Monday, July 15, 2013

Katiba Mpya iondoe vikwazo vya rasilimali za nchi – Maalim Seif


Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Naibu Waziri wa Uingereza anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds, alipofika nyumbani kwake Mbweni pamoja na ujumbe wake kwa mazungumzo.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Naibu Waziri wa Uingereza anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds, alipofika nyumbani kwake Mbweni pamoja na ujumbe wake kwa mazungumzo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema matarajio ya wananchi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ni kuona unaondoa vikwazo vya utafutaji na matumizi ya rasilimali asili zikiwemo mafuta na gesi.
Maalim Seif ameeleza hayo nyumbani kwake mbweni alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Uingereza ulioongozwa na Naibu Waziri anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzi juu  mchakato wa katiba na maendeleo ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Amesema wakati Zanzibar imeshaamua kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano, bado inasubiri taratibu za kisheria ambazo zinaweza kupatikana baada ya kukamilika kwa mchakato wa katiba.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa mchakato huo na suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano, Zanzibar itatangaza zabuni za uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ambapo makampuni mbali mbali yataruhusiwa kuomba zabuni hizo, na hatimaye kuanza rasmi kwa kazi ya uchimbaji.
Amefahamisha kuwa mchakato wa katiba umefikia hatua nzuri baada ya kuanza kwa mabaraza ya katiba tarehe 12/07/2013, ambayo itafuatiwa na bunge la katiba na baadaye wananchi wataamua katiba hiyo kupitia kura ya maoni.
Kuhusu nishati ya umeme ambapo Uingereza ni mshirika wa karibu wa nishati hiyo nchini, Maalim Seif amesema Zanzibar imo katika mchakato wa kutafuta nishati mbadala itokanayo na jua pamoja na upepo, ambapo tayari imeonesha mwelekeo mzuri.
Amesema nishati hiyo itakapopatikana itaondosha usumbufu unaojitokeza mara kwa mara na kupunguza utegemezi wa upatikanaji wa umeme kutoka Tanzania Bara, sambamba na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Aidha Maalim Seif ameelezea mazingira ya uwekezaji Zanzibar, na kuuomba ujumbe huo kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hasa katika sekta za utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Amesema Zanzibar ambayo kwa sasa imetoa kipaumbelele katika sekta ya utalii, inakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa hoteli za nyota tano katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Ameongeza kuwa Zanzibar pia ina mpango wa kujenga bandari ya kibiashara katika eneo la mpigaduni, pamoja kuvifanyia matengenezo makubwa viwanja vya ndege, ili kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji.
Naye Bwana Simmonds amesema Uingereza itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo nishati.
Ameahidi kuwasiliana na makampuni ya utalii, uvuvi na ujenzi ili kuangalia uwezekeno wa kuja kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbali mbali nchini.

No comments:

Post a Comment