Wednesday, June 5, 2013

Wakaazi wa Mogadishu wapokea kwa furaha, waahidi kulinda taa za barabarani za nguvu ya jua

Kadiri utawala wa mkoa wa Benadir unavyojiandaa kufunga taa za barabarani zinazotumia nguvu ya jua kwenye barabara 30 katika wilaya nne za Mogadishu, maofisa walizindua kampeni ya kuuelimisha umma kwa wakaazi kutunza taa hizo.
    Mafundi wakifanya kazi ya kufunga taa za nguvu ya jua katika barabara ya Maka al-Mukarama huko Mogadishu. Wakaazi wasema taa hizo zinawakumbusha fahari ya zamani ya mji mkuu wa Somalia. [Mustafa Abdi/AFP]
  • Mafundi wakifanya kazi ya kufunga taa za nguvu ya jua katika barabara ya Maka al-Mukarama huko Mogadishu. Wakaazi wasema taa hizo zinawakumbusha fahari ya zamani ya mji mkuu wa Somalia. [Mustafa Abdi/AFP]
Manispaa ya Mogadishu inapanua programu yake ya kuweka mwanga katika mji mkuu kwenye barabara kubwa nyakati za usiku, kutoa fursa kwa biashara kuendelea kuwa wazi nyakati za usiku na kusaidia raia kuhisi salama.
Barabara zilizolengwa kuwekewa taa mpya ni zile za upili katika maeneo ya wakaazi ya wilaya za Warta Nabada, Hodan, Howlwadag na Yaqshid. Kipaumbele kitatolewa kwa wilaya nne kutokana na usalama ulioboreshwa kwani sehemu kubwa ya wakaazi wanarudi nyumbani kwao katika maeneo hayo, kwa mujibu wa maofisa.
Kabla ya kufungwa, maofisa wa Benadir walikuwa na mikutano ya kupeana taarifa ya wiki moja na wakaazi kuwaelimisha kuhusu kwa nini taa za barabarani ni muhimu kwa usalama wa umma katika viunga vyao.
"Tunafanya kampeni hii ya mwamko kabla hatujafunga taa ili watu waelewe umuhimu wa kufanya kazi kwa usalama na kuchukulia kwamba ni wamiliki na kuzilinda kama mali yao, badala ya kuziona taa kama mali ya wengine," Gavana Msaidizi wa Benadir Iman Ikar Nur aliiambia Sabahi.
Wakaazi wanapaswa kuwa waangalifu na kufuatilia kwa karibu magenge ya vijana na wanaoshukiwa kuendesha al-Shabaab ambao wangetaka kuziharibu taa ili waweze kufanya shughuli zao kwenye giza, Nur alisema.
Serikali ya Uingereza imetoa mchango wa taa za umeme jua zaidi ya 100, na ufungaji utaanza mapema ambao utafanywa na Chama cha Msaada wa Kimataifa cha Nordic, Nur alisema.
"Jitihada za utawala wa Benadir ni jambo la kufurahia, kwa kuwa utatupa uwezo wa kutoka nje [usiku] na kubainisha watu wakati kuna tukio ambalo linatishia usalama," alisema Sahra Abdi Nur, mama wa watoto wanne mwenye umri wa miaka 28 ambaye alihudhuria programu ya mwamko katika Kituo cha Utafiti na Mjadala katika wilaya ya Hodan.
"Kwa sasa kila mtaa katika maeneo ya jirani yetu kuna giza usiku na huthubutu kutembea katika giza," aliiambia Sabahi.
Amina Yasin, raia wa Howlwadag mwenye umri wa miaka 32, alisema taa za barabarani zitakuwa kama zana katika kuhakikisha usalama.
"Katika matukio mengi, wanachama wa kundi la kupinga amani la al-Shabaab wanafanya kazi kwa siri wakati wa usiku, wakati mwingine wanafanya mashambulizi ya kivita kwa wakazi wa maeneo ya jirani," aliiambia Sabahi. Hata hivyo, ufungaji wa taa hizi utasaidia kuzuia operesheni za al-Shabaab na kufuta uwezo wowote uliobaki kupigana na majeshi ya serikali, alisema.
Kwa Mumin Ahmed, mkazi wa wilaya ya Warta Nabada mwenye umri wa miaka 54, taa zitasaidia wananchi kukumbuka ufahari wa zamani wa Mogadishu.
"Kweli, siwezi kukumbuka mara ya mwisho nilipoiona Mogadishu ikiwa na mwanga wa kutosha," aliiambia Sabahi. "Mbali na umuhimu wa kuimarisha usalama, tutakuwa na thamani katika kuanzisha upya uzuri ambao mji mkuu ulikuwa nao. Pia, ni vizuri kufuatilia wale ambao wanaofanya uchafuzi kama vile migahawa ambayo inatumia fursa ya giza kutupa taka mitaani."
Wakazi watazilinda taa za barabarani dhidi ya wahalifu, alisema Mohamed Ali, mzee wa Kiyaqshid mwenye umri wa miaka 65.
"Hatutakubali yeyote ambaye anapinga amani au kupinga kujengwa kwa taa za barabarani katika mitaa ya viunga vinavyotuzunguka, iwapo ni wahalifu au magaidi [wanaojulikana] -- wote wanaofaidi kutokana na giza la barabarani huko Mogadishu," aliiambia Sabahi.
"Ninauambia utawala wa mkoa wa Benadir, mtatosheleza majukumu yenu kama mtafunga taa kwa ajili yetu na tutawajibika kuzilinda, hivyo tuachieni," alisema.

No comments:

Post a Comment