Polisi wa Djibouti walivamia nyumba ambako wanachama wa chama cha
upinzani cha Union for National Salvation (USN) waliokuwa wanakutana
katika kitongoji cha Warabaley huko Balbala siku ya Jumapili (tarehe 2
Juni), na kuwatia mbaroni watu 13 akiwemo Rais wa USN Ahmed Youssouf.
Mwanachama wa USN na Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Balbala Ali Mohamed
Dato alisema kuwa watu wawili walijeruhiwa katika operesheni hiyo,
iliyofanyika siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Djibouti
Hassan Omar Mohamed kutishia hapo tarehe 29 Mei kuwa atakivunja chama
cha USN ikiwa hakitaacha shughuli zisizoifaa serikali.
Wanachama wa USN waliokamatwa waliachiliwa siku ya Jumatatu
wakisubiri siku ya kufikishwa mahakamani, ambayo bado haijatangazwa.
Tangu matokeo yaliyogombaniwa ya uchaguzi wa bunge
kutangazwa hapo tarehe 23 Februari, upinzani umekuwa ukiwahamasisha
wanachama wake kuandamana kila Ijumaa, licha ya kuwa Wizara ya Mambo ya
Ndani imewapiga marufuku kufanya hivyo.
Serikali ya Djibouti imewatia mbaroni wanachama wa upinzani
katika kujibu maandamano hayo, na kuwashtaki kwa kuchochea vurugu. USN
sasa inadai kuwa kuna wafungwa zaidi ya 600 wa kisiasa nchini Djibouti,
ingawaje serikali inasisitiza kuwa hakuna hata mmoja.
USN imeendelea kutoa wito wa kufutwa kwa chama cha Union for a
Presidential Majority (UMP) kinachoidhibiti serikali, na kuunda hapo
mwezi wa Machi bunge sambamba, Bunge Halali la Taifa (ANL),
linaloongozwa na Ismail Guedi Hared, kiongozi wa mgombea wa USN katika
orodha ya Jiji la Djibouti wakati wa uchaguzi.
"Hofu imeingia makambini," alisema Katibu Mkuu wa USN Abdourahaman
Mohamed Guelleh. "Yote hii ni sehemu ya kampeni ya vitisho ya serikali
lakini sisi hatutasalimu amri."
"Leo chama cha ANL, ambacho kimeundwa na USN, mshindi wa uchaguzi wa
wa tarehe 22 Februari, kinashauriana na watu wa Djibouti katika ngazi ya
taifa," aliiambia Sabahi. "Serikali inatutaka tusizungumze na watu
ambao walituchagua na kutuunga mkono."
Mbunge wa UMP Houssein Ali alisema kuwa USN inahitaji kukubali
kushindwa. "Uchaguzi umemalizika na UMP imeshinda uchaguzi -- upinzani
haina chochote cha kupendekeza kwa watu wa Djibouti isipokuwa kuandamana
mitaani."
"Kila wakati ambapo chama cha kisiasa kinapotaka kuandamana, wanataka
waandamane katika Wizara ya Mambo ya Ndani," aliiambia Sabahi. "Na
sehemu za kuabudia -- kwa mfano huu, misikiti -- kwa hali yoyote haiwezi
kuwa jukwaa la shughuli za kisiasa au maandamano bila ya adhabu kali
chini ya sheria ya jinai."
Moktar Abdi, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Djibouti,
alisema vyama vyote vinahitaji kukaa meza moja ili kuzungumza na
kuafikiana kwa faida ya jumla ya taifa.
"Jinsi mambo yanavyokwenda, nchi inaelekea katika ukuta wa matofali," aliiambia Sabahi.
No comments:
Post a Comment