Monday, June 3, 2013

Tuisaidie vipi Zanzibar itoke kwenye Muungano?

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Hassan Nassor Moyo (kushoto) na Mjumbe wa kamati hiyo Ismail Jussa Ladhu, wakibadilishana mawazo kabla ya ufunguzi wa kongamano la maridhiano lililofanyika hoteli ya bwawani.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Hassan Nassor Moyo (kushoto) na Mjumbe wa kamati hiyo Ismail Jussa Ladhu, wakibadilishana mawazo kabla ya ufunguzi wa kongamano la maridhiano lililofanyika hoteli ya bwawani.
June 3, 2013 By Inaonekana kina Seif Sharrif na kina Karume hawataki hasa Zanzibar iwe dola huru ikiwa na “mamlaka yake”. Kwa karibu miaka miwili sasa wameendelea “kudai” Zanzibar “huru” huku wakipuuzia njia zote rahisi za kuweza kufanya hivyo. Nimejaribu kwa kila namna kuwapa ushauri rahisi wa kuiondoa Zanzibar kwenye Muungano na ikawa nchi huru na tukakutana UN, SADC, na EA kama nchi huru majirani lakini ndugu zetu inaonekana hawataki kuchagua njia hata moja. Badala yake wameendelea na nina uhakika wataendelea kufanya mikutano mingine ya “kudai” Zanzibar huru.
Sasa najiuliza wanataka tuwasaidieje? Wanataka sisi tuwafukuze watoke ili waseme tumewafukuza? Suala la Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili liko mikononi mwa Wazanzibari peke yao.
1. Walipodai Bendera ya Zanzibar Tanzania bara hatukuulizwa; waliamua wakawa nayo
2. Walipotaka wimbo wa Taifa – Tanzania Bara hatukuulizwa; wakawa nao
3. Walipoamua kutangaza Zanzibar ni huru na kuainisha mipaka yake kupitia katiba yao walifanya hivyo bila Watu wa Bara kuulizwa.
Kuna ushahidi wa kutosha kabisa kuwa linapokuja suala la Zanzibar kudai “uhuru” na alama za kuwa bado wao ni dola Zanzibar wana rekodi ya kufanya hivyo bila kuomba kibali kutoka Dodoma au kwa watu wa bara. Sasa kwanini kwenye “mamlaka kamili” ni kama vile “wanataka hawataki”? Kabla sijaamua kuwapa pendekezo jingine naomba Wazanzibar wale asilimia 60 ambao wanaamini kutokana na wingi wao wanawakilisha msimamo wa Wazanzibari wote wafanya mambo yafuatayo ili waharakishe kuitoa Zanzibar kwenye “ukoloni” wa watu wa bara na kuirejesha kuwa ile nchi nzuri, ya heri, ambapo watu wake wote walikuwa wanaishi kwa furaha na maridhiano tangu enzi na enzi.
1. Chama cha CUF na wale wa CCM upande wa Zanzibar ambao wanaamini Zanzibar inakaliwa na Bara kama koloni watangaze kutoutambua Muungano huu kwa vile siyo halali.
2. Wakishafanya hilo la kwanza CUF na CCM Zanzibar wawaambie wabunge wao walioko kwenye Bunge la Muungangano kujiuzulu mara moja ili warudi Zanzibar
3. Wazanzibar wamuambie Makamu wa Rais wa Muungano Dr. Ghaib Bilali pamoja na watumisho wengine wote walioko kwenye Utumishi wa Jamhuri ya Muungano ambao ni Wazanzibari waachie nafasi zao zote ili kutekeleza hilo la 1. Hii itauthibitishia ulimwengu na marafiki zao kuwa kweli wako serious katika kutaka uhuru – huwezi kudai uhuru wakati huo huo unatumikia serikali ile ile!
4. Ili kufanikisha hayo mambo matatu ya kwanza hapo juu na kuwa yasionekane yamefanywa kiholela basi Baraza la Wawakilishi ambao lina wasomi lifanye mambo mawili. Kwanza lilete hoja rasmi ya kuitaka serikali kuandaa mswada wa Sheria ya kusimamia kura ya maoni (referendum) ya jinsi Zanzibar itajitoa, ijitoe lini na vipi na kwa mfumo gani. Na pili ni kuileta sheria hiyo ili ipitishwe na Wawakilishi.
5. Kwa vile inawezekana basi katika sheria hiyo ya No 4 hapo itahitaji Bunge la Muungano liliridhie basi Baraza la Wawakilishi lipitishe sheria hiyo na iridhiwe na Rais wa Zanzibar na hoja ya sheria hiyo iletetwe na hao wabunge wa Zanzibar kwenye Bunge la Muungano (kabla hawajatoka) ili Bunge la Muungano liipitishe na kuruhusu Zanzibar kuanza mchakato wa kutoka kwenye Muungano na ili kwamba Bunge la Muungano nalo liweke utaratibu wa kuhakikisha kuwa mali na haki za Watanganyika Zanzibar haziangukii mikononi mwa Nchi ya Zanzibar!
6. Wazanzibari waharakishe kuweka tarehe ya kutaka kutoka kwenye Muungano ili na sisi watu wa bara tuzidi kuwaombea ili matamanio yao na njozi zao za kuirudisha Zanzibar ambayo inatawaliwa na Tanganyika zitimie.
NB: Ikumbukwe kuwa watu wa bara hatutaki Muungano wa Mkataba. Tunataka Zanzibar watoke bila ya kufuatiwa na kitu kingine chochote zaidi ya mahusiano ya ujirani mwema wa nchi mbiili. Bila ya shaka kutokana na historia inawezekana katika mfumo ujao kutakuwa na makubalianao ya nchi mbili (bilateral agreements) ili kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa huru n.k nk
Sasa kama njia hizi zote hazichukuliwi; tuwasaidie vipi Wazanzibar hawa wanaotaka kutoka kufunga virago?
LET ZANZIBAR GO!!!

No comments:

Post a Comment