Thursday, May 23, 2013

ASKARI ALIYENASWA NA MAGUNIA 18 YA BANGI HUKO HIMO AWATOROKA POLISI

ASKARI Polisi Koplo Edward, anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya (bangi) gunia 18 huko Himo, Kilimanjaro tarehe 18, Mei 2013, ametoroka chini ya ulinzi wa askari polisi saba na kutokomea kusikojulikana.

Mtuhumiwa huyo alikuwa dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser namba PT. 2025 la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema askari huyo akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi saba, walikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya ukaguzi, na walipofika nyumbani kwa  mtuhumiwa, walimwamini na kumwacha kuingia ndani peke yake nao waliingia ndani ili kuendelea na upekuzi, na ndipo mtuhumiwa alipofungua mlango wa nyuma ya nyumba yake na kukimbia bila ya wao kufanikiwa kumkamata
 

Alisema polisi imemkamata Inspekta wa Polisi Izaack Manoni aliyekuwa anasimamia upekuzi huo: “Inspekta Manoni yupo chini ya ulinzi na hatua za kinidhamu dhidi yake zitachukuliwa,” alisema ACP Sabas na kuongeza:  
“Mtuhumiwa Edward, anayetafutwa kwa sasa alishafukuzwa kazi, akipatikana atafikishwa mahakama ya kiraia kusomewa mashitaka ya kufanya biashara ya dawa za kulevya,” alisema.

Alisema tayari mtuhumiwa mwenzake ambaye ni askari polisi mwenye namba G. 2434 PC George, amesomewa mashitaka yake jana.


Mbali na mtuhumiwa huyo, watuhumiwa wengine waliokamatwa na magunia 30 ya bangi wilayani Arumeru nao wamepandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yao.

HALI BADO NI MBAYA MTWARA....WANAFUNZI WAWILI WAMETANDIKWA RISASI, MMOJA AMEFARIKI HAPOHAPO

Mwandishi wetu aliyepo Mtwara ametueleza kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wa eneo la magomeni mkoani mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo..

Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari magereza . Mwanafunzi wa CHUNO amefikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.  
Mwanamke mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 mjamzito ameuawa kwa kupigwa risasi maiti ipo Ligula.




Kwa sasa ( jioni  hii) inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokua eneo la magomeni ambako mbomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule

PICHA ZA SHEHA WA TOMONDO- ZANZIBAR ALIYEMWAGIWA TINDIKALI JANA USIKU

\
Sheha Mohammed Omary Said aliyemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana akiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja akipatiwa matibabu, Sheikh Mohammed amepata maumivu makali sehemu za kifuwa na jicho kuumia

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,Mukhadam Khamis,amesema chombo kilichotumika kumwagia tindikali Sheha huyo kilipatikana eneo la tukio na kwamba polisi imekichukua kwa kukichunguza kitaalam ili kugundua aliyekuwa akikitumia kwa kuangalia alama za vidole.

Sheha huyo alimwagiwa tindikali jana usiku wakati alipotoka nje ya nyumba yake kuchota maji na ndipo mhalifu huyo alipomwagia tindikali na kwamba hakuweza kumtambua.

Sheha Mohammed Kidevu akiwa katika wodi ya Hospitali kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja akipata matibabu ya majaraha ya kitu kinachosadikiwa kwa Tindi Kali,akipata matibabu hayo katika hospitali hiyo.