1 Juni, 2013
Polisi wamepambana tena kwa ghasia na waandamanaji wanaopinga serikali ya Uturuki.
Kitovu cha maandamano ni medani ya Taksim mjini Istanbul ambako polisi wametumia moshi wa kutoza machozi na ambapo ghasia nyingi zilitokea Ijumaa.
Mkaazi mmoja wa Istanbul aliiambia BBC kwamba watu zaidi wanaelekea katika eneo hilo:
"Watu 40,000 wanavuka daraja ya Bosphorus kutoka upande wa Uturuki ulioko Asia kuja ng'ambo ya Ulaya kujiunga na maandamano katika medani ya Taksim.
Safari zote za treni zimesimamishwa ili kuzuwia watu wasije, lakini wanatembea kwa miguu - kila mtu anatembea - na hapa nilipo naweza kusikia ghasia kutoka medani ya Taksim.
Tuko kama mwendo wa dakika 5 tu kutoka medani.
Kwa hivo nafikiri maandamano yanaendelea na pengine kuwa ya ghasia zaidi kushinda Ijumaa."
Maandamano yalianza siku nne zilizopita kupinga mpango wa kujenga maduka katika bustani iliyo karibu na medani ya Taksim.
Waandamanaji, ambao wengi ni vijana, wanaishutumu serikali ya chama cha Kiislamu kwamba inakuwa ya kimabavu.
No comments:
Post a Comment