Mke wa Nelson Mandela, Graca
Machel amesema kwa sasa hana wasi wasi sana kuhusu afya ya rais huyo wa
zamani wa Afrika Kusini kama ilivyokuwa wiki chache zilizopita.
Bi Machel amesema hali ya Mandela inaendelea kuimarika kila uchao.Mandela ambaye ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mwenye umri wa miaka tisini na nne, anasemekana kuwa katika hali mahututi.
Mandela alilazwa hospitalini wiki tano zilizopita na hapo jana rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa mwanaharakati huyo wa uhuru amesalia kuwa mpiganiaji mkubwa kama alivyokuwa miaka hasmini iliyopita.
Mandela alilazwa hospitalini tarehe nane mwezi Juni, kutokana na maambukizi ya mapafu.
Wiki iliyopita, rais Zuma alipuuzilia mbali madai kuwa afya ya Bwana Mandela imezorota kiasi kwamba hawezi kupona tena.
Watu kadhaa ambao wamemtembela hospitalini wamesema kuwa Bwana Mandela angali ana ufahamu na anaweza kujibu na kuitikia salamu.
Mwandishi wa BBC Mjini Johannesburg, amesema kuwa Bi. Machel amekuwa kando ya mumewe tangu alipolazwa hospitalini na amejiepusha na mzozo unaokumba familia ya Bwana Mandela kwa wiki kadhaa zilizopita.
Maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kujiandaa kwa sherehe za kuadhimisha miaka tisini na tano ya kuzaliwa kwa Bwana Mandela wiki ijayo.
Mandela anaenziwa kote duniani kutokana na juhudi zake za kumaliza utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Alifungwa miaka 27 gerezani kabla ya kuachiliwa huru mwaka wa 1990 na kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka wa 1994.
No comments:
Post a Comment