Waziri Mkuu wa Uingereza David
Cameron ameandaa mkutano wa kimataifa jijini London utakaojadili njia za
kuisaidia Somalia kumaliza zaidi ya miongo miwili ya machafuko.
Mkutano huo utajikita zaidi katika masuala ya
kujenga upya vikosi vya ulinzi na kukabiliana na ubakaji ambalo ni suala
linalooonekana kama mwiko.Takriban watu saba waliuawa katika mlipuko wa bomu kwenye gari uliotokea katika mji mkuu Mogadishu siku ya Jumapili. Kundi la Al – Shabab ambalo lina mafungamano na Al – Qaeda linadai kuhusika na shambulio hilo.
Mkutano huo ambao utakua chini ya uenyekiti wa Bw. Cameron na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahamoud unafuatia mkutano kama huo uliofanyika London na jijini Istanbul nchini uturuki mwaka jana, huku wasiwasi ukiongezeka katika jumuiya ya kimataifa kwamba Somalia imegeuka hifadhi ya wanamgambo wenye mahusiano na al Qaeda.
“Ninamatumaini kwamba, wote tunaweza kuafikiana kuhusu mpango wa usalama wa muda mrefu, ambao utamaliza vitisho vya Al Shabab moja kwa moja,” alisema Bw. Cameron.
“Pia ninamatumaini tutaboresha uwazi na uwajibikaji ili watu wafahamu wapi rasilimali zinakwenda. Pia tunahitaji kuendelea na mchakato wa kulijenga taifa la Somalia, ikiwemo mikoa yote ya Somalia na nchi jirani hali kadhalika.”
Mchambuzi wa masuala ya Somalia wa BBC, Mary Harper anasema, kumekuwa na mabadiliko ya ghafla nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kuna serikali mpya, ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili kutambuliwa na Marekani, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na wadau wengine muhimu, anasema.
Hata hivyo, changamoto kubwa zimebakia, ambapo Al – Shabab bado wana uwezo wa kushambulia na serikali inategemea askari wapatao 18,000 tu wa Umoja wa Afrika (AU), kwa ajili ya kulinda usalama.
Somalia pia imegawanyika katika maeneo madogo ya mikoa inayojitawala, mingi ikiwa haipatani na serikali kuu.
Mkoa uliojitenga wa Somaliland na mkoa wenye mamlaka ya kati wa Puntland wamesema hawatahudhuria mkutano huo.
Mkutano utajadili suala ambalo mpaka hivi karibuni lilionekana kuwa mwiko nchini Somalia – ubakaji hasa kwa wanawake wanaoishi kwenye makambi ya watu wasiokua na makazi .
Mfanyakazi wa Kisomali wa shirika la msaada, Ali Adan ameiambia BBC kuwa, uamuzi wa kujadili suala hilo kwenye mkutano ni hatua kubwa .
“Unyanyasaji kingono ni jambo ambalo lilikuwa halizungumziwi nchini Somalia,” anasema.
Jumuiya ya Kimataifa yenyewe imeona umuhimu wa kujadili suala hilo haraka iwezekanavyo kwa sababu limekithiri.
Jumatatu nchi ya Qatar ilisema shambulio la bomu la Jumapili mjini Mogadishu liliwalenga maafisa wake, limearifu Shirika Rasmi la Habari la Qatar, QNA.
Maafisa hao wanne walikuwa wakisafiri kwa kutumia gari la kijeshi la serikali ya Somali wakati msafara wao uliposhambuliwa. Hakuna raia wa Qatar aliyejeruhiwa.
Hata hivyo, watu wengine 10 walijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC mjini Mogadishu.
No comments:
Post a Comment