Saturday, May 18, 2013

MAALIM SEIF AFUNGUA RASMI MRADI MPYA WA MAJI NUNGWI.


maji

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wananchi wa Nungwi kuulinda na kuuenzi mradi wa maji safi na salama katika eneo hilo ili uweze kuwa endelevu.

Amesema mafanikio ya mradi huo yatachangia maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo na kuwa mfano kwa maeneo mengine ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Maalim Seif ametoa wito huo katika sherehe za ufunguzi wa mradi wa maji safi na salama unaotokana na mabadiliko ya tabianchi katika shehia ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema mradi huo ambao ni wa kihistoria katika eneo hilo unapaswa kulindwa na kuenziwa ili usiharibiwe na n kuweza kudumu kwa muda mrefu.
Amefahamisha kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa vijiji vya Nungwi hasa wanawake, na kwamba umeondoa kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo hayo.
Aidha Maalim Seif amewata watendaji wa Mkoa huo kutowaone muhali waharibifu wa mazingira wakiwemo wale wanaochukua mchanga katika maeneo ya fukwe na maeneo mengine yasiyoruhusiwa, wanaofanya uvuvi haramu pamoja na ukataji wa miti ovyo.
Ameeleza kuwa zaidi ya maeneo 148 ya kilimo Zanzibar yameainishwa kuvamiwa na maji ya chumvi na kuathiri shughuli za kilimo katika maeneo mbali mbali sambamba na kupungua kwa eneo la ardhi ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Mara baada ya kufungua mradi huo, Makamu wa Kwanza wa Rais aliukabidhi kwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ili aweze kuundeleza kwa maslahi ya wananchi hao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa UNDP Tanzania Njeri Kamau amewapongeza wananchi wa Nungwi kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo, na kuwataka kuendeleza umoja na mshikimano katika kutekeleza miradi mengine ya maendeleo.
Amesema ametiwa moyo na mafanikio yaliyopatikana kutokana na mradi huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi wa Zanzibar katika kutekeleza miradi mbali mbali.
Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban, amesisitiza kuwa mradi huo ni kwa ajili ya wananchi wa Nungwi na sio kwa shughuli za mahoteli.
Aidha amesema wanakusudia kuweka “stabilizers” katika vituo vya mradi huo ili kuepusha uunguaji wa pampu za maji unaotokea mara kwa mara, hali inayosababishwa na hitilafu za umeme.
Mapema akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Dadi Shajak, amesema mradi huo ni mkubwa zaidi na umekuwa wa mwanzo kufunguliwa kati ya miradi minne unayotekelezwa chini ya mradi wa Mpango wa Mabadiliko ya Tabia nchi Afrika, African Adaptation Program AAP nchini Tanzania.
Amesema mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha lita thelathini elfu (30,000) kwa saa ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni mia tano (500), umefadhiliwa na serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini Tanzania, UNDP chini ya usimamizi wa AAP.
Akisoma risala kwa niaba ya wananchi wa Nungwi, mwalimu Hassan Jani Massoud ameishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao utapunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema kabla ya kuja kwa mradi huo, miradi mbali mbali ya maji ilianzishwa lakini haikuleta ufanisi, lakini mradi huo umeonesha kuleta mafanikio, na kwamba wananchi wa Nungwi wataondokana na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment