Wednesday, June 5, 2013

Shirdon atoa wito kwa Afrika Kusini kuwalinda raia wa Somalia

Somalia Abdi Farah Shirdon alielezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa Wasomali nchini Afrika Kusini, na kutaka serikali ya huko kuingilia kati ili kuzuia vurugu dhidi ya watu wa Somalia baada ya mashambulizi ya mauaji huko Pretoria na Port Elizabeth wiki iliyopita.
"Ninaiomba serikali ya Afrika Kusini kama suala la dharura kuingilia kati na kuzuia vurugu zisizokuwa za lazima na za bahati mbaya dhidi ya jamii za wafanyabiashara wa Somalia ili kudumisha amani na utulivu, kwa hivyo kuimarisha na kukuza mahusiano ya kidugu baina ya watu wetu na serikali zetu," Shirdon alisema katika barua kwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma siku ya Jumatatu (tarehe 3 Juni).
Matamshi hayo ya waziri mkuu yanakuja baada ya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya wafanyabiashara wa Somalia nchini Afrika Kusini wiki iliyopita, ikiwemo mashambulizi ya kikatili dhidi ya Abdi Nasir Mahmoud mwenye umri wa miaka 25.
Mahmoud alipigwa mawe hadi kufa na kundi la watu huko Port Elizabeth siku ya tarehe 30 Mei na video ya simu ya mkononi ya shambulio hilo ilitolewa katika intaneti hivi karibuni. Polisi wanachunguza tukio hilo, lakini hakuna mtu aliyekamatwa bado.
Shirdon alituma rambirambi zake kwa familia za wahanga waliouliwa, kujeruhiwa au kupoteza mali zao wakati wa vurugu za hivi karibuni huko Pretoria na Port Elizabeth.
"Kwa upande mwengine, pia ninawataka Wasomali walioko Afrika Kusini kuheshimu na kufuata kikamilifu sheria na mila za huko, kufanya kazi na Ubalozi wa Somalia mjini Pretoria, kudumisha utulivu, kuelewa kwamba serikali yangu itafanya kazi kikamilifu na serikali ya Afrika Kusini ili kushughulikia matatizo haya yanayotokea," alisema waziri mkuu. "Mawazo yetu yako pamoja na Wasomali ambao wameteseka katika kipindi hiki cha huzuni."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilitangaza hapo Jumanne kwamba ilikuwa inapeleka ujumbe huko Afrika Kusini katika juhudi za kutatua mzozo huu wa kiusalama ambao unaiathiri jamii ya Wasomalia.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje Abdisalam Haji Ahmed Liban alilaani mashambulizi hayo dhidi ya wananchi wa Somalia na kuelezea kusikitishwa kwake na njia ya kikatili ambayo Mahmoud aliuawa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Liban aliitaka serikali ya Afrika ya Kusini kuwalinda Wasomalia na kuharakisha kuwakamata waliotenda uovu.

No comments:

Post a Comment