Monday, July 15, 2013

Bei za vyakula afadhali kidogo – Maalim Seif

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihoji bei ya samaki aina ya change katika soko la Darajani, wakati wa ziara yake ya kutembelea soko hilo. Changu mmoja wa kawaida anauzwa kwa bei ya shilingi 8000 hadi 10,000.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihoji bei ya samaki aina ya change katika soko la Darajani, wakati wa ziara yake ya kutembelea soko hilo. Changu mmoja wa kawaida anauzwa kwa bei ya shilingi 8000 hadi 10,000.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea kuridhishwa kwake na uwepo wa bidhaa muhimu pamoja na matunda katika masoko mbali mbali ya Zanzibar.
Amesema bei ya bidhaa nyingi inaridhisha tofauti na ilivyokuwa Ramadhani ya mwaka jana, lakini tatizo kubwa ni hali ngumu ya uchumi kwa wananchi.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea masoko ya bidhaa na matunda katika manispaa ya Zanzibar.
Masoko aliyoyatembelea ni pamoja na soko la Mombasa, Mwanakwerekwe na soko kuu la Darajani.
Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Waziri wa Biashara Nassor Mazrui, Waziri wa Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mwinyihaji Makame pamoja na viongozi wa Mkoa na Manispaa, Maalim Seif alijionea hali halisi ilivyo katika masoko hayo.
Miongoni mwa bidhaa muhimu alizozihoji ni pamoja muhogo, ndizi mbichi na mbivu, majimbi, maboga, matunda mbali mbali, nyama na samaki.
Amesema kwa ujumla ameridhishwa na uwepo wa bidhaa hizo kwa wingi, licha ya bei ya baadhi ya bidhaa hizo kuwa juu na kupelekea wananchi kutumudu kununua.
Hata hivyo ameelezea kusikitishwa kwake na bei kubwa ya vitoweo, na kuwataka wachuuzi kufikiria namna ya kuwasaidia wananchi wa kawaida.
Ameitaka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais kusimamia utaratibu ulioweka wa kuweko minada katika soko la Mombasa, ili kuondosha usumbufu na msongomano katika masoko mengine.
Akizungumza na wafanyabiashara wa jua kali, Maalim Seif amesema serikali haipendi kuona wananchi wananyanyasika, na kutaka pawepo utaratibu mzuri wa kuendesha biashara katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hata hivyo amewataka wafanyabishara hao kufuata utaratibu watakaowekewa na mamlaka zinazohusika ikiwa ni pamoja na kutoweka biashara njiani zinazopelekea kufunga njia na kuleta usumbufu wa wateja na wananchi kwa jumla.
Amesema baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kumalizika, wafanyabiashara hao watapangiwa utaratibu wa kurejea katika soko la Saateni ambako kituo kikuu cha magari pia kitahamishiwa eneo hilo.
Mapema wafanyabiashara hao waliomba waruhusiwe kufanya biashara katika mwezi huu wa Ramadhan na kuahidi kuondoka baadha ramadhani kumalizika.
Nao wafanyabiashara wa masoko hayo wameelezea juu ya kadhia wanazokumbana nazo zikiwemo uvamizi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo nje ya masoko, hali inayopelekea ugumu wa biashara katika maeneo ya ndani ambayo wamekuwa wakilipia kodi.
Nae Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Abeid Juma, amesema wamekuwa wakizungumza na wafanyabiashara mara kwa mara juu ya utaratibu wa kuendesha biashara zao, lakini bado wafanyabiashara hawajajipanga vizuri kukubaliana na taratibu hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Mwinyihaji Makame, kwa upande wake ameahidi kukutana na wafanyabiashara wa soko la darajani ili kujadiliana juu ya utaratibu bora wa kuendesha biashara katika soko hilo.
Chanzo: Ofisi ya Makamao wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment