Saturday, June 8, 2013

Anayezuia mamlaka kamili ya Zanzibar anajisumbua

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad akipokea nakala ya rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Makamu wa Rais Muungano Dkt Gharib Bilal, huku Jaji Mstaafu Joseph Warioba akishuhudia
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad akipokea nakala ya rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Makamu wa Rais Muungano Dkt Gharib Bilal, huku Jaji Mstaafu Joseph Warioba akishuhudia
KAMA kuna wakati ambao Wazanzibari wamepata nafasi nzuri zaidi ya kueleza hisia zao kuhusu mustakbali wa Muungano wa Tanzania, basi ni kipindi kilichoanzia tangazo la Rais Jakaya Kikwete la kuleta fursa kwa Watanzania kuandika katiba wanayoitaka.
Kwanza hiyo ni fursa ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza kwao kujadili kwa uwazi suala hili ambalo limekuwa likiwasumbua kwa muda wote huo tangu dola yao huru ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilipounganishwa na Jamhuri ya Tanganyika Aprili 26, miaka karibu 50 iliyopita.
Ni fursa pia kwa Watanzania wa upande wa Tanganyika (nchi waliyojitia kuiita Tanzania Bara) kujadili muungano wao kwa kuwa nao, kama walivyo ndugu zao wa Zanzibar, wana maslahi makubwa kutokana na mfumo wa Muungano huo ulioasisiwa kwa nguvu kubwa na aliyekuwa kiongozi wao mkuu baada ya dola yao kupata uhuru Desemba 9 mwaka 1961, Mwalimu Julius Nyerere.
Sababu ya pili ya kujitokeza kwa fursa ya kujadili suala la muungano kwa uwazi ni ule ukweli kwamba Wazanzibari wanazo kumbukumbu nyingi za namna walivyopoteza viongozi wake wakuu kwa sababu ya hatua za viongozi hao kusimama kidete kutetea maslahi ya nchi yao, Zanzibar.
Alisumbuliwa Mzee Abeid Amani Karume kila alipotaka kubadilisha mwelekeo wa Muungano. Mzee Karume aligundua mapema sana kwamba alilaghaiwa na muasisi mwenzake wa muungano, Mwalimu Nyerere. Aligundua kuwa kumbe mwalimu hakuwa na nia njema katika kutaka Muungano.
Ndio maana Mzee Karume mara tu alipotanabahi kuwa alizungukwa, aliamua kila wakati kuchukua msimamo imara wa kuibakisha dola ya Zanzibar katika mstari wa kuwa nchi inayojitegemea. Kwa bahati mbaya, alimudu mambo machache tu lakini mengi yalimshinda kutokana na kubanwa na sheria iliyokuwepo ya mamlaka kuvikwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wazanzibari wangali wanakumbuka kauli mbalimbali za ukakamavu alizokuwa akizitoa Mzee Karume kuonesha kupinga kuporwa mamlaka na Serikali hiyo.
Aliposema “Muungano ni kama koti likikubana livuwe,” aliposema “Muungano mwisho Chumbe,” alipofukuza mawaziri kadhaa wa Mwalimu Nyerere waliotumwa kuja kumwambia hili na lile, alipozuia safari ya wanajeshi wa Kizanzibari kwenda Msumbiji kwa kuwa hakushauriwa wala kujulishwa na muasisi mwenzake wa Muungano, Mwalimu Nyerere kuhusu safari hiyo, alikuwa anadhihirisha kupinga mfumo wa muungano.
Alipokuwa ameandaa sarafu mahsusi ya Zanzibar huku akimkatalia Waziri wa Fedha wa Mwalimu Nyerere, Mzee Amir Jamal aliyetumwa kuja kumshawishi Mzee Karume kupeleka au kusalimisha hazina yake ya fedha Tanganyika, na alipopeleka ujumbe wa kabineti yake kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa muungano, yote hayo ni kudhihirisha alivyopinga mapema muungano wa kinafiki.
Mapema kabisa, Mzee Karume alishuhudia namna muasisi mwenzake alivyohalifu miadi kwa kuandaa sheria zisizokubaliwa na wote wawili – badala ya zile zilizokubaliwa – ikiwemo ya kuwageuza watumishi wa Tanganyika kuwa ni watumishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzibadilisha sheria za Tanganyika kuwa ni sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuunda Mahakama Maalum ya Kikatiba kwa ajili ya kushughulikia mivutano ya kimuungano – na hivyo naye kuamua kwenda kulingana na matakwa ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Mzee Karume alishuhudia vilevile, kuondolewa kwa sheria iliyoweka muda maalum wa kudumu kwa muungano huo na kutathminiwa kama una maslahi kwa washirika wake muda huo utakapokuwa umefika. Muda ulikuwa ni wa miaka 10, kwa maana ya kwamba ilikubaliwa itakapofika mwaka 1974, pande mbili zilizoungana, Tanganyika na Zanzibar, zijadili kama muungano unakidhi maslahi ya pande hizo.
Mzee Karume alipouliwa Aprili 7 mwaka 1972, miaka miwili kabla ya kufika kwa muda wa kutathmini mwenendo wa Muungano, ikaonekana kama vile ingekuwa mwisho wa harakati za Wazanzibari kudai haki ya mamlaka yao. Sivyo.
Mauaji hayo yalikuwa machungu mengine kwa Zanzibar ambayo tayari ilishashuhudia umwagikaji mkubwa wa damu ya wananchi waliodhulumiwa kwa sababu tu ya kupigania nchi yao iliyoingizwa katika muungano wa kilaghai.
Historia inaonesha viongozi wengi wa kisiasa hasa waliokuwa wasomi wa hali ya juu pamoja na maulamaa katika Uislam, waliuliwa kwa siri na kwa dhahiri kwa sababu ya misimamo yao hiyo ya kuisimamia haki ya Zanzibar na Wazanzibari.
Hapo ndipo yanakuja majina makubwa na maarufu ya kina Jaha Ubwa, Othman Sharif, Mdungi Ussi, Ibrahim Saadalla, Abdalla Kassim Hanga na wengineo waliouliwa katika matukio ya kusikitisha wengine wakiwa hawakuzikwa na jamaa zao.
Madai ya Zanzibar yaliendelezwa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliyefuata baada ya hapo, alisimama barabara kuitakia Zanzibar mamlaka yake. Kwa kuwa mfumo wa kudhoofisha yeyote ambaye angeutilia shaka muungano ulishajengwa na kuimarika kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda, juhudi zake ziligonga mwamba.
Ilikuwa mwaka 1984 alipojikuta akihojiwa na Mwalimu Nyerere mbele ya wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwanini aliandaa waraka wa kutaka Muungano ubadilishwe ili kuirudishia Zanzibar mamlaka yake.
Ilikuwa ni bahati mbaya kwamba Mzee Jumbe aliandaa waraka wa kuitetea Zanzibar akiwa peke yake – hakumshauri au kumshirikisha yeyote kati ya mawaziri wake wakati huo. Hili ni jambo lililoleta utata mkubwa kiasi cha kusababisha mawaziri wa Serikali ya Zanzibar kumkana ilipotokea kuulizwa kama walikuwa wanajua lolote kuhusu waraka aliouandaa Mzee Jumbe.
Taarifa za ndani ya serikali zilieleza kwa umakini jambo hilo kuwa ukweli Mzee Jumbe hakushirikisha kiongozi yeyote katika kuandaa waraka huo na kwamba kwa vile wenzake hawakujua ni kitu gani hasa alichokusudia kukipata – tena labda ilikuwa ni jambo la maslahi yake binafsi kuliko nchi – wao waliona wangekumbwa wote na fagio.
Wakaukana waraka na kumtosa Mzee Jumbe. Ilikuwa ni bahati mbaya sana kwa hakika kwa sababu hata kama ilikuja kudhihirika kuwa alichokiandaa kilikuwa na maslahi makubwa ya kuikomboa nchi kutoka minyororo ya kumong’onyolewa mamlaka yake, alilenga pia kujijenga kisiasa kwa nia ya kutwaa madaraka ikitokea Mwalimu Nyerere kung’atuka.
