wa utawala kwa kutochukua hatua zaidi kuwalinda raia wa kigeni , hususan wasomali.
Kulingana na kitengo cha haki za bindamu katika chuo kikuu mjini Pretoria,raia wa Afrika Kusini hawajakuwa wakionywa dhidi ya kuwashambulia raia wa kigeni .
Mwandishi wa BBC Mohammed Allie mjini Cape Town wanasema kuwa ghasia hizo zinahusishwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, nchini Afrika Kusini.
Katika miaka ishirini iliyopita, maelfu ya wasomali wametoroka vita nchini Somalia na kuhamia Afrika Kusini ambako wameweza kuanzisha biashara ndogondogo katika sehemu za mijini.

Umoja wa Mataifa kuisaidiaTanzania kuanzisha benki ya wakulima

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limekubali kuisaidia Tanzania kuanzisha benki teule ya wakulima, gazeti la Daily News la Tanzania liliripoti Jumatano (tarehe 5 Juni).
"Ahadi yangu kwenu ni kwamba FAO itawasiliana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuona jinsi tunavyoweza kusaidia kuanzisha benki," Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva alimwambia Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Da Silva alisifu jitihada za Tanzania za kuwasaidia wakulima, lakini alisema mkazo unapaswa kuwa katika kutoa mikopo kwa wakulima kuliko ruzuku, ambazo aliziita si endelevu.

Waandishi wa habari wa Kenya watishia bunge kwa kuzuia vyombo vya habari

Waandishi wa habari walitishia kusimamisha kutoa habari za bunge Jumatano (tarehe 5 Juni) baada ya Ofisa wa bunge Justin Bundi kuwafukuza kwenye kituo cha habari katika bunge.
"Hatua kama hiyo haijawahi kutokea katika Kenya huru," Mwenyekiti wa chama cha Wahariri cha Kenya Macharia Gaitho alisema kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya. "Wamerudi kwenye zama za kale za kutwezwa, udikiteta na haitegemewi kabisa katika jamii ya kisasa, yenye maendeleo na yenye demokrasia."
Gaitho na wanachama wa chama hicho walitia saini taarifa inayosema watavitaka vyombo vya habari kusimamisha kuchukua matukio ya habari za bunge hadi ufikivu wa vyombo vya habari uliozuiliwa urejeshwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Alphonce Shiundu alisema kuzuia vyombo vya habari kuchukua habari za matukio kutaipeleka Kenya "kwenye zama za siku za giza", kwa mujibu wa Capital FM ya Kenya. "Wakenya wanahitaji kuwasikiliza viongozi wao. Waandishi wa habari wanahitaji kuwaambia Wakenya nini viongozi wao wamesema katika bunge."

Kenya, Somalia yaanzisha kikundi kazi cha kurejesha nyumbani wakimbizi

Kenya na Somalia zimeunda kikundi kazi cha pamoja kuanzisha njia ya kuwarejesha nyumbani na upataji wa makaazi mapya kwa wakimbizi wa Somalia nchini Kenya, gazeti la Daily Nation la Kenya liliripoti Jumatano (tarehe 15 Juni).
Kikundi kazi, kilichoundwa kufuatia kikao cha Nairobi baina ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, kitatoa vigezo kwa ajili ya majadiliano kwenye mkutano huo kuhusu wakimbizi uliopangwa kufanyika mwezi Agosti.
Kenyatta alitoa wito kwa jumuiya za kimataifa kusaidia jitihada za upataji wa makaazi mapya kwa wakimbizi, akisema uwepo wa idadi kubwa ya Wasomali nchini Kenya kumekuwa na athari hasi kwenye uchumi wa nchi, usalama na mazingira.
Mohamud aliishukuru Kenya kwa mchango wake kwenye Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, akitoa salamu zake za rambirambi kwa vifo vya Wakenya na askari wengine.

