Saturday, June 8, 2013

Wasomali wakataa madai ya al-Shabaab juu ya chanjo ya polio

Kwa zaidi ya wiki mbili, wanamgambo wa al-Shabaab walishindwa kuzuia kampeni ya kitaifa inayoongozwa na serikali ya kuwakinga watoto dhidi ya polio, maafisa wa afya ya umma walisema.
Kama sehemu ya kampeni ya propaganda hiyo, wanamgambo walivamia mitaa katika maeneo wanayoyadhibiti ya Bulo Barde, Buale na Baardheere, wakieneza uongo kuhusu chanjo hiyo ili kuwatisha wazazi.
"Chanjo hii ni ajenda ya nchi za Magharibi dhidi ya Waislamu," wanamgambo walisema kwa kutumia vipaza sauti katika magari yaliyokuwa yanazungukazunguka, kwa mujibu wa Abdinur Dahir, mkaazi wa Bulo Barde mwenye umri wa miaka 46.
"Chanjo hii ina vitu vyenye sumu ambavyo vinaweza kuwafanya watoto wasiwe na uwezo wa kuzaa," wanamgambo hao walisema. "Chanjo hii ina virusi vinavyosababisha UKIMWI. Wakingeni watoto wenu!"
Vikundi vyengne vyenye uhusiano na al-Qaida vimeeneza proaganda kama hiyo inayolenga kampeni ya chanjo huko Afghanistan na Pakistan ya kuwakinga watoto dhidi ya polio, ugonjwa uliotokomezwa kwa kiasi kikubwa lakini unaoambukiza sana na inayoweza kusababaisha kupooza kusikotibika.
Wasomali wengi hata hivyo, walikataa kuamini madai ya al-Shabaab kuhusu hatari za chanjo hiyo.
Kwa kweli, familia nyingi ziliipokea vizuri kampeni hiyo na kukusanyika kwa makundi makubwa ili watoto wao wachanjwe, Yasin Nur alisema, afisa wa mpango wa chanjo katika Idara ya Afya kwenye Wizara ya Maendeleo na Masuala ya Jamii.
"Mahitaji haya makubwa kwa upande wa wazazi kuwachanja watoto wao kunadhihirisha kwamba madai ya kupotosha yaliyofanywa na al-Shabaab yameangukia patupu," Nur aliiambia Sabahi.
Serikali ya Somalia ilianzisha kampeni ya awamu mbili ya kuzuia polio katikati ya mwezi wa Mei baada ya kesi nne za polio kuthibitishwa katika miezi sita iliyopita. Awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, kuanzia tarehe 14 hadi 18 mei, ilikusudiwa kuwachanja zaidi ya watoto 440,000 wenye umri wa miaka 10 na chini ya hapo. Awamu ya pili, kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni, iliwalenga zaidi ya watoto 640,000 wa kundi la umri huo huo, Nur alisema.
Wizara ya Maendeleo na Masuala ya jamii iliendesha kampeni hiyo kwa msaada wa Shirika la Afya Duniani na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na mashirika mengine yasiyo ya kifaida.

Kushirikiana na vingozi wa jamii, kuwaelimisha wazazi

Katika kuelekea kwa kampeni hiyo ya chanjo, viongozi wa maeneo na viongozi wa kikabila na kidini waliendesha kampeni za matangazo ili kuzishawishi jamii kupuuza uvumi wa al-Shabaab na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwachanja watoto wao dhidi ya polio.
Isaaq Aadan, ambaye aliratibu kampeni katika mikoa ya Bay na Bakool, alitathmini kampeni ya matangazo huko kuwa ya mafanikio.
"Juhudi za mwamko za kuzihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hii zilisababisha familia nyingi kukubali kuchanja watoto wao kwa kuwa viongozi wa jamii, viongozi wa kidini na kambi za watu wa ndani waliokimbia makazi yao (IDP) waliwataka watu kutumia fursa ya chanjo hiii," Aadan alisema.
Kabla ya kampeni hiyo ya chanjo, timu za kuhamasisha jamii pia zilifanya matembezi ya nyumba kwa nyumba ili kuwataka wazazi wasiamini madai ya uongo yanayofanywa na al-Shaabab, alisema. Wafanyakazi wa afya waliwaamba wazazi kuhusu madhara ya kuambukizwa na polio na kwamba njia pekee ya kuwakinga watoto wao ni kupitia chanjo.
"Licha ya propaganda na uvumi ambao umekuwa ukienezwa na al-Shabaab dhidi ya chanjo ya polio, mpaka hivi sasa tumeshuhudia maendeleo kwa kiasi kikubwa kwa vile familia nyingi zimefahamu umuhimu wa kuwachanja watoto wao na ndio maana walizipokea timu za chanjo wakati wa kampeni," Aadan alisema.

Polio inasambaa katika maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabaab

Kampeni za chanjo zilifikia maeneo makubwa nchini na kuwafikia mamia ya watoto ambao huko nyuma walikuwa hawapati chanjo ya polio. Al-Shabaab hata hivyo, walipiga marufuku kampeni za chanjo katika maeneo yao wanayoyadhibiti na kuwazuia wafanyakazi wa chanjo wasiwafikie.
Marufuku hiyo inayaweka maisha ya watoto hatarini, wafanyakazi wa afya walisema.
"Ingawa kufukuzwa kwa kikundi hicho chenye msimamo mkali cha al-Shabaab kutoka miji mikuu ya kati na kusini ya Somalia kumewasaidia wafanyakazi wa afya kuwafikia watoto zaidi na zaidi na kuwapa chanjo ya polio ... virusi vya polio vinasambaa katika maeneo chini ya udhdibiti wa al-Shabaab kwa hivyo kuwa vigumu kuweza kuwafikia watoto [katika maeneo hayo]," alisema Said Yussuf, mfanyakazi wa chanjo.
Amina Mohamed, mama mwenye umri wa miaka 34 ambaye anaishi katika Kambi ya Tawakal mjini Mogadishu, aliwapeleka watoto wake wote kwa ajili ya kuchanjwa.
"Nimesikia kwamba al-Shabaab wanawataka akina baba na akina mama wote wasiwachanje watoto wao kwa misingi kwamba chanjo hii imetengenezwa na nchi za Kikristo, na ina vitu vya sumu ambavyo vingeweza kuwasababishia watoto kutoweza kuzaa watakapokuwa wakubwa," Mohamed alisema.
"[Wafanyakazi wa chanjo] walituambia kwamba madai haya na uvumi zilizopangwa na al-Shabaab ni sehemu ya propaganda [za kuchanganyikiwa] kwa kikundi hicho kwa ajili ya lengo lao la bure kwa gharama ya afya ya watoto wetu," alisema. "Kwa kweli, tunaelewa kwamba al-Shabaab hawako sahihi na kwamba ni kikundi kinachotumia picha potofu ya dini na kwamba madai na uvumi wanazosambaza zimeundwa ili kuwapotosha watu wa Somalia. Kwa sababu hii, tunakataa kukubali madai hayo dhaifu yanayoundwa na al-Shabaab."

No comments:

Post a Comment