Thursday, April 25, 2013

TRAFIKI AKABWA KOO.... POLISI WALAANI NA KUDAI WAMEDHALILISHWA


Siku moja baada ya kituo cha ITV kuonesha mzozo uliosababisha askari wa usalama barabarani kuwa katika wakati mgumu kutokana na kukunjwa na raia wakati akiamua ugomvi baina ya madereva wawili baada ya kutokea ajali , jeshi la polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni limelaani na kutoa onyo kali na kuongeza kuwa tukio hilo limelidhalilisha jeshi la polisi na kwamba halivumiliki.


  

VURUGU ZA LINDI: NYUMBA 15 ZA VIONGOZI WA CCM ZIMECHOMWA NA MIFUGO YAO IMEKATWA MAPANGA NA WANANCHI



Nyumba zaidi ya saba za kuishi na nane za maduka pamoja na mifugo; vyote vikimilikiwa na viongozi wa CCM, akiwamo mbunge na madiwani wilayani Liwale, vimeteketezwa kwa moto na kuharibiwa na wahalifu.

Mali hizo zikiwamo za viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Liwale, vimeteketezwa kwa kilichdaiwa kuwa ni kupinga kulipwa malipo kidogo ya korosho, msimu wa mwaka jana.


Taarifa ya Polisi, ilisema jana kuwa watu wanaodhaniwa kuwa wakulima wa korosho, walijaribu kuzuia gari lililokuwa na malipo ya korosho, wakipinga malipo ya pili ya zao hilo na kufanya vurugu na uharibifu wa mali.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alionesha wasiwasi bungeni  akisema huenda kuna baadhi ya watu, wakiwamo wanasiasa walio nyuma ya matukio hayo ili kuficha uovu wao na wengine kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
 
Waliochomewa nyumba katika vurugu hizo, ni Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Liwale, Mohammed Mngomambo,  Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya, Abdallah Chande na Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ilulu, Hamza Mkunguru. 

Wengine walioathiriwa na vurugu hizo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Diwani wa CCM, Abas Mtalilo ‘Chigogola’ na madiwani wenzake,  Hassan Myao, Musa Mkoyage, Mzee Salehe na Amina Mnoche.
 

  Akizungumza na mwandishi jana, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Hemed Ndimane alisema duka lake la vyakula lilivamiwa na mali zote kuporwa. Ng’ombe watano waliouawa kwa kukatwa mapanga, ni mali ya  Mkunguru. 
 
Naye Mitambo alisema nyumba zake mbili zilichomwa moto huku moja ikiteketezwa kabisa, nyingine ikibomolewa paa na kunyofolewa milango na madirisha.

Mbunge huyo alisema Chigogola alichomewa nyumba ya vyumba 11, pikipiki mbili, trekta dogo ‘power tiller’ na ng’ombe wake 12 waliuawa.
 
 Alisema Mngomambo alichomewa nyumba kama alivyofanyiwa Chande; sawa na madiwani wote wa kata za mjini Lindi. 
 
Ingawa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema atatoa taarifa baadaye, lakini taarifa ya makao makuu ya Polisi, Dar es Salaam, ilisema mpaka jana watuhumiwa 19 walikuwa wamekamatwa kwa mahojiano. Vurugu hizo zilizoanza juzi asubuhi, eneo la Liwale ‘B’. 


Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Ulenga, Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana jana baada ya tukio hilo huku Kamanda akisisitiza kuwa hadi jana mchana walikuwa wakiendelea na vikao, kabla ya kutoa taarifa kamili kwa vyombo vya habari.
 

 Ulenga alisema wananchi hao walivamia maduka na nyumba za viongozi hao na kuziteketeza kwa moto, kutokana na madai kwamba walipata malipo ya pili ya Sh 200 badala ya Sh 600 kwa kilo.
 

 “Lazima tufahamu ni kwa nini, kama mauzo yalikuwa Sh 1,100 kwa kilo, wataalamu wanatakiwa watoe maelezo juu ya malipo hayo yaliyofanywa Liwale,” alisema Ulenga.
 

 Bei ya korosho kwa kilo ilikubaliwa kuwa Sh 1,200 kwa kilo, lakini baada ya kushuka kwa bei katika soko la dunia, ilishuka na kuwa kati ya Sh 1,000, Sh 1,070 na 1,100.
 

 Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Lindi, Killian Kapamba alisema hajui kama vurugu hizo ni za ununuzi wa korosho au za kisiasa, kwa kuwa mali za viongozi wa kisiasa ndizo zilizoharibiwa.
 

 Alisema inakuwa vigumu kubaini sababu za vurugu hizo kwa kuwa pia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Umoja, ambacho ndicho chenye jukumu la kutoa malipo hayo, kilikuwa hakijaanza kutoa malipo ya pili kwa wakulima na wanachama.
 

 Hata hivyo, taarifa kutoka Polisi zilisema baadhi ya viongozi waliodaiwa kuhusika na uchochezi huo, wamekamatwa.
 

Akizungumza bungeni jana, Malima alieleza kusikitishwa na vitendo vya wananchi kuchukua hatua mkononi na kuharibu mali bila kutoa fursa ya matatizo yao kushughulikiwa.
 

 Malima ambaye alionesha wasiwasi wa wanasiasa kuwa nyuma ya vurugu hizo, alisema hayo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu,  Zainabu Kawawa (CCM), kuliwasilisha suala hilo bungeni.
 

 Zainabu wakati akitoa hoja hiyo, aliitaka Serikali kutengeneza  utaratibu utakaowezesha wakulima hao kulipwa fedha wanazodai, ambazo ni Sh 400 walizopunjwa katika malipo ya korosho.
 