Hospitali za Kenya zachelewa kutekeleza agizo la msamaha wa ada ya uzazi

Chini ya agizo la serikali mpya, huduma za uzazi kwa sasa ni bure katika hospitali za umma, vituo vya afya na kwenye kliniki nchini Kenya, lakini baadhi ya vituo vya kutoa huduma za afya bado havifuati agizo hili la msamaha wa ada zinazohusiana na uzazi.
"Serikali yangu imefanya mipangilio ya bajeti inayotosha kuwezesha akina mama wote wajawazito kupata huduma za uzazi bure katika vituo vya afya vya umma, kuanzia tarehe 1 Juni, 2013," Rais Uhuru Kenyatta alisema katika kulihutubia taifa Siku ya Madaraka, kufuatia ahadi ya kampeni ya Muungano wa Jubilee aliahidi kutekeleza wakati wa siku 100 za mwanzo madarakani.
Fedha zilizowekwa katika bajeti ya mwaka 2013-2014 zinawapa Wakenya wote fursa nzuri ya kupata huduma za msingi za afya kwenye vituo na zahanati zinazoendeshwa na serikali, rais alisema.
Kenyatta pia alifuta ada ya shilingi 10 (senti 12 ) na shilingi 20 (senti 23), ambayo zahanati na vituo vya afya vimekuwa vikitoza wagonjwa.
Hata hivyo, baadhi ya vituo vya afya vimeendelea kutoza akina mama wanaokwenda kujifungua watoto wao.
"Wakati agizo la rais linatolewa, kwa kawaida tunapaswa kusubiri waraka kutoka wizarani ukitoa maelekezo," Mrakibu wa Hospitali ya Mbagathi huko Nairobi Daktari Andrew Sule aliiambia Sabahi. "Wakina mama wanaokuja kujifungua watapaswa kulipa hadi tutakapopokea mawasiliano rasmi."
Idadi ya akina mama wanaoshindwa kurejea nyumbani baada ya kujifungua kwa kushindwa kulipa ada ya uzazi -- ambayo inagharimu shilingi 7,000 (dola 82) kwa ujifunguaji wa kawaida na shilingi 15,000 (dola 176) kwa huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji -- wamekuwa wakiruhusiwa kurudi nyumbani kwa sababu hatimaye ada itafutwa, alisema.
Mkurugenzi wa hospitali kuu ya Garissa Musa Mohammed alisema kituo chake pia hakitakuwa na haraka ya kutekeleza agizo la rais. Ada ya kujifungua inaleta mapato mengi kwa hospitali yoyote, na fedha hizo huenda kwenye gharama za ukarabati, alisema.
"Kunapaswa kuwa na utaratibu na itifaki ya jinsi [vituo] vya uzazi vitakavyotunzwa kwa sasa ambapo ada ya uzazi imefutwa," aliiambia Sabahi. "Tangu Jumatatu, tulikuwa hatujapokea mawasiliano yoyote rasmi kuhusu matarajio ya siku zijazo."
Hata hivyo, baadhi ya hospitali zinasita kidogo kutekeleza sera mpya.
Siku ya Jumapili (tarehe 2 Juni), Jackson Mutua wa viunga vya jirani na Kayole vya Nairobi alimpeleka mke wake katika Hospitali ya Wilaya ya Mama Lucy Kibaki.
"[Huduma] za uzazi za bure nilipewa taarifa zake na mfanyakazi wa hospitali baada ya kuulizia ni fedha kiasi gani nilizokuwa natakiwa kulipia," aliiambia Sabahi.
Ufutaji wa ada ulikuja katika wakati muafaka, alisema, kwa sababu alipanga kukopa fedha kwa rafiki ili kulipia gharama. "nafanya kazi kama fundi mwashi na sikuwa na fedha wakati mke wangu [alipojisikia] uchungu," alisema. "Sasa naweza kuzingatia katika kutafuta chakula kwa ajili ya mke wangu na mtoto wangu aliyezaliwa."
Omar Mwanjama, ofisa ugani wa Baraza la taifa la Kudhibiti UKIMWI katika mkoa wa kaskazini mashariki mwa Kenya, alisema kufuta ada ya uzazi kunasaidia kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa kuwa wanawake wachache wangechagua kujifungulia nyumbani.
"Sasa, wakina mama wanaweza kwenda hospitalini ambako watasaidiwa na wataalamu," alisema.
Mbunge wa jimbo la Tarbaj Mohammed Ibrahim Elmi alisema ameyapokea maagizo, lakini itahitaji kujitoa rasmi ili kufuatilia kikamilifu.
"Katika matukio mbalimbali, maelekezo kama hayo yaligeuka kuwa kauli za kisiasa kuivutia halaiki," aliiambia Sabahi. "Ili yaweze kufuatwa, yanapaswa kuwa katika mawasiliano ya maandishi ili yatekelezwe."

