Monday, July 1, 2013

Rais Barack Obama alipowasili Tanzania


Rais Barack Obama wakati wa ziara yake Afrika Kusini
Rais wa Marekani Barack Obama, amewasili nchini Tanzania katika mkondo wake wa mwisho wa ziara yake barani Afrika.
Ziara ya Obama inasemekana kulenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika huku kukiwa na wasiwasi kuwa Marekani inaachwa nyuma na China katika uhusiano wao na Afrika.
Obama amewasili Tanzania baada ya ziara yake ya Afrika Kusini ambako rais mstaafu Nelson Mandela anaugua.
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na familia yake pamoja na maafisa wake wa serikali na wacheza densi za kitamaduni walimkaribisha Obama na familia yake mjini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi wa Tanzania kupitia mitandao ya kijamii wamekosoa ziara ya Obama katika nchi yao, wakisema kuwa ziara yake imeathiri shughuli za maisha yao ya kila siku.
Obama alitembelea Senegal kabla ya kupitia Afrika Kusini na kisha Tanzania ambako ziara yake ya Afrika inaishia kabla ya kurejea Marekani.
Obama ameambatana mamia ya wafanyabiashara na swala la uchumi linatarajiwa kupewa kipamboele kwenye ajenda.
Aidha Obama atatembelea kiwanda cha kuzalisha umeme kinachomilikiwa na Marekani kufuatia tangazo lake mwishoni mwa wiki wa mpango wa mabilioni ya dola kufadhili mradi wa uzalishaji wa kawi.
Mpango huo wa miaka mitano, unatarajiwa kuwezesha nchi nyingi Afrika kuweza kupata kawi kwa ushrikiano na nchi zingine za Afrika na sekta binafsi.
Wakati wa ziara yake, nchini Afrika Kusini, kiongozi huyo wa Marekani hakumtembelea Mandela ambaye anasalia kuwa mahututi hospitalini akiigua maradhi ya mapafu.
Duru zinasema kuwa barabara zimefungwa na usalama kudhibitiwa vilivyo, mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment