Tuesday, April 23, 2013

Muingereza awafananisha Watanzania na nguruwe

Bibi. Sarah Hermitage ambaye ni Mwanasheria raia wa Uingereza, mwanaharakati wa kupambana na rushwa na pia mwekezaji katika shamba la Silverdale. Anapatikana @Chomachomp au http://thesilverdalecase.blogspot.com/
Bibi. Sarah Hermitage ambaye ni Mwanasheria raia wa Uingereza, mwanaharakati wa kupambana na rushwa na pia mwekezaji katika shamba la Silverdale.
Anapatikana @Chomachomp au http://thesilverdalecase.blogspot.com/
KATIKA hali inayoonyesha dharau kwa Watanzania na waumini wa Dini ya Kiislamu, Muingereza Sarah Hermitage, amefananisha Watanzania na nguruwe ambaye ni mnyama haramu kwa mujibu wa imani ya Kiislamu.
Sarah ambaye amekua akiwakashifu viongozi na wananchi wa Tanzania mara kwa mara alivuka mipaka na kufananisha Watanzania na nguruwe, baada ya kulalamikiwa kwa vitendo vyake vya kutoa maneno machafu kwa Watanzania katika mitandao ya kijamii.
Kauli hizo za Sarah amekua akizitoa kupitia mitandao ya twitter kupitia ukurasa wake wa https://twitter.com/Chomachomp kwa muda mrefu sasa bila kuchukuliwahatua zozote na viongozi wala watendaji wa serikali ya Tanzania.
Kauli ya Sarah kuita Watanzania ilianzia pale Mtanzania mmoja ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe Mbaraka Islam, kulalamikia kitendo chake cha kutukana viongozi na Watanzania wote kwa ujumla wao bila kuwa na hoja zinazowahusu.
Huku akijua aliyewasiliana naye ni Muislamu, Sarah aliandika katika ukurasa wake kwamba “anga la Tanzania limejaa nguruwe wanaopaa, Mbaraka Islam, ni kupe wa mwezi”, akimaanisha kwamba Mbaraka Islam ni mmoja wa nguruwe wengi wanaoelea katika anga la Tanzania.
“Kwa maana yoyote anayotaka kuuaminisha umma na katika mazingira ya Tanzania na Dini yetu, haiwezekani kwamba Sarah hakujua kwamba ni kashfa nzito ya Kidini kumfananisha Muislamu na nguruwe kwa namna yoyote ile. Alijua mimi ni Muislamu alifanya hivyo kusudi.
“Huyu mama (Sarah) amefanya hivyo baada ya kuona Watanzania wamelala na hakuna anayethubutu kumgusa hasa viongozi wetu anaowatukana anavyotaka bila kuguswa na yeyote,” alisema Islam na kuongeza kwamba amechukua hatua kadhaa ambazo hajapenda kuziweka hadharani kwa sasa.
Kwa mujibu wa imani ya dini ya Kiislamu, mnyama nguruwe ni haramu na najisi na kwamba haruhusiwi kuliwa na unapomgusa unapaswa kujitakasa kwa kuoga mara saba moja ikiwa ni kwa kutumia mchanga.
Sarah alikerwa na makala aliyoandoka Islam katika gazeti la Raia Mwema, ambayo  ilielezea kukerwa na maneno machafu anayoyatoa kwa Watanzania.
Katika makala hiyo, Islam alisema:
KWA takriban miaka mitano sasa, raia mmoja wa Uingereza, Sarah Hermitage amekuwa akiendesha kampeni ya kumchafua Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya Tanzania, taasisi muhimu za nchi yetu kama vile mahakama, waandishi wa habari na hata Watanzania ambao wamekua wakimpinga.
Pamoja na kuwa kumekua na mapungufu katika serikali yake na vyombo vyake kama ilivyo kwa serikali nyingine Duniani ikiwamo ya Uingereza, Muingereza huyu amekua akitoa kashfa kwa kila jambo linaloandikwa ama kujadiliwa kuhusiana na viongozi wa Tanzania na taasisi zake na kwa kutumia lugha isiyo na staha.
Watanzania siku zote wakiwamo wanasiasa, waandishi wa habari na wanaharakati, wamekua wakiikosoa na hata kuishambulia serikali na vyombo vyake inapokosea jambo ambalo ni jema na linasaidia kuimarisha utawala bora, lakini kwa staili anayotumia Muingereza huyu ni kupitiliza mipaka na zaidi ya yote ni udhalilishaji usioweza kuvumilika kwa mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake.
Dhumuni la Sarah Hermitage na washirika wake wakiwemo baadhi ya Watanzania ni kuzishawishi nchi za Magharibi wakianzia na Uingereza kusitisha misaada na uwekezaji katika Tanzania. Hilo angeweza kulifanya huko kwao kwa kuwasiliana na serikali yake, lakini badala yake amekuwa akitumia mitandao ya kijamii na barua pepe tena kwa kutumia lugha ya kukashifu na kudhalilisha.
