KATIKA hali inayoonyesha dharau
kwa Watanzania na waumini wa Dini ya Kiislamu, Muingereza Sarah
Hermitage, amefananisha Watanzania na nguruwe ambaye ni mnyama haramu
kwa mujibu wa imani ya Kiislamu.
Sarah ambaye amekua akiwakashifu
viongozi na wananchi wa Tanzania mara kwa mara alivuka mipaka na
kufananisha Watanzania na nguruwe, baada ya kulalamikiwa kwa vitendo
vyake vya kutoa maneno machafu kwa Watanzania katika mitandao ya
kijamii.
Kauli hizo za Sarah amekua
akizitoa kupitia mitandao ya twitter kupitia ukurasa wake
wa https://twitter.com/Chomachomp kwa muda mrefu sasa bila
kuchukuliwahatua zozote na viongozi wala watendaji wa serikali ya
Tanzania.
Kauli ya Sarah kuita Watanzania
ilianzia pale Mtanzania mmoja ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe
Mbaraka Islam, kulalamikia kitendo chake cha kutukana viongozi na
Watanzania wote kwa ujumla wao bila kuwa na hoja zinazowahusu.
Huku akijua aliyewasiliana naye
ni Muislamu, Sarah aliandika katika ukurasa wake kwamba “anga la
Tanzania limejaa nguruwe wanaopaa, Mbaraka Islam, ni kupe wa mwezi”,
akimaanisha kwamba Mbaraka Islam ni mmoja wa nguruwe wengi wanaoelea
katika anga la Tanzania.
“Kwa maana yoyote anayotaka
kuuaminisha umma na katika mazingira ya Tanzania na Dini yetu,
haiwezekani kwamba Sarah hakujua kwamba ni kashfa nzito ya Kidini
kumfananisha Muislamu na nguruwe kwa namna yoyote ile. Alijua mimi ni
Muislamu alifanya hivyo kusudi.
“Huyu mama (Sarah) amefanya hivyo
baada ya kuona Watanzania wamelala na hakuna anayethubutu kumgusa hasa
viongozi wetu anaowatukana anavyotaka bila kuguswa na yeyote,” alisema
Islam na kuongeza kwamba amechukua hatua kadhaa ambazo hajapenda
kuziweka hadharani kwa sasa.
Kwa mujibu wa imani ya dini ya
Kiislamu, mnyama nguruwe ni haramu na najisi na kwamba haruhusiwi kuliwa
na unapomgusa unapaswa kujitakasa kwa kuoga mara saba moja ikiwa ni kwa
kutumia mchanga.
Sarah alikerwa na makala aliyoandoka Islam katika gazeti la Raia Mwema, ambayo ilielezea kukerwa na maneno machafu anayoyatoa kwa Watanzania.
Katika makala hiyo, Islam alisema:
KWA takriban miaka mitano sasa,
raia mmoja wa Uingereza, Sarah Hermitage amekuwa akiendesha kampeni ya
kumchafua Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya Tanzania, taasisi muhimu za
nchi yetu kama vile mahakama, waandishi wa habari na hata Watanzania
ambao wamekua wakimpinga.
Pamoja na kuwa kumekua na
mapungufu katika serikali yake na vyombo vyake kama ilivyo kwa serikali
nyingine Duniani ikiwamo ya Uingereza, Muingereza huyu amekua akitoa
kashfa kwa kila jambo linaloandikwa ama kujadiliwa kuhusiana na viongozi
wa Tanzania na taasisi zake na kwa kutumia lugha isiyo na staha.
Watanzania siku zote wakiwamo
wanasiasa, waandishi wa habari na wanaharakati, wamekua wakiikosoa na
hata kuishambulia serikali na vyombo vyake inapokosea jambo ambalo ni
jema na linasaidia kuimarisha utawala bora, lakini kwa staili anayotumia
Muingereza huyu ni kupitiliza mipaka na zaidi ya yote ni udhalilishaji
usioweza kuvumilika kwa mtu mwenye mapenzi mema na nchi yake.
Dhumuni la Sarah Hermitage na
washirika wake wakiwemo baadhi ya Watanzania ni kuzishawishi nchi za
Magharibi wakianzia na Uingereza kusitisha misaada na uwekezaji katika
Tanzania. Hilo angeweza kulifanya huko kwao kwa kuwasiliana na serikali
yake, lakini badala yake amekuwa akitumia mitandao ya kijamii na barua
pepe tena kwa kutumia lugha ya kukashifu na kudhalilisha.
