TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013
UTANGULIZI:Usiku
wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New
Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango
la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Soma zaidi....
Tukio
hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika
tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya
utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu
kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa
kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.Ukiacha matukio
hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi
Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012
huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya
mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani
kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia
kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa
risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.Kama hiyo haitoshi,
tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada
ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi
na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa
polisi walidhani Matutu ni jambazi.Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa
Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha
kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi
kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi
milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad,
iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya
kukamilisha uhalifu wao.Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa.
Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha
kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling'olewa meno
mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji hawa, katika unyama wa
ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na
kuondokana nayo.Hali hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza
na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki.
Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo,
ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.Katika kikao cha
Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano
na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio
hilo kubaini limetokana na nini.Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa
Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi
la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo
Vya Habari Tanzania (TMF). Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio
la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa
waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa
na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka. Timu hii imefanya kazi
usiku na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26.
Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi
wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo
vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari
zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi
5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa
tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya
kutekwa kwake.Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa
kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba
kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.Leo tunawasilisha
muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake,
itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa
kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold
stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia
ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea
ziafuatazo:
HADIDU
REJEA:1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa
kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na
viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi
dhidi yake.2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika
katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.3.
Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd
na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free
Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.4. Kuchunguza jambo
jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa
kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na
kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika
YALIYOJIRI
KATIKA UCHUNGUZI:1.0. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio
la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama
kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya
mashambulizi dhidi yake.Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika
eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi
yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo
wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au
kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo
viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata
kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama
ifuatayo:-
1.1. Wiki
tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi
aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na
Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa
limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia
hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na
polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya
kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.
1.2.
Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda
walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo
cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa 'alarm' ilipiga kelele,
Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.
1.3.
Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba
zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza
mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera
za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa
hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.
1.4. Kuna
askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane
kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo
mpango wa kumteka na kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na
wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake
Kibanda alisema:"Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia 'unaandika sana
usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini
nyumbani kwako'. Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari
sana."Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha
kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia,
niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha
kabisa."Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba
ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee
ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea."
1.5.
Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media
Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta
damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku,
ng'ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya
ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha
kuwapo kwa tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New
Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa
na kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na
hapa tunamnukuhu Kibanda:"Aliniambia Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu
Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa kutokana
na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali
au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima
madaktari wadhibiti sana blood clotting."Na kweli, nilivyoletwa hapa
Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila
siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina linahifadhiwa)
aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa na
kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa)
naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua."Ofisa huyu,
alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya
kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester united
kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda
alishambuliwa.
2.0.
Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo
wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.2.1. Familia ya Kibanda na
Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa
na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.
2.2.
Kibanda alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla
akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada.
Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. Aliogopa
kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu,
wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:"Nilivyoona ningefungua geti hata
mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya
simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu,
imani yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo
tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi."Mlinzi huyo
alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini
akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba.
Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi
saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda
walifanyafanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi
hicho. "Watu hawa wana mafunzo maalumu," anahitimisha.
2.3. Mke
wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti
na utaratibu wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni
hadi Kibanda anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia
televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia. Anasema hakusikia honi
wala tukio la Kibanda kutekwa. "Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza
kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala
mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza
sipati jibu."2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa
Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake
na kumwambia. "Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi."
Mwenzake alimwambia "Unaota maana kuna kelele za mpira." Siku hiyo
kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.Ni kweli
zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda
alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira.
Binti aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na
kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya
kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti
mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela
kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.2.5. Kibanda kwa upande wake,
anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili
wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha
akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, aliatokea
mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. "Mama Joshua
nisaidieeeeee."Katika kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake
wakisema mara tatu "Afande piga risasi." Kibanda alijaribu kupambana,
akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho,
lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu.
Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng'olewaje na wala
pingiri ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda
mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0.
Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na
nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free
Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
3.1.
Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia
Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama
ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari
imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na
tasnia ya habari kwa ujumla.
3.2.Mazingira
ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano
katika chumba cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na
imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New
Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani
ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni
hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince
Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi
huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
3.3. Timu
ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari
(2006) Ltd kwa kuwapo kundi la 'Habari Wazawa' na 'Habari wa Kuja'.
Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na
watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
3.4.
Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi
kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa
Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi
msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo
kuliko yeye Kibanda. Kwa maneno yake, anasema:"Nilihofu kuwa Mbowe
anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na
Mbowe au Ngurumo."Anasema alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika
kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana
ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada
ya makala hiyo, yalimshukuma aondoke.
4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.
4.1.
Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu
waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. Hata
hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe
aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph
Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha
Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2.
Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick katika naye alidai kuwa
ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya
kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha
taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza
kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
4.3.
Maelezo ya Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza
kuwa watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi
Mabibo, umbali ambao kwa kiwaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10.
4.4. Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku
anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka
Muhimbili. Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa
kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila
akarudishiwa mali zake zote. "Alipouliza amefuata nini polisi, akawambia
kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha
kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini," anasema Chongolo. Timu ya
uchunguzi ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa
chini.
4.5. Pia
taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya
madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo
(inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013.
Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa
5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.
5.1.
Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii
inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari
wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari
kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa
mwaka 2015.
5.2.
Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari.
Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina
ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Simu hizi hata habari za
kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka, ndani ya
vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika
habari fulani.
5.3.
Usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari
unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi.
Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi anasema: "Hili ni jambo muhimu
sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia."
5.4. Pia
alishauri waandishi wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo
inawataka wao kuwa ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya
kutegemea matakwa ya wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.
6.0. KILICHOBAINIKA:
6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi yake ya uandishi wa habari(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi(iv) Vitendo vya rushwa.
6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi yake ya uandishi wa habari(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi(iv) Vitendo vya rushwa.
6.2. Timu
imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na
rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa
walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa na kuumizwa
kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au
mapenzi.
6.3.
Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa
vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa
kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo
huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa kwa Kibanda na waandishin
wengine.
6.4.
Baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya
dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.6.5. Wanayataja
matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda
anaodaiwa kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare
kuwa vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja
kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.
6.6.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo
vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama
cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa
vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya
macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia
kujenga hoja hiyo.
6.7.
Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa
CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia
baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka,
kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na
wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali
yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa
njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia
CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli
ya Chadema kuwa NCHI HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9.
Dhana nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana
vita binafsi, hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika
mipango yao na hilo ndilo limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha
mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi
huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie Kibanda.
7.0. MAPENDEKEZO:Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.7.2.
Yanahitajika
marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba
vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari
inayokubalika.
7.3.
Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari
wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya
kuwawezesha wanahabari kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua
mara moja.
7.4. Kwa
kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia
matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi
na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT),
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika
kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.
7.5.
Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri
tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na
mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu
kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.
7.6. Kuna
viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa
au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama kuwania
madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola. Kwa
mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari wachukue
tahadhari kuanzia sasa.
7.7.
Taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili
vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria
hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.
8.0.
HITIMISHO:Ni dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza
katika siasa na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua
wajibu wa msingi. Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria
katika taarifa hii kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua
stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.Na kwa upande wa vyombo vya habari
na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha
usalama wa waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira
yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0. SHUKRANI:
9.1.
Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi
sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha
mwanga wa nini kilitokea.
9.2.
Tunapenda kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki
kikamilifu na kuiwezesha timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali
kufanikisha kazi hii.
9.3.
Tunapenda kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa
uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari
uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda.
Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye
lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.
9.4.
Tunawashukuru Kibanda, mkewe Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa
Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa
kwa Timu hii.
9.5.
Tunawashukuru wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na
ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.
10.0.
WAJUMBE WA TIMU:Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1.
Deodatus Balile – Mwenyekiti2. Pili Mtambalike – Mjumbe3. Jane Mihanji –
Mjumbe4. Tumaini Mwailenge – Mjumbe5. Rashid Kejo – Katibu
Mwisho....
No comments:
Post a Comment