Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
ameunga mkono kauli iliyotolewa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya
Maridhiano Zanzibar Eddi Riyami ya kuwataka Wazanzibari wasiotaka
mamlaka kamili ya Zanzibar wajitokeze hadharani kama wanavyofanya wale
wanaodai mamlaka kamili ya Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ameeleza hayo katika
viwanja vya Kibanda maiti mjini Zanzibar katika mkutano wa hadhara
uliolenga kusherehekea “Umoja wa Wazanzibari” ulioasisiwa kufuatia
maridhiano ya kisiasa.
Amesema hatua ya Wazanzibari kudai mamlaka ni haki yao, na kwamba hakuna dhambi ya kudai jambo hilo.
Amefahamisha kuwa wazanzibari walio wengi wameungana kudai mamlaka
ya nchi yao kwa njia ya amani na demokrasia, na kutoa wito kwa wale
wasiotaka mamlaka ya Zanzibar wajitokeze hadharani.
Amewahakikishia wananchi kuwa hatorudi nyuma katika kuitetea
Zanzibar kuwa na mamlaka yake, ili iweze kutambulika kimataifa na kuweza
kuratibu na kushughulikia mambo yake ya nje.
Kwa upande wake Katibu wa kamati ya maridhiano Ismail Jussa Ladhu,
amewaomba viongozi wa vyama vyote kushirikiana na wananchi katika kudai
mamlaka ya nchi, ili wazanzibari waweze kujikomboa kutokana na kile
alichokiita ukoloni wa Tanganyika.
Katika risala ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar iliyosomwa na
Ameir bin Ameir kutoka Bwejuu, amesema pamoja na mambo mengine, katiba
mpya izingatie uwepo wa Jamhuri ya Zanzibar na uraia wake.
Mambo mengine waliyotaka yatolewe katika orodha ya mambo ya
Muungano ni pamoja na sarafu, benki kuu, mambo ya nje, vyama vya siasa,
baraza la mitihani pamoja na mafuta na gesi.
No comments:
Post a Comment