Watanzania wote tuna jukumu la
kutetea heshima ya nchi yetu, lakini wapo wale ambao tumewapa jukumu la
kusimama mstari wa mbele. Jambo la kusikitisha ni kwamba ni watu
wachache sana kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe ambaye ambaye
amekua na ujasiri wa kumkabili Muingereza huyu, kwa kumwambia wazi
kwamba kama ni misaada ana haki ya kuishawishi nchi yake kuzuia misaada
kwa Tanzania lakini si kwa kudhalilisha Watanzania.
Zitto alienda mbali zaidi kwa
kusema kwamba nchi nyingi tajiri duniani ikiwamo Uingereza, zimejengwa
kwa kutumia rasilimali walizozipora katika nchi walizozitawala ikiwamo
Tanzania na kwamba nchi hizo zinaweza pia kuendesha shughuli zake bila
misaada ya dharau. Bahati mbaya sana watendaji wengine wengi ambao
wanapaswa kutetea heshima yetu, hili suala limewapita, pengine kutokana
na kutokua na taarifa sahihi ama kwa kutowajibika.
Jambo la kujiuliza, wale ambao
miongoni mwa majukumu yao ya kila siku ni kutetea na kulinda hadhi na
heshima ya nchi yetu wanafanya kazi gani? Sasa tunawalipa mishahara
mikubwa na marupurupu ya nini kama hawawezi kututetea tunapodhalilishwa
ama kutukanwa?
Hali hii inatufanya tukumbuke
ujasiri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara kadhaa
aliwatunishia misuli viongozi wa mataifa makubwa walipotaka
kuidhalilisha nchi yetu, sembuse raia mmoja ambaye amekua akitumia
matatizo yake binafsi kutaka kuidhalilisha Tanzania na kutaka
kuishinikiza serikali yake na nyingine kuichukia Tanzania.
Jinsi anavyotumia mtandao wa twitter kuchafua Tanzania
Sarah Hermitage amekua akitafuta
katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani na nje ya Tanzania
vinavyoandika taarifa zozote kuhusu Tanzania na kuziongezea maneno ya
kukashifu na kejeli.
Kwa mfano amekua amechukua
taarifa inayomunukuu Raia Jakaya Kikwete akiitaka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupambana na rushwa hadi ndani ya Baraza
la Mawaaziri, na yeye kuongezea maneno akisema, “kundi moja la majambazi
linaliambia kundi lingine la majambazi kukamata mwizi”.
Akachukua taarifa iliyochapishwa
katika vyombo vya habari ikimnukuu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
akikaribisha wawekezaji katika kilimo na yeye kuongeza maneno akisema,
“Mheshimiwa Pinda kitakachoendelea kukandamizi uwekezaji katika kilimo
cha Tanzania ni uporaji wa ardhi ya wawekezaji katika mtindo wa Mugabe
(Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe).”
Amekua akidiriki kukashifu hadi
majaji wote wa Tanzania kwamba wana bei akisema, “sina hakika kama
unaweza kupata jaji ambaye si mla rushwa. Wote wana bei,” kauli ambayo
hata Watanzania wanakua wakiitoa kwa uangalifu maana hata kama kuna
majaji ambao si waadilifu, haiwezekani wakawa ni wote, kama ilivyo
katika taasisi nyingine.
Raia mmoja wa Kenya anayeishi Tanzania, aliyejitambulisha kwa jina la Marigi Patrick aliandika katika mtandao kwa kusema;
“Sisi Wakenya tuna matatizo yetu
na tumekua na tofauti kubwa sana za wazi wazi, lakini anapotokea raia wa
kigeni kumshambulia kiongozi wetu tena kama Rais wa nchi, tunaungana na
kumshughulikia. Kuna wakati Wazungu walimshambulia Rais Mwai Kibaki,
sote tukisaidiwa na wabunge wetu na vyombo vya habari tulimshambulia
hadi akakoma kutudharau.”
Marigi ambaye anajihusisha na
biashara ya bima, anasema Watanzania bado ni wachanga katika demokrasia,
ama wanadharau kila kitu bila kujua madhara yake katika hadhi na
heshima ya Taifa, na ndio maana wanashindwa kutofautisha kati ya
demokrasia na udhalilishaji unaofanywa na raia wa nchi nyingine kama
alivyo Sarah Hermitage.
No comments:
Post a Comment