Kilichomfika Mzee Jumbe baada ya hapo ni kulazimishwa kujiuzulu baada ya kujitetea kwa ujasiri mkubwa, huku akitaka aachiwe arudi Zanzibar ambako ndio angetangaza kujiuzulu kwa kuwa ndiko kwenye mamlaka yake. Hakuruhusiwa, badala yake alijiuzulu palepale na kuanza kutengwa kiulinzi huku akiwa amezuiliwa haki zake za kibinadamu.
Hizi ni pamoja na haki ya kuwasiliana na familia yake, haki ya kwenda atakapo, haki ya kushirikiana na watu atakao na kadhalika. Simu zilikatwa kwenye nyumba zake mbili, Unguja na Pemba.
Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyefuata hakuwa na makubwa zaidi ya kujitahidi kuleta sera ya kuregeza masharti ya biashara hivyo kuchochea uingiaji wa bidhaa nyingi nchini zilizosaidia kuinua uchumi wa nchi na mapato ya wananchi. Alikaa kwa mwaka mmoja tu kupandishwa kwenda kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1985.
Katika awamu hizo mbili, Zanzibar ilianza kufunguka kidunia. Misingi ya nchi ya kidemokrasia ilianza kujengwa. Ndipo Zanzibar ikapata katiba yake huru baada ya ile iliyofutwa mara tu ilipoingia Serikali ya Mapinduzi ambapo ilipindua katiba na sheria na kuweka mahakama za wananchi badala ya zilizofuata sheria.
Paliandikwa Katiba ya 1984 ambayo ilikuwa na ruhusa ya haki zote za kibinadamu – Bill of Rights – wakati tayari likiwepo na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, mfano wa Bunge kwa nchi nyingine.
Mzee Idris Abdulwakil hakuwa na makubwa ingawa alikuwa na msimamo wa dhati wa kuitetea Zanzibar kama ilivyodhihirika wakati fulani alipoyaeleza baadhi ya mambo yanayopaswa kutizamwa upya kwa lengo la kuiwezesha Zanzibar kukuza uchumi wake.
Hapo ikaja zama ya Dk. Salimin Amour Juma ambaye alikuwa akiuma na kupuliza katika kutetea maslahi ya Zanzibar. Mara kadhaa alisikika akiwa mkakamavu lakini akisalimu amri baada ya kutishiwa na uongozi wa juu. Hili lilidhihirika alipoingiza Zanzibar katika Jumuiya ya Nchi za Kiislam – Organisation for Islamic Conference (OIC) – mwaka 1994, na kuitoa haraka baada ya Mwalimu Nyerere kutumia rungu la Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, Wazanzibari hawasahau jinsi serikali yake ilivyoandaa waraka maalum wa kuyahoji masuala kadhaa yaliyo chini ya Muungano na kutaka majadiliano. Kuna tume ya Amina Salum Ali iliyokuja na mapendekezo ya kurekebisha masuala yanayoweza kuisaidia Zanzibar kiuchumi hasa kwa kuwa eneo hilo halikuwa moja na mambo ya Muungano ndio maana Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mpaka leo haitizami uchumi wa Zanzibar inapoandaa sera za kifedha.
Ila inafurahisha kukuta kwamba pamoja na hasara zote hizo zikiandamana na vitisho vya dola kubwa ya Tanganyika iliyojigeuza kinyemela na kuvaa koti la Muungano, Wazanzibari hawakutetereka. Waliendelea kudai haki yao ya kuondokana na utawala wa Waafrika wenzao.
Katika harakati zao paliandikwa vitabu na mashairi mengi kuelezea ubaya wa kuikandamiza Zanzibar. Miongoni mwa vitabu hivi ni kile alichoandika Abdulrahman Mohamed Babu kiitwacho I Saw The Future And It Works, Mzee Jumbe kiitwacho The Partnership: 30 Years of Turbulent Zanzibar na Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru alichoandika Dk. Harith Ghassany, Mzanzibari aliyelewea Uarabuni.
Hatua za sasa ni mfululizo wa jitihada za Wazanzibari kudai haki ya kurudisha mamlaka yao ya kujitawala. Kama si sasa basi hakika ni halafu hakutakuwa na namna ya kuzuia madai yao. Italazimu haki iachiwe kusimama.
Chanzo: Fahamu – Kalamu ya Mzanzibari

No comments:

Post a Comment