Watanzania wote tuna jukumu la kutetea heshima ya nchi yetu, lakini wapo wale ambao tumewapa jukumu la kusimama mstari wa mbele. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni watu wachache sana kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe ambaye ambaye amekua na ujasiri wa kumkabili Muingereza huyu, kwa kumwambia wazi kwamba kama ni misaada ana haki ya kuishawishi nchi yake kuzuia misaada kwa Tanzania lakini si kwa kudhalilisha Watanzania.
Zitto alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba nchi nyingi tajiri duniani ikiwamo Uingereza, zimejengwa kwa kutumia rasilimali walizozipora katika nchi walizozitawala ikiwamo Tanzania na kwamba nchi hizo zinaweza pia kuendesha shughuli zake bila misaada ya dharau. Bahati mbaya sana watendaji wengine wengi ambao wanapaswa kutetea heshima yetu, hili suala limewapita, pengine kutokana na kutokua na taarifa sahihi ama kwa kutowajibika.
Jambo la kujiuliza, wale ambao miongoni mwa majukumu yao ya kila siku ni kutetea na kulinda hadhi na heshima ya nchi yetu wanafanya kazi gani? Sasa tunawalipa mishahara mikubwa na marupurupu ya nini kama hawawezi kututetea tunapodhalilishwa ama kutukanwa?
Hali hii inatufanya tukumbuke ujasiri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara kadhaa aliwatunishia misuli viongozi wa mataifa makubwa walipotaka kuidhalilisha nchi yetu, sembuse raia mmoja ambaye amekua akitumia matatizo yake binafsi kutaka kuidhalilisha Tanzania na kutaka kuishinikiza serikali yake na nyingine kuichukia Tanzania.
Jinsi anavyotumia mtandao wa twitter kuchafua Tanzania
Sarah Hermitage amekua akitafuta katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania vinavyoandika taarifa zozote kuhusu Tanzania na kuziongezea maneno ya kukashifu na kejeli.
Kwa mfano amekua amechukua taarifa inayomunukuu Raia Jakaya Kikwete akiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupambana na rushwa hadi ndani ya Baraza la Mawaaziri, na yeye kuongezea maneno akisema, “kundi moja la majambazi linaliambia kundi lingine la majambazi kukamata mwizi”.
Akachukua taarifa iliyochapishwa katika vyombo vya habari ikimnukuu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikaribisha wawekezaji katika kilimo na yeye kuongeza maneno akisema, “Mheshimiwa Pinda kitakachoendelea kukandamizi uwekezaji katika kilimo cha Tanzania ni uporaji wa ardhi ya wawekezaji katika mtindo wa Mugabe (Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe).”
Amekua akidiriki kukashifu hadi majaji wote wa Tanzania kwamba wana bei akisema, “sina hakika kama unaweza kupata jaji ambaye si mla rushwa. Wote wana bei,” kauli ambayo hata Watanzania wanakua wakiitoa kwa uangalifu maana hata kama kuna majaji ambao si waadilifu, haiwezekani wakawa ni wote, kama ilivyo katika taasisi nyingine.
Raia mmoja wa Kenya anayeishi Tanzania, aliyejitambulisha kwa jina la Marigi Patrick aliandika katika mtandao kwa kusema;
“Sisi Wakenya tuna matatizo yetu na tumekua na tofauti kubwa sana za wazi wazi, lakini anapotokea raia wa kigeni kumshambulia kiongozi wetu tena kama Rais wa nchi, tunaungana na kumshughulikia. Kuna wakati Wazungu walimshambulia Rais Mwai Kibaki, sote tukisaidiwa na wabunge wetu na vyombo vya habari tulimshambulia hadi akakoma kutudharau.”
Marigi ambaye anajihusisha na biashara ya bima, anasema Watanzania bado ni wachanga katika demokrasia, ama wanadharau kila kitu bila kujua madhara yake katika hadhi na heshima ya Taifa, na ndio maana wanashindwa kutofautisha kati ya demokrasia na udhalilishaji unaofanywa na raia wa nchi nyingine kama alivyo Sarah Hermitage.

Israel yaituhumu Syria kutumia silaha za kemikali

 23 Aprili, 2013 - Saa 10:13 GMT

Mizoga ya wanyama ambao wenyeji wanasema wameuawa na silaha za kemikali
Kwa mara ya kwanza kabisa Israel imeituhumu Syria hadharani kuwa inatumia silaha za kemikali kupigana dhidi ya waasi nchini humo.
Mkuu wa idara ya utafiti wa kijasusi nchini Israel Brigadier Itai Baron ameliambia kongamano kuhusu usalama kwamba silaha hizo zimetumika mara kadhaa , ikiwa ni pamoja na shambulizi lililotekelezwa tarehe kumi na tisa mwezi uliopita wa Machi, ambalo maafisa wa Syria walisema lilitekelezwa na wanamgambo.
Amesema silaha hizo za kemikali huenda zinajumuisha sumu hatari ya Sarin.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutumika mrundiko wa silaha za kemikali zilizopo nchini humo katika mzozo uliopo nchini humo ambao unaingia katika mwaka wake wa tatu.

Mchango wa Museveni wazua mjadala

 23 Aprili, 2013 - Saa 10:05 GMT

Rais Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekabidhi kikundi cha vijana mfuko uliokuwa na dola laki moja pesa taslimu na hivyo kuzua maswali kuhusu lengo la matumizi ya pesa hizo.
Mchango huo uliotolewa ulionyeshwa wazi kwa televisheni, huku watu wakilaani hatua hiyo kwa mitandao ya kijamii.
''Kungekuwa na mfumo wa kuhakikisha kuwa vijana wanatumia vyema pesa hizo,'' alisema mdadisi mmoja kwa jina Peter Magelah.
Naye waziri mmoja alinukuliwa akisema kuwa kutoa pesa hizo kwa njia ya wazi hadharani kunaonyesha uwazi.
Museveni aliahidi kusaidia vijana wakati wa kampeini zake mnamo mwaka 2011.
Waziri anayehusika na maswala ya Rais Frank Tumwebaze, alisema kuwa Rais anaunga mkono miradi ya vijana ya kujikimu kimaisha.

Wengi walishangilia wakati Rais Museveni alipotoa mfuko huo wenye shilingi milioni 250 pesa za Uganda kabla ya kuwakabidhi waakilishi wa vijana katika eneo la Busoga.

Wakati huohuo, aliwakabidhi vijana hao basi dogo , lori na pikipiki 15.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala anasema kuwa vijana wamezoea kumuona Rais akitoa pesa hadharani hasa katika hafla za hadhara.
Lakini kilichowashangaza wananchi wengi ni kiasi cha pesa zilizotolewa na picha inayomuonyesha Museveni akishikilia mfuko wenye pesa.
Waganda wengi wanaotumia mtandao wa kijamii wa Twitter, wamekuwa wakitoa maoni yao, kuhusu kitendo cha Rais.
Bwana Peter Magelah, amesema kuwa hizi tu ni mbinu za kisiasa za Rais Museveni kujipatia umaarufu.
"je tunafahamu vipi pesa hizo zitatumiwa, hakuna njia ya kuhakikisha zimetumiwa ipasavyo.Hakuna njia ya kuhakikisha kuwa kuwa pesa hizo zitarejeshwa ikiwa zitatumiwa vibaya. Ni hasara kubwa kwa nchi.''

Ubalozi wa Ufaransa Libya washambuliwa

 23 Aprili, 2013 - Saa 09:39 GMT

Bomu limelipuka nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuwajeruhi walinzi wawili huku ikisababisha uharibifu mkubwa.
Mlipuko huo ulisababisha uharibifu katika sehemu moja ya ofisi hizo na pia kuharibu nyumba jirani.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli, Rana Jawad anasema kuwa inaaminika kuwa mlipuko huo ulisababishwa na gari lililokuwa na mabomu.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, aliitaka serikali ya Libya kuchukua hatua za haraka kukabiliana na waliosababisha shambulio hilo.
Aliongeza kwamba shambulizi hilo lililenga nchi za kigeni zinazopambana dhidi ya ugaidi.
Balozi za kigeni nchini Libya zimewahi kushambuliwa katika siku za nyuma, lakini hili ndilo shambulizi la kwanza kubwa dhidi ya ubalozi wa kigeni mjini Tripoli.
Shambulizi liliwahi kufanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi mwezi Septemba mwaka jana na kusababisha kifo cha balozi Christopher Stevens pamoja na maafisa wengine wamarekani .
Shambulio la leo lilifanyika muda mfupi baada ya saa kumi na moja asubuhi katika mtaa wa kifarahari mjini Tripoli.
Wakaazi wa eneo hilo walighadhabishwa sana na shambulizi hilo na kulalamikia ukosefu wa ulinzi mzuri wa sehemu hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Libya, Mohammed Abdel Aziz alilaani vikali shambulizi hilo, ingawa hawajaeleza ni nani wanayemshuku kulifanya.