VIONGOZI waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Zanzibar kwa kweli wanachekesha kwa namna wanavyotunisha misuli ya shingo kupinga utashi wa wananchi wa Zanzibar kutaka mabadiliko ya mfumo wa muungano wao na Tanganyika. Waelewe kuwa suala la Wazanzibari kudai kurudishwa mamlaka iliyokuwa nayo serikali baada ya uhuru wa 10 Desemba, 1963 ni haki yao isiyopingika. Hata kama mtu atapinga, bado haki ya kutaka watakacho wananchi haitafutika.
Muungano wowote, hata wa watoto unapaswa kuwa endelevu. Unapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia haki kwa walioungana. Watoto walioungana watapendana. Lakini upendo kwao utakuwa na maana tu iwapo watachangia kwa usawa kile walichokubaliana.
Utasikia Khadija lete mchele. Haya naleta lakini wewe lete nazi. Naye atasema sawa, lakini na Riziki yeye alete kuni za kupikia. Riziki ataridhia kuleta kuni. Ila naye atasema Mariam alete chumvi. Watatajana hivyo katika utaratibu wa kuchangia mpaka wahakikishe chakula kitapikika. Kikiwiva watakula pamoja. Hao ni watoto, itakuwa watu wazima walioungana?
Kilio cha Wazanzibari tangu Muungano ulipoasisiwa mwaka 1964 ni kutokuwepo kwa nia njema. Hazikupita siku nyingi, muasisi mmojawapo, Mzee Abeid Amani Karume, alibaini hilo. Aliona kumbe mwenzake alikuwa na malengo yasiyokuwa ya kuungana kwa maana ya kusaidiana na kuinuana kiuchumi.
Mzee Karume ambaye alisalimisha mamlaka ya dola ya Zanzibar – Jamhuri ya Watu wa Zanzibar – alianza mapema kutoa hotuba za kumshitua Mwalimu Julius Nyerere, muasisi mwenzake wa Muungano aliyenukuliwa kabla ya hapo kuchukizwa na kuwepo kwa visiwa vya Unguja na Pemba karibu na Tanganyika.
Makubaliano ilikuwa kila mshirika wa Muungano atabaki na sheria zake kwa mambo ya maslahi ya watu wake, bunge lake, watumishi wake, mahakama yake mpaka ngazi ya Mahakama Kuu. Ushirikiano utakuja kwenye ngazi ya Mahakama ya Rufaa. Kulipaswa kuwepo Mahakama Maalum kwa ajili ya kushughulikia mizozo ya kimuungano. Haipo.
Mzee Karume aliendelea kuchukua msimamo mkali wa kuhakikisha haki za Zanzibar zinalindwa. Alithubutu kukataa maagizo mengi yaliyotoka kwa Mwalimu Nyerere, ikiwemo pale alipotumwa Waziri wa Fedha, Amir Jamal, kumshawishi aisalimishe Hazina ya Zanzibar kwa Hazina Kuu ya Tanzania. Alikataa kwa kauli kali.
Mzee Karume alisema wazi Hazina ya Zanzibar ni mali ya wananchi wa Zanzibar na akamtaka Mzee Jamal arudi na salamu hizo kwa Mwalimu Nyerere. Mpaka alipopigwa risasi tarehe 7 Aprili, 1972, Hazina ya Zanzibar ilibaki Zanzibar.
Wazanzibari wanataka nchi yenye mamlaka kamili kwa sababu wanajua wametezwa nguvu za kujiongoza kwa mambo kadhaa, yakiwemo yale yanayogusa mzizi wa uchumi. Uchumi si suala la Muungano lakini raslimali au nyezo za kuujenga, karibu zote zinadhibitiwa na Serikali ya Muungano.
Watakuzaje uchumi wao wakati hata Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo katika fedha zilizotumika kuianzisha mwaka 1967, asilimia 11 ilikuwa ni mchango wa Zanzibar uliotokana na kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB), haisimamii uchumi wa Zanzibar.
Ndio ukweli benki kuu hii kwa muda wote wa uhai wa Muungano haijishughulishi kuutizama uchumi wa Zanzibar na inapotunga sera za kifedha haijali kama zaweza kuwa na athari kwa uchumi wa Zanzibar.
Ni kwa sababu hiyo wakati fulani katika miaka ya 1990, Serikali ya Zanzibar ililalamikia hatua ya Serikali ya Muungano kuteremsha ghafla thamani ya sarafu bila ya kuifahamisha Zanzibar ambayo wakati uamuzi huo unatangazwa, ilishapanga bajeti yake.
Bajeti iliparaganyika kiasi cha kulazimu kupangwa upya. Ingetekelezwa vipi wakati ilizingatia kiwango cha thamani ya fedha ya nchi ambacho tayari kimebadilishwa? Kwa agizo la viongozi wa juu wa serikali mbili, wataalamu wa Wizara ya Fedha ya Muungano na wale wa Zanzibar walijadiliana namna ya kuipunguzia Zanzibar makali ya athari za mparaganyiko huo wa bajeti.
Na kwanini benki kuu ya Tanzania isihudumie uchumi wa Zanzibar kama inavyohudumia ule wa Tanganyika? Hizi serikali si zinatumia sarafu moja ya Shilingi? Zitatenganishwaje katika kusimamiwa kiuchumi?
Watalaamu walisema hatua hiyo ilifanywa kwa makusudi ya kuitia adabu Zanzibar kwa kuwa ilikataa kusalimisha Hazina yake. Nani asiyejua kuwa ndege mjanja hukimbiza ubawa wake? Kama wakubwa wameshaona wenzao hawakuwa na nia njema katika kutaka muungano, kwanini wasabilie kila kitu hata vile ambavyo wangenufaika vikibaki kwao tu? Ni mwendawazimu tu anayekata mkono anaolia.
Kwa miaka yote hiyo ya uhai wa Muungano, Serikali ya Muungano imeiwekea ngumu Zanzibar kutekeleza programu zake za kukuza uchumi kupitia mradi wa Bandari Huru (Duty Free Port), Maeneo Huru ya Kiuchumi (ZAFREZA). Sasa kwanini izuiwe wakati uchumi si suala la Muungano na hizo ni nyenzo za kuiwezesha kujenga uchumi wake?
Nani amesahau namna viongozi wa Zanzibar walivyodhalilishwa kwa kukaripiwa walipoingiza nchi katika Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC) wakati ikijulikana wazi kilichofuatwa hapo ni fursa ya kuinua hali za wananchi kupitia misaada? Serikali ya Muungano walijua, lakini waliwalaghai Watanzania ili tu kuivunja dhamira njema ya wenzao wa Zanzibar.
Waliagiza kuitoa Zanzibar katika jumuiya hiyo kwa ahadi ya kuchukua hatua ya kujiunga. Visingizio visivyo idadi, bali hili halijatekelezwa hadi leo.
Sasa viongozi wenye upeo wa Zanzibar wameamua kushikana na Wazanzibari kudai haki ya kujiongoza. Mzee Hassan Nassor Moyo na Kamati ya Maridhiano wanaungwa mkono na umma kwa sababu wanazungumza lugha inayotii maoni ya wananchi walio wengi. Busara zao ndizo zilizosaidia kuleta utulivu uliopo baada ya kufanikiwa kushawishi viongozi wakuu wa kisiasa mwaka 2009, Amani Abeid Karume wa CCM na Maalim Seif kwa CUF na kukubaliana kufuta siasa chafu.
Kutokea viongozi wachache wakagoma kwa ghamidha na chusha, huku wakitishia wale wanaotaka mabadiliko na kuridhia mbinyo uliopo, ni kujisumbua. Utakuja wakati utashi wa Wazanzibari utakosa wa kuuzuia.
Viongozi wagumu wanachokifanya ni kuzidisha nguvu ya propaganda. Wanakaa wakitega umma unasema nini na unataka nini katika dhamira yao ya kujitawala, ndipo wajibu. Kwa bahati mbaya, wanajibu pumba si hoja zilizotolewa. Hoja hujibiwa kwa hoja zilizopangiliwa na siyo viroja.
Baada ya kuona harakati za Wazanzibari kutaka mamlaka kamili ya kujiongoza zimepamba moto, na kwa kweli haziwezi kudhoofishwa, wameamua kumbana kiongozi anayependwa na kutegemewa wakidai eti amemdharau Rais Dk. Ali Mohamed Shein aliyemteua.
Hoja ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai kwamba eti Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amemdharau rais kwa anachodai kutoa kauli zinazoweza kuleta mtafaruku wa maelewano kati ya Dk. Shein na Karume aliyestaafu, ni kulazimisha kosa lisilokuwepo kimantiki wala kisheria.
Anayefikiri vizuri anajua nafasi ya Karume na Maalim Seif katika hali tulivu iliyopo. Vilevile anajua nafasi ya Dk. Shein na ahadi aliyoitoa baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi 2010. Je, amejiuliza kama yanayotendeka chini ya uongozi wa Dk. Shein, yote yanazingatia utashi wa wananchi walio wengi?
Je, anaweza kueleza ni nini maana ya rais kuwaambia wananchi asiokubaliana nao kimitizamo wahame nchi? Kwani alidhani urais ni kukubaliwa kila unachokiamini? Au urais ni kuamua kila unachokiwaza hata kama sivyo wananchi waonavyo? Au anaamini anayo haki ya kuongoza kwa maamuzi yoyote apendayo bila ya kuulizwa kitu na wananchi? Ndo maana akasema wananchi wanaitakia nini serikali yake, siyo?
Kama anaamini hayo, basi nahofia kuwa watu wanaongozwa kwa ulimi badala ya maarifa. Hapo kunaashiria hatari.
No comments:
Post a Comment