Huu ndio mtazamo wa ndugu Zitto kwa ufupi juu ya suala la Mtwara.

Zitto Kabwe:


Serikali iangalie upya namna inavyolitazama suala la Mtwara. Hivi sasa suala hili linaonekana kiusalama zaidi badala ya kuliona kama suala la kijamii na maendeleo lenye kuhitaji kujenga imani ya wananchi.

Suala hili linahitaji muda na heshima kwa wananchi. Ni vema tuache sauti ya wananchi kusikika na kuzitolea maamuzi sahihi yenye kujenga kuaminiana na kuheshimiana kati ya dola na wananchi.

Suala la Mtwara ni zaidi ya gesi asilia. Ni matokeo ya kutengwa kimaendeleo kwa muda mrefu. Suala la Gesi ni nafasi ya kuunganisha watu wa kusini na Jamhuri ya Muungano. Tuamue sasa kufanya maamuzi sahihi na kuunganisha Jamhuri yetu au kukosea na kudharau na kuivunja Jamhuri yetu.

Kama Kuna mataifa ya kigeni/makampuni binafsi yanahusika na hali ya Mtwara. Serikali iyataje mataifa hayo na makampuni hayo hadharani na vibaraka wao.Vinginevyo nadharia hizi zitaonekana ni ni propaganda tu kwa lengo la kufunika kombe mwanaharamu apite.

Nadharia zote za kuelezea masuala ya Mtwara zinakimbia suala la msingi ie kutengwa kwa muda mrefu sana kwa mikoa ya kusini kwenye maendeleo ya nchi. Ahadi za Rais Ben Mkapa kuhusu Mtwara Corridor, ahadi za Rais Jakaya Kikwete za 2005 na biashara ya korosho ni miongoni mwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtwara. Suala hili la msingi lazima lipatiwe majawabu mwafaka kwa maelezo yenye heshima kwa wananchi badala ya dharau na vijembe dhidi ya raia.

Kuna kukosa imani kukubwa kwa wananchi dhidi ya Serikali. Suala hili ni pana zaidi na linasambaa Tanzania nzima. Malalamiko yanaposhawishiwa kihofu tu huleta matatizo makubwa sana. Hali ya namna hii haijawahi kutokea nchini mwetu. Kukamata na kufunga viongozi wa wananchi haitosaidia kamwe.

Kutumia nguvu ya dola kuzima vuguvugu la wananchi sio njia pekee ya kujenga amani. Makovu ya kutumia nguvu ya dola huchukua muda mrefu sana kupona. Lazima kubadili mkakati wa kuongoza na kuliweka Taifa sawa.

Zitto Zuberi Kabwe (Mb)
24th May 2013


Nimeambatanisha nakala ya hotuba yake ya "Mtwara wanauliza Mtatuachaje?" iliyotolewa Tabora. Hotuba hiyo imezungumzia kwa kina suala la Gesi Mtwara na hivyo kutoa elimu zaidi juu ya suala hilo la Gesi.

HOTUBA TABORA|Mei 24, 2013

  • Nchi yetu ni tajiri lakini wananchi wake ndiyo masikini kutokana na sera mbovu za CCM.
  • Geita ndiyo ina mgodi mkubwa kuliko yote barani Afrika, (baada ya Ghana na Afrika Kusini) lakini ndiyo mji masikini Tanzania.
  • Wallahi naomba 2015 ifike hara tuwaweke CCM pembeni manake vinginevyo nchi hii itakuwa imeuzwa yote!K
  • Kenyatta anaongelea kila mwanafunzi kuwa na Laptop, siye tunaongelea nani Achinje!
  • CCM walisema CUF cha Waislam, Chadema cha Wakristo. Sasa CCM ni cha nani? Cha wapagani? Tusikubali kugawanywa!


Hatuwezi kukubali hali hii.. Na ni lazima watu wa Tabora muwe na Hasira. Lakini hali ya umasikini limekua zaidi ndani ya nchi yetu.

Nchi ni tajiri sana wananchi wa Tabora. Asije mtu akawadaganya kwamba Tanzania ni nchi maskini! Tanzania ni nchi tajiri yenye watu masikini na Siyo nchi maskini. Nchi yetu ni tajiri lakini wanachi wake ndiyo masikini kwa sababu ya sera mbovu za Chama cha Mapinduzi

Mungu ametupa kila kinachotakiwa kuwa kwenye Utajiri! Kila kitu! Sijui wajerumani waliongozwa na nini… Kwa Sababu wajerumani walipokuja na kuipata hii Tanzania, walipata kila kitu.

Kila kona ya nchi hii ina utajiri wake. .. Kwenda Kanda ya Ziwa ni dhahabu na almasi zimejaa.. Yamegunduliwa madini ya Nickel ambayo yanatumika kutengeneza ndege kule Ngara Kagera; ndio sisi (Tanzania) tuna madini ya namna hiyo mengi zaidi kuliko nchi zote duniami!

Ukienda huko mpanda kuna shaba, kuna makaa ya mawe. Ukienda Songea kuna Uranium kuna makaa ya mawe. Kuna Chuma Cha Liganga kule Rudewa mkoa wa Songea mpya

Sasa Gesi ndio usiseme! Tumegundua gesi nyingi sana. Mtwara, Lindi na Pwani. Mafuta yamejaa Ziwa Tanganyika. Hakuna jambo ambalo Mungu hajatupa katika nchi hii. Lakini leo katika kila watanzania 100 wa Tanzania 35 wanaishi katika hali ambayo hawawezi kupata mlo mmoja kwa siku. Asilimia 35 ya Watanzania!

Jana kulikuwa na seminar kule bungeni. Kuhusu sera ya gesi asilia. Wametugaia sera siku ya Ijumaa, Jumamosi Seminar. Na kwa style za CCM ile seminar ni wabunge wamepitisha. Yaani wataenda huko kwenye majukwaa na watasema “Sera hii imeshirikisha wadau na wabunge wamepitisha”. KWA SEMINA TU. Wabunge wanaishia kwenye seminar wanapigwa laki mbili mbili za posho, kisha wanasifia sifia pale wanapitisha hiyo sera na ndiyo Imetoka hiyo!

Watu wa Mtwara wanalia kila siku. Watu wa Mtwara wameandamana mpaka wakachukua hatua ambazo si za kisheria za kuchoma nyumba za watu sababu ya gesi. Serikali, Rais, Waziri, mkuu wa Mkoa wanasema watu wa Mtwara wajinga hawa… Wenyewe walivyokuwa wanafaidi matunda ya Watanzania wengine mbona Watanzania wengine hawakulilia Kahawa? Pamba?

Lakini waziri alisahau. Kwamba Mtwara ilikuwa inazalisha korosho… Asilimia 80 ya korosho ilikuwa ikitoka Mtwara. Na ndio zao la pili kwa fedha za kigen baada ya Tumbaku ya Tabora.

Watu wa Mtwara walikluwa wakiuliza tu “Mtatuachaje??” “Gesi imepatikana lakini mnatuachaje??” Hilo tu! Serkali ikataharuki! “Kuwa watu wabinafsi hawa” Serkali ya CCM imechoka kabisa. Imechoka!

Sababu watu wa Mtwara wameona… Watu wa Mwanza walivyo nyonywa kwenye dhahabu. Wameona watu wa Shinyanga walivyonyoshwa kwenye dhahabu. Wameona watu wa Tabora mlivyonyonywa kwenye dhahabu.

Tabora, Nzega kuna mgodi unaitwa resolute, Golden Pride. Ule Mgodi umekaa toka 1997, Mkataba wake ulisainiwa hapo Tabora Hotel sassa hivi panaitwa Orion. Ule mgodi dhahabu imekwisha. Wameuza nje dhahabu ya thamani ya dola Billion 3 kwa muda waliokaa hapo toka mwaka 1997 mpaka 2012… Hizo ni trillion 5 na zaidi. Lakini leo hali ya Nzega ni ile ile kana kwamba hakukuwa na dhahabu Nzega…

Watu wa Mtwara wameona hilo!

Shinyanga kuna Migodi miwili katika wilaya moja ya Kahama. Mgodi wa Bulyanhulu na mgodi wa Buzwagi. wAtu wa Shinyanga hawajafaidika na na migodi hiyo. Mgodi wa Buzwagi dhahabu inaisha ndani ya miaka miwili. Ya Bulyanhulu wenyewe utaenda hadi 2032, lakini watu wa Shinyanga hawajaona faida ya dhahabu.

Watu wa Mtwara wameona hilo!

Geita, (sasa hivi ni mkoa wa Geita kwa hiyo siyo Mwanza tena) ni mmoja wa wilaya masikini zaidi katika Tanzania, lakini ndiyo ina mgodi mkubwa wa dhahabu katika bara la Afrika lakini ndio wilaya masikini zaidi Tanzania. Wanazalisha wakia za dhahabu, kule Kigoma tunaita tola, Kwa kiingereza wanaita ounces (million 1 kwa mwaka). Lakini Geita ni moja ya willaya masikini Tanzania.

Mtwara waliona hilo!

Kwa hiyo gesi ilivyogundulika kule… Serkali jambo la kwanza ilisema tunajenga bomba toka Mtwara mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kuzalisha umeme. Hamna ubaya kuzalisha umeme… Tunatumia gharama kubwa sana kuzalisha umeme hapa nchin. Tunaagiza mafuta mengi sana kutoka nje kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Bei ya umeme wa Maji ni cent 2 za dola kwa kila unit moja. Bei ya umeme wa gas ni senti 6 za dola kwa kila uni moja. Bei ya umeme kwa diesel ni senti 42 za dola kwa kila unit 1. Kwa hiyo haina shida , kuzalisha umeme kwa gas ni nafuu zaidi kuliko kuzalisha kwa mafuta,

Lakini watu wa Mtwara wakasema “huu umeme hauwezi kuzalishwa Mtwara hadi ukapelekwa Dar? “ Swali Lao ni hilo tu! “Je gharama za kujenga bomba toka Mtwara hadi Dar es Salam?, na gharama za kujenga Mitambo ya umeme Mtwara mkasafirisha umeme hadi Dar es Salam zipoje? Sie tungependa uzalishwe hapa” Serikali ikachanganikiwa “Wasaliti nyie, sio wazalendo n.k” wakawatukana wana Mtwara, kwa kuuliza,, Kwa kuwahoji.

Lakini Mtwara wakasema sisi hatutaki yatukute kama yaliyowakuta wa Nzega, Hatutaki yaliyowakuta wa Geita, hatutaki yaliyowakuta wa Kahama. Kahama pale Bulyanhulu watu walifukiwa kwenye mashimo.. Geita leo bado mpaka kuna watu wanaishi mahakama ya mwanzo kama wakimbizi ndani ya nchi yao, kwa sababu eneo lao ambalo wawaliokuta dhahabu wakaondolewa wakaambiwa nyie hamna mahali pa kukaa.. Mtwara wanasema “Mnatuachaje?”

Sasa wameleta sera ya gesi juzi bungeni… Mie nikai chek, na kusema hawa watu hawapo serious! Sera ile inasema ya kwamba gas inapovunwa – sera haihusiki. Sera inahusika na uchuuzi . Yaani ni hivi… Serkali ije iseme haihusiki na namna ambavyo mkulima anavyolima tumbaku ila inahusika na namna ile Mkulima yule anavyoisafirisha ile tumbaku toka Urambo mpaka Tabora. Yaani kwenye uchuuzi, siyo uzalishaji.

Nikawaambia, haiwezekani… Kama mna nia ya kuwa na sera madhubuti, lazima muanzie kwenye utafutaji.. Uje kwenye uchimbaji… Uje kwenye usafirishaji. Sera ile inakataa haya.

Lakini hii ni kwa sababu tayari wameshaingia kwenye mikataba mibovu na chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo wanaogopa makampuni ya wazungu kuwainglia kwenye hiyo mikataba. Lakini baya zaidi watu wa Tabora niwaambie wakati tunatengeneza Sera.. na baadae tutengeneze sheria…

Tayari Chama Cha Mapinduzi kimesha anza kuuza vitalu vipya vya mafuta na Gesi Tanzania. Sasa unauza Vitalu wakati Sera hakuna? Unauza Vitalu wakati sheria hakuna? Watu wa namna gani sisi? Hawa watu wamelogwa na nani? Wallahi naomba 2015 ifike hara tuwaweke pembeni manake vinginevyo nchi hii itakuwa imeuzwa yote!

Kila kona ya nchi hii ina utajiri… Tatizo letu ni namna utajiri huu unavyo endeshwa … Ndiyo tatizo letu Tanzania. Na ndiyo maana tunataka Watanzania wote muungane pamoja! Ili tuweza hakikisha ya kwamba, tunakwenda mbele.

Ssa hivi nchi yetu ipo kwenye hatari. Hatari kubwa tuliyio nayo ni kuwa tayari tumeingizwa kwenye sumu ya udini. Leo hii Watanzania wanaanza kuangaliana kwa dini zao. Wanaanza kuangalia ,,, Enhee wameteuliwa wakuu wa Wilaya, waislamu wangapi na Wakristo wangapi? Wameteuliwa mawaziri.. Enhee Wakristo wangapi na Waislamu wangapi? Imeteuliwa Tume ya Katiba Enhee Waislamu wangapi na Wakristo wangapi? Hazijawahi kuwa hivyo hata siku moja! Tunagawanywa hivyo sababu mataifa makubwa wanataka tupigane waje wanyonye gas, wanyonye mafuta,wabebe dhahabu wajiondokee zao! Ndio wamefanya hivyo Nigeria, Ndio wamefanya hivyo Sera Leione, Ndio wamefanya hivyo jirani zetu wwa Congo.

Tukikaa vibaya … Na midomo mibaya ya sisi wana Siasa Mtagawanyika nyie! Leo hii rais wa Kenya… Uhuru Kenyatta anazungumzia kila mtoto wa Kenya kupewa Computer anapo anza darasa la Kwanza. Tanzania tunazungumzia nani achinje! Ndipo tulipofika… Na Watanzania nyie mnapenda mambo madogo madogo haya… Mambo madogo madogo ndiyo mnayo yapenda; Nani achinje? Miaka yoote hii mbona tulikuwa hatuulizani nani achinje? Kwa nini tuulizane leo?

Nchi yetu itakuwa ya tatu kwa uzalishaji wa Uranium ifikapi mwaka 2015. Ambayo inatumika kutengeneza mabomu ya Nuclear. Nchi yetu itakuwa miongoni mwa nchi yenye gas nyingi zaidi duniani. Nchi yetu ni ya tatu kwa uzalishaji wa Dhahabu Afrika. Kwa hiyo wageni wanafahamu, nani achinje? Mnapigana huko nani achinje, wanabeba Gas, wanabeba dhahabu, wanabeba Tanzanite, wanabeba kila aina ya kitu wanachotaka kubeba.

Msiwe wajinga… Msikubali kugombanishwa na sisi Wanasiasa. Msikubali masuala ya udini yanapenywezwa makusudi, ili tugombane tusiwa na mshikamano,.

Wakati wa Kampeni Kigoma mwaka 2010, nilienda kwenye Kijijini, Nikakuta mgombea wa CCM amewaambia watu msimchague huyu Muislam, nichagueni mimi Muanglikana mwenzenu. Nikawaambia wale watu wa Batiazo, hivi wakati mimi nachaguliwa hapakuwa na bara bara Kigoma, toka Malinzi mpaka mjini. Leo kuna bara bara hii………… Ile bara bara wanapanda Waislamu peke yao? ( Wakajibu hapana) Wanapanda wakristo peke yao? (Wakajibu hapana) Kwa nini mchague tokana na dini ya mtu?

Lakini leo hii nyinyi kila mtu ajiulize toka moyoni mwake hapa… Kuna mbegu mbaya chafu ya udini inapandwa.. Tusikubali… Tusikubali! CCM walikuwa wanatumia mbegu hii ya Udini kwa ajili ya kutugawa wapiga kura; 2005 walisema CUF chama cha Udini na Waislam, mwaka 2010 wakasema Chadema chama cha Udini na Waislamu (Samahani) Chamba cha Wakristo.

CUF cha Waislam, Chadema cha Wakristo. Sasa CCM ni cha nani? Cha wapagani? Hayo ndiyo mambo ambayo Watanzania inabidi tujiulize! Tusikubali kugawanywa!

Mtu anasali msikiti gani ama kanisa gani haituhusu! Tunachotaka ni kila mtu apate haki yake bila kujali Dini yake! Kama wewe ni kijana wa Tanzania Mkrito unaomba kazi, upate kazi tokana na vyeti vyako! Siyo kutokana na dini yako! Kama wewe ni kijana Mtanzania Muislamu, umeomba kazi upewe kazi tokana na vyeti vyako, siyo kutokana na dini yako.

Tusikubali ifike huko! Na niliwaambia Bungeni, kwamba Hamna sababu ya kutafutana lawama. Leo hii tukisimama CCM wanasema Chadema ni wadini, Chadema nao tunanasema CCM in wadini! Mnamsaidia nani? Viongozi lazima tukae chini wote tuseme hapana! Muelekeo huu wan chi si mzuri! Tukaeni chini.. Ndio busara hizo. Busara si kurushiana lawama. Mkirushiana lawama mnazidi kugawanyika tu! Chadema ikisimama ikasema Udini umesababishwa na CCM, CCM nao wakisimama Udini umesababishwa na Chadema , tutafika wapi? Kutakuwa na suluhisho? Tutapata jawabu?

Majawabu ni kuwa sisi viongozi wa Siasa, Wa Chadema, wa CUF, Wa CCM laziam tukae chini kujasema huko tunakokwenda, mitaani kwenu… Hali uliyokuwa unaishi na jirani wako hapo nyuma (kwa amani) ndiyo hali inabidi irudi na iwe hivyo! Inapaswa tutumie Busara kuiokoa Tanzania yetu! Ni wajibu wetu sote...

(Mwisho)