 “Naomba nieleze masikitiko yangu juu ya tukio la jana (juzi) usiku katika wilaya ya Liwale…wakulima wa korosho wameghadhabika na kuamsha mapambano  kati yao na polisi, hadi kusababisha uharibifu wa mali zikiwamo nyumba za viongozi,” alisema Kawawa.
 

Alisema wakulima hao walichukua hatua hiyo, baada ya kutotimiziwa malipo ya korosho ya Sh 1,200 kwa kilo. Alisema awali walilipwa Sh 600 tu, baadaye wakapewa Sh 200 na hadi sasa hawajamaliziwa Sh 400 zilizobaki.
 

 “Kwa maana hiyo wakulima hao walilipwa Sh 800 tu, wanachodai ni tofauti ya Sh 400, nimezungumza na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika amenieleza kuwa bei ya korosho imekuwa ikibadilikabadilika,” alisema Zainabu.
 

 Aliiomba Serikali iingilie kati mgogoro huo kwa kuahidi kama inaweza kufidia Sh 400, ili mkulima wa korosho alipwe Sh 1,200.


Akijibu hoja hiyo, Malima alisema: “Hii lazima tukubaliane kuwa kuna vitu vimejificha humu, sehemu zote ambazo zinalimwa korosho ikiwamo Mkuranga, kuna matatizo ambayo yanasababisha korosho kutouzwa na matatizo haya hayalingani kote, yanatofautiana,” alisema.
 

 Alisema kwingine matatizo ya wakulima wa korosho yanatokana na vyama vya ushirika wakati kwingine kuna matatizo ya wanunuzi. 



“Sasa mimi nashangaa kwa nini vurugu za namna hii zinaibuka? Kuna sababu nyingi, pengine hata hawa viongozi wa ushirika wanahusika ili kuficha maovu yao au hata tu masuala ya kisiasa,” alisema Malima.
 

 Kutokana na vurugu hizo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, ametuma timu maalumu ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Issaya Mngulu, kwenda kuongeza nguvu mkoani humo kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa.
 

 Timu hiyo imetakiwa kuhakikisha hali ya amani na utulivu inarejea haraka na waliohusika na uhalifu, wanakamatwa na kufikishwa mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake.

Maelfu ya watoto kuchanjwa Somalia


Somalia ina idadi kubwa ya vifo vya watoto duniani
Mpango wa kutoa chanjo kwa zaidi ya watoto milioni moja nukta tatu umezinduliwa nchini Somalia.
Chanjo hiyo itakuwa ya kukinga watoto dhidi ya aina tano ya magonjwa ikiwemo Homa ya mapafu, Hepatitis na ugonjwa wa uti wa mgongo.
Shirika la afya duniani ndilo linatoa chanjo hizo kwa ushirikiano na shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.
Somalia ni moja ya nchi zenye mpango duni wa kutoa chanjo kwa watoto pamoja na kuwa nchi yenye idadi kubwa ya vifo vya watoto duniani.
Wataalamu wansema kuwa mmoja kati ya watoto watano, hufariki kabla ya kufikisha miaka mitano hali inayotokana na mfumo mbaya wa afya ambao umezoroteshwa na otovu wa usalama.

30 wauawa baada ya jengo kuporomoka Bangladesh


Watu wengi wanahofiwa kukwama ndani ya vifusi
Vikosi vya uokoaji vinasema, watu wapatao 30 wamefariki dunia na mamia wengine wanahofiwa kukwama baada ya jingo la ghorofa nane kuporomoka katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
Juhudi za ziada zinaendelea kuwaokoa watu walionaswa kwenye kifusi. Watu wapatao 200 wamejeruhiwa kufuatia ajali hiyo. Jeshi linasaidia shughuli za uokoaji katika eneo la tukio nje kidogo ya jiji la Dhaka.
Matukio ya majengo kuporomoka nchini Bangladesh ni ya kawaida kutokana na majengo mengi marefu kujengwa kinyume na sheria za ujenzi.
Jengo lililoporomoka lilikuwa na kiwanda cha nguo, benki na maduka kadhaa. Liliporomoka asubuhi wakati watu wakielekea makazini.
Watu wengi wamekusanyika karibu na eneo la tukio wakiwatafuta ndugu na marafiki. Mwandishi wa BBC mjini Dhaka anasema haijafahamika kilichosababisha jengo hilo kuporomoka, lakini vyombo vya habari nchini humo vimearifu kwamba, nyufa zilionekana kwenye jengo hilo siku ya Jumanne.
Polisi wameviambia vyombo vya habari kwamba, waliona ghafla sehemu ya nyuma ya jengo hilo ikianguka Jumatano asubuhi na baada ya muda mfupi jengo lote likafuatia isipokua nguzo kuu na sehemu ya ukuta wa mbele hali iliyosababisha taharuki.
Maafisa wanasema, ni sehemu ya chini pekee ya jengo hilo la Rana Plaza ndio ilibakia imara baada ya kuporomoka, wakati wanajeshi na waokoaji wa idara ya zimamoto wakiwa na vifaa vya kukatia vyuma na matingatinga wakifukua kifusi ili kuwaokoa watu walionaswa .
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Mohammed Asaduzzaman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, hali ilikua mbaya sana.
Novemba mwaka jana, moto uliounguza kiwanda cha nguo nje ya jiji la Dhaka uliua watu 110 na kusababisha wananchi kupigia kelele kuhusu viwango vya usalama kwenye viwanda husika.

Mara mwisho jengo la ghorofa nne liliporomoka jijini Dhaka mnamo mwaka 2010 na kusababisha vifo vya watu 25 na wengine kadhaa kujeruhiwa.