Tanzania imekosolewa na gazeti maarufu la Marekani wakati Rais Obama akipokewa kwa nderemo na vifijo.
Gazeti hilo maarufu nchini Marekani la The New York Times, limechapisha
habari za kuonesha matukio ya ukatili yanayofanyika Tanzania.
Habari hiyo iliyochapishwa katika toleo lake ya Juni 30, imeleza tukio
la kuteswa na kuumiza kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen
Ulimboka.
Mwandishi wa habari hiyo amejaribu kunukuu kauli ya Dk. Ulimboka
akieleza jinsi alivyotekwa na kuteswa kinyama kisha kutupwa kwenye Msitu
wa Mabwepande.
Mwandishi huyo amesema kuwa Tanzania inaheshimika nje ya nchi kama
kisiwa cha amani ndani ya ukanda wenye machafuko wa Afrika Mashariki.
Kwamba kutokana na sifa hizo, Tanzania imejizolea sifa na ufadhili wa
fedha kutoka kwa mataifa mbalimbali yaliyoendelea, ikiwamo Marekani,
ambayo mwaka jana
iliipatia zaidi ya dola milioni 480.
Alisema kuwa wakati Rais Obama akiwasili Tanzania makundi ya kutetea
haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wanasema matukio ya vitisho
na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa yanashika kasi. “Kuna woga, si
amani”.
Ananukuu kuwa waandishi wamekuwa wakishambuliwa na
mmoja aliuawa akiwa anatekeleza kazi yake ya uandishi wa habari.
Aliongeza kuwa Julai mwaka jana, serikali ililifungia gazeti huru la
uchunguzi la kila wiki la Mwanahalisi, ambalo lilikuwa likiandika kwa
undani kuhusu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, ambalo
lilihusisha uhalifu huo na serikali ya Rais Kikwete.
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari yenye makao makuu yake New York
nchini Marekani, wiki jana ilimtaka Rais Obama kuliibua suala la uhuru
wa vyombo vya habari atakapokutana na Rais Kikwete jijini Dar es Salaam.
Gazeti hilo pia limetaja vurugu za kisiasa kuwa zilichukua sura mpya na
ambayo haikutegemewa wakati bomu la kurushwa kwa mkono lilipolipuliwa
katika mkutano wa
hadhara wa kampeni za uchaguzi wa madiwani wa
CHADEMA na kusababisha vifo vya watu wanne mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment