Thursday, July 25, 2013

Njama ya uasi yatibuka Ivory Coast


Gereza la Maca ambako wahalifu sugu wanafungwa
Njama ya uasi pamoja na jaribio la wafungwa kutoroka jela kubwa zaidi nchini Ivory Coast imetibuka na kusababisha vifo vya wafungwa wawili.
Polisi walilazimika kurusha gesi ya kutoa machozi pamoja na kufyatua risasi ili kutuliza hali katika gereza la Maca mjini Abidjan.
Maafisa wanasema kuwa walinzi wawili wa magereza walijeruhiwa vibaya.
Purukushani lilizuka Jumanne jioni wakati wafungwa kadhaa walipovunja milango ya magereza yao na kuwaachilia huru baadhi ya wafungwa.
Gereza hilo huwahifadhi wahalifu sugu na baadhi ya maafisa kutoka kwa iliyokuwa serikali ya rais wa zamani Laurent Gbagbo.

Rais wa Sudan Kusini (Salva Kiir) avunja baraza la mawaziri


Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amelivunja baraza lake la mawaziri pamoja na kumfuta kazi makamu wa rais Riak Machar katika mabadiliko makubwa zaidi kuwahi kutekelezwa katika historia ya miaka miwili ya taifa hilo.
Aliyekuwa waziri wa habari, Barnaba Marial Benjamin, ameiambia BBC kuwa mawaziri wote kutoka kwa Makamu wa Rais Riek Machar wameondolewa.
Duru zinasema haijabainika iwapo kuna waziri yeyote miongoni mwa wale waliofutwa kazi atarejeshwa katika baraza jipya la mawaziri litakalobuniwa.
Pia hakuna sababu iliyotolewa kuhusiana na hatua ya rais kuwafuta kazi maafisa hao , lakini wadadisi wanasema kuwa Bwana Kiir na makamu wake Machar wamekuwa na mgogoro wa mamlaka kwa miezi kadhaa sasa.
Sudan Kusini imekumbwa na matatizo chungu nzima hasa ya kiuchumi tangu kujitenga na Sudan mwaka 2011.
Uthabiti wake umetatizwa na malumbano kati yake na Sudan kuhusu mipaka na swala la mafuta.
Hivi karibuni baadhi ya maafisa wa Bwana Kiir, wamekuwa wakizungumzia kuwepo minong'ono kuhusu uongozi wake.
Ripoti zinasema kuwa Kiir anajitahidi kusalia na ushawishi katika chama cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM), ambacho kinathibiti serikali.
Kwa upande wake bwana Machar, ambaye mwezi Aprili alipunguziwa mamlaka, alisema huenda akagombea uongozi wa chama cha SPLM dhidi ya rais Kiir, kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Kuvunja baraza la mawaziri ni dalili ya juhudi kubwa za rais kubadilisha sio tu serikali yake bali pia mamlaka na njia za kuingia madarakani nchini humo.
Ingawa mabadiliko yaliyotangazwa jana yamekuwa yakitarajiwa, wakati wa kutangazwa kwake ndio umeleta shaka na wasiwasi kuwa rais huenda anatumia mamlaka yake kubana upinzani na kuzuia mgawanyiko katika serikali yake.

Marekani kuchelewesha ndege kwa Misri


Marekani inanuia kuikabidhi Misri ndege 20 za kivita
Marekani imesema kuwa itachelewesha mpango wake wa kuikabidhi Misri ndege za kivita aina ya F-16 huku mgogoro wa kisiasa ukiendelea kutokota nchini Misri kufuatia kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Rais Mohammed Morsi.
Msemaji wa idara ya ulinzi nchini Marekani, George Little alisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa kutokana na hali inayokabili Misri kwa sasa.
Marekani inadadisi ikiwa kuondolewa mamlakani kwa Morsi ilikuwa mapinduzi ya kijeshi, hali inayoweza kusababisha Marekani kusitisha msaada wake kwa Misri.
Hapo jana mkuu wa jeshi la Misri Generali Sisi , aliitisha maandamano ya umma akiwataka wananchi kuliruhusu jeshi kukabiliana na kile alichokiita tisho la ugaidi.
Lakini Abdel Fattah al-Sisi aliongeza kuwa hakuwa anaitisha maandamano kwa lengo la vurugu huku akiwasihi wananchi kuwa na maridhiano.
Katika jibu lake kwa wito wa jeshi, chama cha Muslim Brotherhood, ambacho kinamuunga mkono Morsi, kilisema kuwa Generali Sisi alikuwa anaitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndege hizo nne aina ya F-16 ni sehemu ya ndege nyingine 20 ambazo zimeitishwa, kati ya hizo nane tayari zikiwa zimepelekwa Misri.
Hata hivyo Marekani iliahidi tarehe 11 mwezi Julai kuwa bado ina mpango wa kuikabidhi Misri ndege hizo.