Wednesday, July 31, 2013

Vifo kutokana na HIV vyapungua Afrika


UNAIDS inasema kuwa vifo vinavyotokana na 
HIV vimepungua Afrika kwa asilimia 40
Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba Afrika imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.
Vifo vinavyotokana na maradhi ya Ukimwi Mashariki na Kusini mwa Afrika vimepungua kwa asili mia 40.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na ukimwi- UNAIDS umehusisha hatua za sasa na kutolewa kwa dawa za kukabiliana na makali ya Ukimwi.
Umoja wa Mataifa umesema mataifa ya Botswana, Ethiopia, Kenya, Zambia na Zimbabwe yamepunguza idadi ya watu wanaokufa kwa ukimwi kwa zaidi ya nusu.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa Maradhi nyemelezi ya kifua kikuu pia yamepungua sana tangu mwaka 2005.

Mohammed Morsi yuko salama' Ashton

Ashton alikutana na Morsi ingawa anasema hajui aliko
Mwakilishi wa mambo ya nje katika Muungano wa Ulaya Catherine Ashton amekutana na Rais aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohammed Morsi katika eneo lisilojulikana. Morsi amekuwa akizuiliwa na jeshi tangu kuondolewa madarakani mapema mwezi huu.
Ashton amewaambia waandishi wa habari mjini Cairo kwamba Bw. Morsi alikua salama na kwamba alikubaliwa kutazama habari kwenye runinga na kusoma gazeti.
Alisema walijadili haja ya Misri kuganga yajayo na kuweka amani.Baroness Ashton amesema mchakato wa utawala mpya sharti ushirikishe pande zote
Msemaji wa Bi Catherene Ashton, alisema kuwa mkutano ulifanyika katika eneo lisilojulikana ambako Morsi anazuiliwa na kuwa ulidumu kwa masaa mawili.
Hakutoa maelezo kuhusu walichokijadili.
Hata hivyo tayari ameshakutana na maafisa kadhaa wa serikali akiwemo rais wa muda Adly Mansour, mkuu wa majeshi, Generali Abdel-Fattah al-Sisi na makamu wa rais wa maswala ya kigeni,Mohamed ElBaradei.
Alisema kuwa atatoa wito kwa pande zote mbili kushirikishwa katika serikali. Ziara ya Ashton ambayo ni ya pili nchini Misri inakuja baada ya wafuasi zaidi ya sabini wa Morsi kuuawa kwenye makabiliano na vikosi vya usalama nchini Misri.
Wafuasi wa kiongozi huyo wamesema kuwa wanapanga kufanya maandamano Jumanne huku serikali ya muda ikiwatahadharisha dhidi ya kuhusika na ghasia na kuwa watakaovunja sheria watachukuliwa hatua.
Maafisa wa usalama pia wametishia kuvunja maandamano ya wafuasi hao waliopiga kambi nje ya medani iliyo karibu na msikiti wa Rabaa al-Adawiya mjini Cairo.

Zimbabwe yapiga kura kupata utawala mpya


Wapiga kura Zimbabwe
Raia wa Zimbabwe wanapiga kura katika uchaguzi wa Urais unaotajwa kuwa na ushindani mkali huku kukiwa na madai ya udanganyifu. Rais Robert Mugabe wa miaka 89 amesema atang'atuka ikiwa yeye na chama chake cha Zanu-PF watashindwa.
Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na chama chake cha Movement for Democratic Change (MDC) wamelalamikia Zanu-PF kwa kuhitilafiana na utaratibu wa uchaguzi ili kunyakua ushindi, lakini chama tawala kimekanusha madai hayo.Shughuli za kampeini zimekua ghasia zozote huku kukiwa na visa vichache sana vya kuwatisha wapiga kura.
Vyama vya Zanu-PF na MDC viliunda serikali ya muungano mwaka wa 2008 baada ya muafaka wa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia matokeo ya Urais yaliyozua utata. Bw.Tsvangirai alishinda awamu ya kwanza, lakini akajiondoa kwa raundi ya pili akilalamikia mashambulizi yaliyolenga wafuasi wake.
Serikali ya Zimbabwe imewapiga marufuku waangalizi wa magharibi kuchunguza uchaguzi wa leo. Hata hivyo Muungano wa Afrika{AU}, Kanda ya Kusini mwa Afrika{SADC} na makundi ya kijamii nchini Zimbabwe yamekubaliwa kufuatilia jinsi uchaguzi utakavyoendeshwa.
Watu milioni 6.4 wamejiandikisha kupiga kura hii, na maelfu walijitokeza kwenye kampeini za uchaguzi. Matokeo yanatarajiwa kutolewa kwa siku tano zijazo.Mwandishi wa BBC aliyeko Harare amesema kuna foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura leo ikiwa siku ya mapumzoko kuhakikisha raia wanapata nafasi ya kuamua serikali mpya.
Mshindi wa moja kwa moja sharti apate asili mia 50 ya kura zote kutangazwa Rais. Ikiwa hakuna mgombea atapata kura hizo, raundi ya pili imepangwa kufanyika Septemba 11. Uchaguzi huu ndio wa kwanza kufanyika Zimbabwe chini ya katiba mpya iliyopitishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Mgomo wa wanafunzi wa sekondari ya Lutheran Junior seminari umeingia siku ya 2.




Mgomo wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lutheran junior Seminary inayomilikiwa na kanisa la kilutheri Tanzania umeingia siku ya pili baada ya wanafunzi  kugoma kutwa nzima kuingia madarasani na kuandamana katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam na kulazimu jeshi la polisi kuingilia kati kuzuia maandamano.
 Wanafunzi hao wamesikika wakiimba wanataka kuonana na askofu mkuu wa KKKT Alex Malasusa huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali ambapo wakiwa njiani katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam jeshi la polisi walisitisha maandamano kwa madai ya kutofuata taratibu za kuomba kibali.
Wanafunzi hao walilazimika kurudi shuleni kwa maandamano wakisindikizwa na ulinzi wa jeshi la polisi lakini walipofika shuleni hapo mambo yalionekana kuwa magumu zaidi hata hivyo hawakutaka kusikiliza walimu na ikamlazimu mkuu wa wilaya Saidi Amanzi kufika shuelni hapo na kuzungumza na uongozi ni wa shule ambapo amesema inawalazimu kusubiri viongozi wa KKKT kutoka makao mjini Arusha .
Kwa upande wao wanafunzi wamesema wataendelea na mgomo huo kutokana na ahadi zilizotolewa kushindwa kutekelezeka na kushinikiza kutaka kuonana na askofu mkuu Alex Malalasusa ili awasaidie kutatua kero zao.