Djibouti yaendelea kukandamiza upinzani

Polisi wa Djibouti walivamia nyumba ambako wanachama wa chama cha upinzani cha Union for National Salvation (USN) waliokuwa wanakutana katika kitongoji cha Warabaley huko Balbala siku ya Jumapili (tarehe 2 Juni), na kuwatia mbaroni watu 13 akiwemo Rais wa USN Ahmed Youssouf.
  • Askari wa kikosi cha polisi cha Djibouti wakijitayarisha katika kitongoji cha Balabala tarehe 1 Machi, 2013 kukabiliana na wanaharakati vijana waliokuwa wanaipinga serikali kuwakamata viongozi wa upinzani. [Na Harbi Abdillahi Omar/Sabahi]  
  • Askari wa kikosi cha polisi cha Djibouti wakijitayarisha katika kitongoji cha Balabala tarehe 1 Machi, 2013 kukabiliana na wanaharakati vijana waliokuwa wanaipinga serikali kuwakamata viongozi wa upinzani. [Na Harbi Abdillahi Omar/Sabahi]
Mwanachama wa USN na Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Balbala Ali Mohamed Dato alisema kuwa watu wawili walijeruhiwa katika operesheni hiyo, iliyofanyika siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Djibouti Hassan Omar Mohamed kutishia hapo tarehe 29 Mei kuwa atakivunja chama cha USN ikiwa hakitaacha shughuli zisizoifaa serikali.
Wanachama wa USN waliokamatwa waliachiliwa siku ya Jumatatu wakisubiri siku ya kufikishwa mahakamani, ambayo bado haijatangazwa.
Tangu matokeo yaliyogombaniwa ya uchaguzi wa bunge kutangazwa hapo tarehe 23 Februari, upinzani umekuwa ukiwahamasisha wanachama wake kuandamana kila Ijumaa, licha ya kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imewapiga marufuku kufanya hivyo.
Serikali ya Djibouti imewatia mbaroni wanachama wa upinzani katika kujibu maandamano hayo, na kuwashtaki kwa kuchochea vurugu. USN sasa inadai kuwa kuna wafungwa zaidi ya 600 wa kisiasa nchini Djibouti, ingawaje serikali inasisitiza kuwa hakuna hata mmoja.
USN imeendelea kutoa wito wa kufutwa kwa chama cha Union for a Presidential Majority (UMP) kinachoidhibiti serikali, na kuunda hapo mwezi wa Machi bunge sambamba, Bunge Halali la Taifa (ANL), linaloongozwa na Ismail Guedi Hared, kiongozi wa mgombea wa USN katika orodha ya Jiji la Djibouti wakati wa uchaguzi.
"Hofu imeingia makambini," alisema Katibu Mkuu wa USN Abdourahaman Mohamed Guelleh. "Yote hii ni sehemu ya kampeni ya vitisho ya serikali lakini sisi hatutasalimu amri."
"Leo chama cha ANL, ambacho kimeundwa na USN, mshindi wa uchaguzi wa wa tarehe 22 Februari, kinashauriana na watu wa Djibouti katika ngazi ya taifa," aliiambia Sabahi. "Serikali inatutaka tusizungumze na watu ambao walituchagua na kutuunga mkono."
Mbunge wa UMP Houssein Ali alisema kuwa USN inahitaji kukubali kushindwa. "Uchaguzi umemalizika na UMP imeshinda uchaguzi -- upinzani haina chochote cha kupendekeza kwa watu wa Djibouti isipokuwa kuandamana mitaani."
"Kila wakati ambapo chama cha kisiasa kinapotaka kuandamana, wanataka waandamane katika Wizara ya Mambo ya Ndani," aliiambia Sabahi. "Na sehemu za kuabudia -- kwa mfano huu, misikiti -- kwa hali yoyote haiwezi kuwa jukwaa la shughuli za kisiasa au maandamano bila ya adhabu kali chini ya sheria ya jinai."
Moktar Abdi, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Djibouti, alisema vyama vyote vinahitaji kukaa meza moja ili kuzungumza na kuafikiana kwa faida ya jumla ya taifa.
"Jinsi mambo yanavyokwenda, nchi inaelekea katika ukuta wa matofali," aliiambia Sabahi.