Sunday, May 12, 2013

Syria yarejesha lawama zote kwa Uturuki

 12 Mei, 2013 - Saa 14:41 GMT

Syria imekanusha vikali tuhuma kutoka Uturuki kwamba ilihusika na miripuko miwili ya mabomu yaliyotegwa ndani ya magari Jumamosi katika mji wa wa mpakani wa Reyhanli, ambayo iliuwa watu 46.
Mji wa Reyhanli baada ya miripuko wa mabomu Jumamosi
Waziri wa Habari wa Syria, alisema serikali ya Uturuki ndio ya kubeba lawama kwa sababu imeruhusu eneo lake kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa.

Ilikuwa jawabu kali kutoka kwa serikali mjini Damascus ambayo imekanusha kabisa kuwa idara yake ya ujasusi ndio iliyofanya mashambulio ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari, na imewatupia lawama zote wakuu wa Uturuki.
Waziri wa Habari, Omran Zoabi, alisema serikali ya Uturuki ndiyo iliruhusu na kuwezesha silaha, mabomu, magari, wapiganaji na fedha kuvuka mpaka wake na kuingizwa Syria.
Hayo yamelifanya eneo la mpakani kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa; na viongozi wa Uturuki lazima wabebe dhamana ya kisiasa na kiutu.
Na upinzani wa Syria nao piya umeilaumu serikali ya Syria kwa mashambulio ya jana ukisema hilo ni jaribio la kuleta mzozo baina ya Uturuki na maelfu ya wakimbizi wa Syria waliopewa hifadhi na Uturuki.
Kuna hasira kati ya Waturuki kuwa vita vya Syria vimetapakaa na kuleta umwagaji damu nchini mwao.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kukutana na Rais Obama mjini Washington, hapo Alhamisi.

No comments:

Post a Comment