Monday, June 3, 2013

Vijana amkeni wakati wenu ni huu

Youth_Summit1 

WIKI nzima iliyopita mamia ya Waafrika walimiminika Addis Ababa, Ethiopia. Wengi walikwenda kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao miaka 12 iliyopita uliuzaa Muungano wa Afrika(AU).
Baadhi yetu tulikwenda kuitathmini hiyo miaka 50, kuangalia tulikotoka, tuliko na tuendako.Tulitathmini kwa kiwango gani malengoya Umoja huo yametimizwa na nini cha kufanywa kuliendeleza Bara la Afrika katika kipindi cha miaka 50 ijayo.
Bahati mbaya katika kufanya tathmini hiyo kuna wenye kusahau tulikotoka. Hivyo inakua rahisi kwao kukosoa kila kitu na kuufananisha Muungano wa Afrika na debe tupu.
Tumekwisha wazoea wenye kuona raha kuugeuza Umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism) uwe kama punda kirongwe, wa kustahiki bakora tu. Na kila wapatapo fursa wanautandika na kuubeza Muungano huo.
Wana usahau mchango adhimu wa Umajumui wa Kiafrika katika ukombozi wa Afrika. Tukiiangalia historia ya Afrika ya tangu mwanzoni mwa karne iliyopita hadi sasa tunaona kwamba nguvu kubwa iliyolisukuma mbele bara hili kuelekea uhuru ni ile dhana ya Umajumui wa Kiafrika pamoja na vuguvugu lake.
Mavuguvugu ya Umajumui wa Kiafrika yalikuwa kama matufali ya kujengea lile vuguvugu kubwa la kuwania uhuru wa nchi za Kiafrika.
Miongoni mwa mavuguvugu hayo ni lile la Rassemblement Démocratique Africain (RDA), lililoasisiwa 1946 mjini Bamako, Mali, chini ya uongoziwa Félix Houphouët-Boigny.
RDA lilikuwa jumuiya ya mwanzo ya Umajumui wa Kiafrika katika nchi za Kiafrika zitumiazo lugha ya Kifaransa. Ilikuwa si chama kimoja bali mtandao wa vyama mbalimbali vilivyo kuwa na mwelekeo mmoja katika nchi tafauti za Kiafrika.
Kwa upande wa kanda zetu za Afrika ya Mashariki na ya Kati tulikuwa na jumuiya ya Pafmeca na baadaye Pafmecsa ikiijumuisha na nchi ya Afrika ya Kusini.
Halafu kulikuwako Mkutano wa Watu Wote wa Afrika (AAPC) uliofanywa mara tatu — Accra (1958), Tunis (1960) na Cairo (1961). Mikusanyiko yote hiyo ilisaidia kuleta uzinduzi wa kisiasa Afrika.
AAPC ulikuwa mkutano uliohudhuriwa na wawakilishi wa vyama vya kisiasa vya nchi zilizokuwa huru wakati huo pamoja na vile vya nchi zisizokuwa huru, vyama vya wafanyakazi pamoja na mavuguvugu mengine.
Lengo lilikuwa kupigania uhuru wa makoloni, kuziimarisha nchi zilizokuwa huru na kuupinga ukoloni mamboleo. AAPC ilikuwa na sekretariati yake mjini Accra na katibu mkuu wake wa kwanza alikuwa George Padmore mzaliwa wa Trinidad.
Tukiyaacha mavuguvugu hayo ya Umajumui wa Kiafrika kulikuwako pia na nchi za Kiafrika zilizoonyesha ari ya Umajumui wa Kiafrika katika jitihada zao za kuzisaidia nchi nyingine zijikomboe.
Hapa ndipo tunapoona mchango wa Tanzania wa kuisimamia Kamati ya Ukombozi ya Umojawa Nchi Huru za Kiafrika na pili msaada wake wa kuvisaidia vyama vya ukombozi vya Msumbiji, Angola na Namibia.
Zambia nayo kadhalika ilitoa mchango mkubwa kusaidia ukombozi wa nchi zilizo kusini mwa Afrika na Guinea-Conakry ilikisaidia chama cha ukomboziwa Guinea-Bissau na Cape Verde, PAIGC.
Nchi nyingine iliyokuwa huru na iliyojitolea kusaidia ukombozi wa Afrika ni Morocco ikiwa chini ya Mfalme Mohammed wa Tano.
Serikali ya Morocco, nikiutaja mfano mmoja tu, ilikisaidia sana chama cha KANU cha Kenya. Nakumbuka siku ambayo Joseph Murumbi, ambaye baadaye alikuwa makamu wa Rais wa Kenya, alivyokuwa akisafiria paspoti ya Morocco wakati Kenya ilipokuwa chini ya utawala wa Kiingereza.
Mbali ya nchi kuna na watu. Au tuseme ‘mijitu’, mashujaa wa ukombozi wa Afrika. Ninawadhukuru wachache tu hapa: Kwame Nkrumah, Ahmed Ben Bella, Gamal Abdel Nasser, Ahmed SekouTouré, Modibo Keita, Haile Selassie, Jomo Kenyatta, Julius Nyerere, Kenneth Kaunda, Patrice Lumumba, Agostinho Neto, Amilcar Cabral, Eduardo Mondlane na Samora Machel.
Nimewataja wanaume lakini kulikuwako na wanawake walioshika bunduki. Mfano mzuri ni Josi na Muthemba Machel wa Msumbiji.
Kweli sikatai kwamba baadhi ya hao mashujaa wa Kiafrika walizifuja nchi zao baada ya uhuru. Wengine waligeuka kuwa madikteta.
Lakini hayo ni mengine. Hayo ni ya hapo. Ya sasa ni mengine. Afrika ya leo si ya miaka 20 au 30 iliyopita. Imetoka mbali na imepiga hatua.
Sasa takriban nchi zote za Kiafrika ni huru (nchi 54) tukiziacha zile za Sahara ya Magharibi, Mayotte (kimoja kati ya visiwa vine vya Comoro ambacho bado kinatawaliwa na Ufaransa) na visiwa vya Chagos ambavyo ni vya Mauritius lakini vinavyokaliwa na Uingereza.
Sasa wakazi wa Afrika wanapindukia watu bilioni moja na idadi hiyo inaongezeka kwa kima cha watu wapatao milioni mbili na laki tatu kila mwaka.
La kutia moyo na ambalo wakati huohuo linatoa changamoto kubwa ni ujana wa wakazi hao wa Afrika. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo asilimia isiyopungua 70 ya wakazi haoni vijana walio chini ya umri wa miaka 25.
Changamoto inayotukabili ni kwamba wengi wa vijana hao hawana ajira. Na hawa si vijana wasiona ujuzi, wasio na elimu. Ni vijana waliosoma kuwashinda wazee wao.Lakini hawana mbele hawana nyuma.
Takwimu zinaonyesha pia kwamba Afrika inainuka kiuchumi.Lakini kuna tatizo:wananchi wanazidi kuwa masikini na kwenye kaumu hiyo wamo hao vijana.
Miaka zaidi ya 50 tangu 1960, uliokuwa ukiitwa Mwaka wa Afrika, bado hatuna uwezo wa kujilisha wenyewe. Ni wazi kwamba ile ajenda yetu ya kiuchumi NEPAD, imeshindwa kutukwamua.Lazima tujiulize kwanini?
Kwa nini madaktari wetu wanakimbilia Ulaya na Marekani ilhali tuna ukosefu mkubwa wa madaktari barani Afrika?
Kwa nini mpaka leo hatukuweza kuifanya iwe haki ya kimsingi kila mtu barani humu kupata maji safi na huduma ya afya?
Kwa nini serikali zetu zina tabia ya kuwaonea raia na kwa nini wanaume tunawaonea wanawake?
Kwa nini Muungano wa Afrika uwe unagharimiwa na wengine? Kwa nini takriban asilimia 90 ya fedha zake zinatoka kwa wafadhili, taasisi za kibeberu? Kwa nini baadhi ya nchi wanachama hazilipi ada zao?
Ikiwa hali ni hiyo ile dhana ya Umajumui wa Kiafrika si itajiangamiza yenyewe?
Tuna mengi ya kuuliza, mengi ya kusema, mengi ya kutufanya tufoke.
Lazima tutambue kwamba maslahi ya Afrika si sawa na maslahi ya madola makubwa au ya mabara mengine. Na tukitambua hayo inafaa tujiandae kuwawezesha vijana wetu hasa kwa vile wakazi wa Marekani na wa bara la Ulaya wanazeeka.
Ili Afrika izidi kupata ufanisi miaka 50 ijayo Umajumui wa Kiafrika utapaswa uunganishe nguvu zake na zile za serikali za Kiafrika, za Waafrika walioughaibuni na zile za mavuguvugu ya umma pamoja na asasi za kiraia.
Vijana wa leo wana jukumu kubwa la kuifafanua Ajenda ya Kiafrika itayoweza kuungwa mkono na wengi barani humu. Ili Umajumui wa Kiafrika uwe na maana katika karne hii ya 21 vijana watabidi wanadi waziwazi kwamba lengo lao ni ukombozi wa pili wa Afrika.
Ajenda yao iwe ni ajenda ya ukombozi, ya kuyakomboa mawazo. Lazima wahubiri mapinduzi,mapinduzi ya mawazo, mapinduzi ya namna tunavyojiangalia, mapinduzi ya kubadili jinsi tunavyo yakabili na kuyatanzua matatizo yetu.
Mapinduzi hayo au ukombozi huo ni muhimu ikiwa tunataka tuwe na kizazi kipya cha viongozi kilichoroa ari ya Umajumui wa Kiafrika.
Wale wasemao kwamba hii ni karne ya Afrika hawajakosea. Lakini lazima tuhakikishe kwamba hivyo ndivyo ilivyo.
Ikiwa vijana wetu hawatoweza kuanza kuibadili hali ya Afrika basi tusahau; Afrika itaendelea kubwagwa chini mpaka litapolia baragumu la mwisho wa dunia.
CHANZO: RAIA MWEMA

No comments:

Post a Comment