Wednesday, June 5, 2013

Wasomali watafakari juu ya kuwepo kwa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia

Kwa kumbukumbu ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU) iliyoadhimishwa mwaka huu 2013, Wasomali wengi walitoa shukrani kwa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) -- kikosi kilichosaidia kuwaondoa al-Shabaab Mogadishu na kudhoofisha udhibiti wa kikundi hicho cha wanamgambo kwenye nchi hiyo.
    Askari wa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) akisimamia sheria za barabarani katika barabara ya Mogadishu wakati wa operesheni tarehe 25 Mei ambayo ililenga kuboresha usalama katika mji mkuu huo wa Somalia. [Tobin Jones/AU-UN IST/AFP]
  • Askari wa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) akisimamia sheria za barabarani katika barabara ya Mogadishu wakati wa operesheni tarehe 25 Mei ambayo ililenga kuboresha usalama katika mji mkuu huo wa Somalia. [Tobin Jones/AU-UN IST/AFP]
"Tunawashukuru sana AMISOM kwa sababu walituokoa kutoka kwa al-Shabaab," Mkaazi wa Mogadishu Aweys Isse, mwenye umri wa miaka 26, aliiambia Sabahi. "Kwa hakika, wameleta amani na kutuwezesha kupumzika; mji mkuu wetu haukuwahi kuwa katika amani kama ilivyo sasa katika miaka 22."
Vikosi vya Afrika vilifanya jukumu kubwa la kurejesha amani nchini Somalia na kufanikisha misheni ambayo hakuna kikosi kingine cha kigeni kingeweza kufanya, alisema.
"Jiji hili limekuwa na matatizo mengi, lakini leo hii ninaweza kuhisi utulivu," alisema Nadifa Ali, mwenye umri wa miaka 50 mama wa watoto 11 ambaye anauza mirungi huko Beledweyne. "Ninafanya kazi kwa ajili ya watoto wangu na sina hofu kuhusu watoto wangu [usalama] kama ilivyokuwa wakati al-Shabaab walipokuwa wanatawala hapa."
Vikosi vya AMISOM viliingia kwa mara ya kwanza Somalia mwaka 2007. Kimsingi kazi ya misheni hiyo ilijikita katika kulinda amani, lakini vilianza shughuli Mogadishu wakati al-Shabaab ilipokuwa katika kukaribia kuishinda serikali ya mpito ya Somalia. Vikosi vya Afrika vilivisaidia vikosi vya Somalia kuwaondoa al-Shabaab kutoka katika mji mkuu mwezi Agosti 2011 na kuendelea kufanya kazi ya kupunguza ushawishi wake katika majimbo.
Mahi Sufi, mwenye umri wa miaka 32, mwangalizi wa msikiti huko Baidoa, alikumbuka miaka kabla vikosi vya AMISOM na Somalia kuukomboa mji wake kutoka utawala wa al-Shabaab.
"Al-Shabaab ilitutishia na kutufanya kukosa uhuru," aliiambia Sabahi. "Walilazimisha mtazamo wao wa Uislamu kwetu bila ya kuelekeza tabia zao katika kanuni halisi za Uislamu."
"Sasa hivi tuko huru kusoma vitabu vya dini yetu bila ya kumhofia yeyote isipokuwa Mungu," alisema.
Hata hivyo, Abdiaziz Dayah, mwenye umri wa miaka 49, mwalimu wa sekondari ya juu Mogadishu, alisema baadhi ya shughuli za AMISOM zimesababisha matatizo pamoja na mazuri. Tukirejea mashambulizi dhidi ya raia katika mapambano dhidi ya al-Shabaab, alisema AMISOM lazima "wawajibike kwa watu waliowauwa".

Suluhisho la Afrika kwa matatizo ya Afrika

Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Somalia Hussein Farah alisema nchi za Afrika zimepata uzoefu mkubwa kwa kupeleka vikosi vyake Somalia, na kufaulu kwa misheni ya kulinda amani ya AMISOM ni mfano ambao unaweza kuigwa katika sehemu nyingine za bara, kama vile nchini Mali.
"[Nchi za Afrika] lazima zitafute ndani yake suluhisho kwa matatizo ya Afrika na nchi zilizobakia duniani kutoa msaada tu," Farah alisema.
Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa ajili ya Somalia Mahamet Saleh Annadif alitathmini operesheni ya AMISOM ya sasa kuwa ni mafanikio.
"[Ushiriki wa AU huko Somalia] ulikuwa ni uamuzi uliofanywa na Afrika kutatua tatizo barani Afrika, na tumefanikiwa katika operesheni hii ambayo iliendeshwa na vikosi vya Afrika tu bila kuvihusisha vikosi vya Umoja wa Mataifa kama zilivyo operesheni nyingine za AU," aliiambia Sabahi.
Kimsingi, Somalia, ilikuwa ni miongoni mwa nchi wanachama waanzilishi wa Shirika la Umoja wa Afrika -- jina asilia la Umoja wa Afrika -- ambalo lilianzishwa huko Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 25 Mei, 1963.
Huku ikiingia katika miaka yake ya 51, AU ina matumaini ya kutimiza hata zaidi kushughulikia matatizo yanayoikabili Afrika.
Lakini wachambuzi kama vile Abdikarim Daud, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Mogadishu, alikuwa na wasiwasi kama umoja huo una uwezo wa kutimiza malengo makubwa.
"Umoja wa Afrika bado hauna uwezo wake binafsi wa operesheni za kusimamia uletaji amani katika nchi kama vile Somalia," alisema, akiongeza kwamba gharama za uendeshaji za AMISOM zinalipwa na Umoja wa Mataifa.
"Hata hivyo, [nchini Somalia] wametimiza jambo walilokuwa hawawezi kulifanya kabla kwa kushughulikia kwa mafanikio tatizo ndani ya Afrika kwa kuzingatia uamuzi wa AU," Daud, aliyekuwa kanali katika Jeshi la Taifa la Somalia, aliiambia Sabahi.
"[AU] ilikuja kuisaidia Somalia wakati ambapo dunia nzima haikuizingatia Somalia na ilifanikiwa katika kurejesha kwa kiasi fulani utulivu," alisema.

No comments:

Post a Comment