Nigeria inapanga kuondoa baadhi
ya wanajeshi wake, kati ya 1,200 kutoka jeshi la kulinda amani la Umoja
wa Mataifa nchini Mali, Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara
ametangaza.
Rais Ouattara ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amesema wanajeshi hao
wanahitajika nyumbani kukabiliana na wanamgambo wa Kiislam.Haijafahamika bado ni vikosi vingapi vya Nigeria vitabakia Mali, ambako uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai.
Vikosi vya Ufaransa na Afrika viliwatimua wanamgambo wa Kiislam kutoka kaskazini mwa Mali Februari mwaka huu.
Jeshi la Umoja wa Mataifa sasa linashirikiana na jeshi la Mali kulinda usalama kwa ajili ya uchaguzi. Linatarajiwa kuongezeka hadi kufikia askari 11,200, pamoja na polisi 1,400 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi, katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Rais Ouattara amesema kuondolewa kwa wanajeshi hao kunatokana na matatizo ya ndani nchini Nigeria.
“Hawataondoa wanajeshi wote. Sehemu muhimu ya vikosi hivyo itabakia Mali,” amesema.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram walipoanzisha uasi mwaka 2009 ili kuunda taifa la Kiislam katika eneo lenye Waislam wengi la Kaskazini mwa Nigeria.
Hali ya hatari ilitangazwa tarehe 14 Mei katika majimbo ya kaskazini mashariki ya Adamawa, Borno na Yobe, huku zaidi ya wanajeshi 2,000 wakipelekwa kuvunja kambi za Boko Haram na operesheni za uasi.
Uchaguzi mkuu wa mwezi huu nchini Mali una lengo la kumaliza miezi ya mtafaruku wa kisiasa ulioanza baada ya wanajeshi kumpindua Rais Amadou Toumani Toure mnamo Machi 2012, na kuruhusu waasi na wanamgambo wa Kiislam kudhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Ufaransa ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa mali ilipeleka zaidi ya askari 4,000 Januari mwaka huu baada ya waasi kutishia kuuteka mji mkuu wa Mali, Bamako.
Nchi za Magharibi zimeahidi kutoa msaada wa dola za Kimarekani bilioni 43 kusaidia kufufua uchumi wa Mali, ukiwa unahusishwa na utekelezaji wa mpango wa maridhiano ya kisiasa na kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment