Serikali
ya Iraq inafikiria wazo la kuanzisha chuo cha mafunzo ya Taaluma ya
uchimbaji wa mafuta na gesi ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
katika azma yake ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya pande hizo
mbili.
Balozi
wa Iraq katika kanda ya Afrika Mashariki Dr. Adel Mustafa Kamil
ambaye makao makuu yake yapo Mjini Nairobi Nchini Kenya alisema Iraq
imeamua kufungua ukurasa mpya wa mawasiliano na marafiki zake ikilenga
zaidi mataifa ya Bara la Afrika.
Akizungumza
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini
kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar Balozi wa Iraq katika Kanda ya Afrika
Mashariki Dr. Adel Mustafa alisema hatua hiyo itaweza kuijengea Uwezo
Tanzania ambayo tayari imeshaonyesha dalili za kuwa na rasilmali hiyo.
Alisema
wakati Tanzania inajiandaa kuwa na muelekeo wa uchumi mpya ni vyema
mipango hiyo ikaenda sambamba na upatikanaji wa wana taaluma wazalendo
watakaokuwa na uwezo kamili wa kuendesha miradi hiyo kitaalamu.
Hata
hivyo Balozi Adel Mustafa alishauri kwamba itapendeza zaidi iwapo
baadhi ya wanafunzi hao wakapatiwa mafunzo ya mwanzo Nchini Iraq ili
kupata taaluma ya nadharia na ile ya vitendo.
Balozi
huyo wa Iraq Kanda ya Afrika ya Mashariki Dr. Adel Mustafa
alifahamisha kwamba Iraq imepita katika kipindi kizito cha vita
kilichopelekea kulega lega kwa uhusiano wake na Mataifa mengi Duniani.
Dr. Adel Mustafa alisema hatua inayoendelea kuchukuliwa na
Serikali ya Iraq hivi sasa ni kuwatumia Viongozi na maafisa wake
kuhakikisha uhusiano wake na nchi rafiki unarejea kama kawaida.
Katika
kuendelea kudumisha uhusiano wa pande hizo mbili Balozi Adel Mustafa
ametoa ombi maalum kwa Viongozi wa Juu wa Serikali zote mbili ile ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya
ziara maalum Nchini Iraq kwa lengo la kudumisha uhusiano huo.
“
Tunaanza kufarajika hatua kwa hatua kufuatia maombi tunayopokea kutoka
kwa mataifa yanayohitaji watendaji na wananchi wao kupatiwa fursa za
masomo Nchini Iraq “. Alifafanua Dr. Adel Mustafa Kamil.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alimueleza Balozi wa Iraq Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Dr. Adel
Mustafa Tanzania imefarajika kuona Iraq imerejea tena katika hali ya
utulivu na amani.
Balozi
Seif alisema migogoro ya kisiasa inayotokea au kubuniwa na baadhi ya
watu wakorofi popote pale duniani mara nyingi husababisha kuwakosesha
haki zao wananchi walio wengi.
Alieleza
kwamba amani ni muhimu na bila ya hilo hakuna maendeleo. Hivyo wananchi
wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla wanatarajia kwamba amani waliyonayo
Wairaq itawapa fursa ya kupiga hatua zaidi katika kuimarisha uchumi
wake.
“
Tanzania ilishtuka kidogo kutokana na mitihani iliyoipata nchi ya
Iraq. Lakini hivi sasa tumefarajika kusikia na wakati mwengine kuona
katika mitandao kwamba Iraq imerejea katika hali ya amani kama kawaida
yake “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimfahamisha Balozi huyo kwamba Zanzibar
inahitaji zaidi kupata fursa za taaluma katika kuwaendeleza wananchi
wake hasa katika sekta ya mafuta na Gesi.
Balozi Seif alisema Taifa la tayari limekuwa na uzoefu na kupiga hatua kubwa katika taaluma ya masuala ya mafuta na gesi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment