Tuesday, July 23, 2013

Migogoro ya ardhi yaathiri uchumi Afrika


Nchini Zambia kuna wakulima wengi wa Ngano
Ukuwaji wa uchumi katika bara la Afrika unakwamishwa na migogoro ya umiliki wa ardhi kubwa ya kilimo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na benki ya dunia.
Bara hilo ni makao kwa nusu ya ardhi ya kilimo duniani ingawa inakabiliwa na viwango vikubwa vya umaskini.
Lakini benki ilisema kuwa ukosefu wa wakulima kuthibitisha umiliki wa ardhi , matatizo ya kisheria na watu kupokonywa mashamba yao, zimekuwa changamoto kwa kilimo.
Sheria za ardhi zinapaswa kuboreshwa barani Afrika ikiwa bara hilo litaweza kufanikiwa kutumia rasilimali zake vyema na kubuni nafasi za kazi.
Makamu wa rais wa benki hiyo barani Afrika , Makhtar Diop, amesema kuwa licha ya kuwa na ardhi kubwa na madini bado ni bara maskini zaidi.
Wanawake ni asilimia sabini ya wakulima Afrika ingawa wananyimwa ardhi kutokana na mila za kitamaduni.
''Hali halisi, haikubaliki na lazima ibadilike, ili waafrika wote wanufaike na ardhi zao,'' alisema bwana Diop.
Ripoti hiyo inapendekeza kuwa serikali ziweze kuhakikisha jamii na watu binafsi kumiliki ardhi na hata kutumia teknolojia mpya kuweza kufanya utafiti na uchunguzi wa umiliki wa ardhi.
Mwandishi wa BBC Mark Doyle, anasema kuwa migogoro ya kisheria kuhusu umiliki wa ardhi, ni kawaida barani Afrika.
"ni kawaida katika maeneo ya vijijini kuwa mashamba hugawanywa miongoni mwa familia, na kusababisha hali ya mvutano kuhusu nani anamiliki nini.''
Benki hiyo imesema kuwa huu ndio wakati mwafaka kuweka vizuri sheria ya umiliki wa radhi ili waafrika wafaidike zaidi na kupanda kwa bai ya bidhaa na kuimarisha uekezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa usimamizi mzuri wa ardhi, pia utazuia wizi na unyang'anyi wa mashamba
Katika miaka ya hivi karibuni, waekezaji kutoka nchi tajiri zaidi wamenunua mamilioni ya hekari za mashamba na wao hudai kuwa mashamba hayo hayana wamiliki.

M23 wadaiwa kubaka na kuua DRC

 
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch limesema kuwa kundi la wapiganaji la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrsia ya Congo limewaua zaidi ya watu arobaini na kuwabaka zaidi ya wanawake na wasichana sitini tangu Machi mwaka huu.
Baada ya kuwahoji zaidi ya watu mia moja eneo hilo, shirika hilo lilisema kuwa waasi hao wanawasajili kwa nguvu vijana huko DRC na wengine kutoka nchi jirani ya Rwanda.
Kundi hilo limeongeza kuwa Jeshi la Rwanda bado linawasadia moja kwa moja waasi hao licha ya serikali ya Kigali kupinga hilo mara kwa mara.
Wakati huohuo, jeshi la DRC hapo jana lilishambulia ngome za waasi hao karibu na mji wa Goma Mashariki mwa DRC.
Haya yalikuwa mashambulizi ya kwanza tangu vita kati ya pande hizo mbili kuanza Jumatatu asubuhi na kusitishwa siku hiyo mchana.
Kundi hilo limesema liko umbali wa kilomita nne kutoka mji wa Goma, ingawa limesema lengo lake ni kulazimisha serikali kufanya mazungumzo nao wala sio kuteka mji wa Goma.
M23 liliuteka mji wa Goma, kwa siku kumi mwezi Novemba kabla ya kuondoka mjini humo kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa kufanya mazungumzo na serikali ya rais Joseph Kabila.
Mazungumzo na serikali yalianza mjini Kampala mwezi Disemba ingawa baada ya miezi miwili jeshi likaanza tena mapigano na waasi hao mwezi Julai tarehe 14.
Kulingana na Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha takriban watu 4,200 kutoroka makwao.

Saturday, July 20, 2013

Hotuba ya kwanza ya rais Adly Misri


Chama cha Muslim Brotherhood nchini Misri kimetoa wito kwa mamilioni ya watu kushiriki maandamano mengine dhidi ya hatua ya jeshi la nchi hiyo kumpindua kiongozi aliyechaguliwa Mohamed Morsi.
Katika taarifa yake, kiongozi wa Muslim Brotherhood Mohamed Badie, ametoa wito kwa jeshi kufikiria upya hatua yake na likubali wanachotaka watu.
Lakini katika hotuba yake ya kwanza tangu kuwa kaimu rais, Adly Mansour, ameahidi kuimarisha usalama na utulivu dhidi ya wale wanaotaka kuzusha ghasia nchini Misri
Wiki mbili baada ya jeshi kumwondoa mamlakani Mohammed Morsi, bwana Mansour alisema kuwa serikali yake itajitolea kuhakikisha kuna usalama na uthabiti.
Wakati huohuo, chama cha Muslim Brotherhood kimekataa kujiunga na baraza la muda la mawaziri lililotangazwa wiki hii.
"tunapitia kipindi kigumu, na baadhi wanataka vurugu ilihali tunataka kusonga mbele,'' alisema kaimu kiongozi wakati akitoa hotuba kwenye televisheni.
"tutapigana vita vya kuhakikisha kuna usalama na tutalinda mapinduzi.''
Bwana Morsi aliondolewa mamlakani tarehe tatu mwezi Julai katika kile wafuasi wake walisema ni mapinduzi ya kijeshi.
Jeshi hata hivyo linasema kuwa lilikuwa linatimiza mahitaji ya watu baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Nigeria kuondoa wanajeshi wake Mali


Jeshi la Nigeria
Nigeria inapanga kuondoa baadhi ya wanajeshi wake, kati ya 1,200 kutoka jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Mali, Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara ametangaza.
Rais Ouattara ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amesema wanajeshi hao wanahitajika nyumbani kukabiliana na wanamgambo wa Kiislam.
Haijafahamika bado ni vikosi vingapi vya Nigeria vitabakia Mali, ambako uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai.
Wanajeshi wa Nigeria ni sehemu ya jeshi la Afrika lenye askari 12,600 ambao walichukua jukumu la kulinda amani kutoka kwa Ufaransa Julai mosi mwaka huu.
Vikosi vya Ufaransa na Afrika viliwatimua wanamgambo wa Kiislam kutoka kaskazini mwa Mali Februari mwaka huu.
Jeshi la Umoja wa Mataifa sasa linashirikiana na jeshi la Mali kulinda usalama kwa ajili ya uchaguzi. Linatarajiwa kuongezeka hadi kufikia askari 11,200, pamoja na polisi 1,400 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi, katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Rais Ouattara amesema kuondolewa kwa wanajeshi hao kunatokana na matatizo ya ndani nchini Nigeria.
“Hawataondoa wanajeshi wote. Sehemu muhimu ya vikosi hivyo itabakia Mali,” amesema.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram walipoanzisha uasi mwaka 2009 ili kuunda taifa la Kiislam katika eneo lenye Waislam wengi la Kaskazini mwa Nigeria.
Hali ya hatari ilitangazwa tarehe 14 Mei katika majimbo ya kaskazini mashariki ya Adamawa, Borno na Yobe, huku zaidi ya wanajeshi 2,000 wakipelekwa kuvunja kambi za Boko Haram na operesheni za uasi.
Uchaguzi mkuu wa mwezi huu nchini Mali una lengo la kumaliza miezi ya mtafaruku wa kisiasa ulioanza baada ya wanajeshi kumpindua Rais Amadou Toumani Toure mnamo Machi 2012, na kuruhusu waasi na wanamgambo wa Kiislam kudhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Ufaransa ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa mali ilipeleka zaidi ya askari 4,000 Januari mwaka huu baada ya waasi kutishia kuuteka mji mkuu wa Mali, Bamako.
Nchi za Magharibi zimeahidi kutoa msaada wa dola za Kimarekani bilioni 43 kusaidia kufufua uchumi wa Mali, ukiwa unahusishwa na utekelezaji wa mpango wa maridhiano ya kisiasa na kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Mateka wa MSF waachiliwa na Al shabaab


Montserrat Serra (kushoto) na Blanca Thiebaut (Kulia) walipelekwa Somalia na watekaji wao

Wahudumu wawili wa shirika la madaktari wasio na mipaka - MSF wameachiliwa huru na wapiganaji wa Al Shabaab.Wahudumu hao walitekwa nyara mwaka 2011 katika kambi ya wakimbizi wa Kisomali kaskazini mwa Kenya.
Shirika la Medecins Sans Frontieres limesema kuwa wafanyakazi hao wawili wote wako salama na wenye afya na wanatazamia sana kujiunga na jamaa zao.
Montserrat Serra na Blanca Thiebaut walitekwa nyara kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab mwezi Oktoba mwaka 2011.
Kufuatia kutekwa nyara kwao pamoja na mateka wengine wa Kenya, nchi hiyo ililazimika kutuma vikosi nchini Somalia kupambana na wanamgambo wa al-shabaab.
Katika taarifa ya shirika hilo, ni afueni kubwa kwa shirika hilo kuweza kuthibitisha kuachiliwa kwa wanawake hao.
Wanawake hao walitekwa nyara tarehe 13 mwezi Oktoba mwaka 2011 na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki na ambao walifyatulia risasi gari la wanawake hao huku wakimjeruhi dereva aliyekuwa raia wa Kenya.
Kambi hiyo ya Dadaab ambayo ndiyo kambi kubwa zaidi duniani ya wakimbizi, inawahifadhi wakimbizi laki tano ambao wametoroka vita vya miaka mingi na njaa nchini Somalia ambayo inapakana na Somalia.
Bi Serra, ambaye ni mwalimu kutoka , Girona nchini uhispania, alikuwa mfanyakazi nchini Kenya kwa miezi miwili alipotekwa nyara. Alikuwa amefanya kazi na mashirika mengione ya misaada Amerika ya kusini na Yemen.
Moja ya magari yaliyotumiwa kuwateka nyara wafanyakazi hao

Mwanamke mwingine Thiebaut ambaye ni mhandisi wa kilimo, kutoka Madrid alikuwa ndio amekamilisha tu masomo yake ya digri katika chuo cha mafunzo ya uchumi mjini London alipotekwa nyara.
Kenya ililituhumu kundi la al-Shabab kwa kuhusika na utekaji nyara huo pamoja na matukio mengine sawa na hilo mwaka 2011 na hivyo kutishia usalama wa nchi.
Ilituma vikosi vyake nchini Somalia kuweza kupambana nao na kisha kuteka maeneo mengi ya nchi hiyo kutoka kwa kundi la al-Shabab.
Wanajeshi wake nchini Somalia sasa wamejiunga na kikosi cha jeshi katika muungano wa Afrika ambao wanasaidia serikali dhaifu ya Somalia.

Askari akamatwa kwa kudhalilisha maiti



Wanajeshi wa DRC wakitoa ulinzi katika eneo la Kanyarucinya, yapata kilomita 12 kutoka mji wa Goma.
Afisa mmoja wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametiwa nguvuni baada ya kuchafua maiti za wapiganaji wa waasi nchini humo.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa DRC, Lambert Mende, ameiambia BBC kwamba Luteni Solomo Bangala alizuiliwa jana Alhamisi na maafisa wa kijeshi baada ya mapigano kuzuka kati ya jeshi na waasi wa M23 katika eneo la mashariki karibu na mji wa Goma.
Kukamatwa kwa afisa huyo kunajiri muda mfupi tu baada ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon kuzungumzia madai ya kuwepo dhuluma na mateso dhidi ya wafungwa kutoka makundi ya waasi pamoja na wale waliouwawa zinazotekelezwa na wanajeshi wa Kikongomani.
Kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa kinatathmini upya hatua yake ya kuunga mkono vikosi vya serikali ya DRC kufuatia shutuma hizo.

Waasi wa M23
Mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23 yalianza siku ya Jumapili karibu na mji wa Goma.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien aliyepo katika mji wa Goma anasema uwanja wa mapigano ulikuwa takriban kilomita 7 katika vilima kutoka mji huo.
Hapajakuwa na mapigano yoyote katika kipindi cha siku mbili zilizopita na jeshi limesema limefanikiwa kuwafukuza waasi yapata kilomita 6, anasema mwandishi wetu.
Mwezi Novemba, wanamgambo wa M23 waliuteka kwa kipindi kifupi mji wa Goma, kisha wakaondoka baada ya kutimizia msururu wa ahadi ikiwemo kuanzisha mazungumzo na serikali.
Waasi wa M23, ambao kwa wingi wanatoka kabila la Watutsi walijiondoa katika jeshi la serikali mwezi Aprili mwaka 2012, na kuanzisha mapigano yaliyowaacha takrikaban watu 800,000 bila makao katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchini Uganda mwaka huu ili kushughulikia malalamishi ya waasi hao yamekwama.

Friday, July 19, 2013

Mapigano ya kikabila yazuka Kidal, Mali.


Wanajeshi wa Ufaransa walioko katika eneo hilo wameripotiwa kufyatua risasi hewani kutawanya makundi hayo mawili.
Wapiganaji wa kundi la waasi la MNLA nchini Mali
Machafuko hayo yanajiri wiki moja kabla ya kuandaliwa uchaguzi wa urais katika taifa hilo lililotekwa na wanamgambo wa kiislamu mwaka uliopita.
Wakati huo huo shirika la kutoa msaada, Islamic Relief, lenye makaazi yake nchini Uingereza limeonya kwamba licha ya mzozo kumalizika, eneo la kaskazini mwa Mali bado linakubwa na mkasa wa kibinadamu huku shule nyingi zikibaki kufungwa na masoko mengi kuahirishwa.
Mzozo uliopo kaskazini mwa mali umebuni kisiwa cha umaskini mkubwa katika eneo ambalo tayari limeathirika na kiangazi na uhaba wa chakula kabla ya vita kuzuka.
Shirika la Islamic Relief linasema watu milioni moja unusu sasa wanategemea chakula cha msaada , huku wengine milioni mbili wakikabiliwa na tishio la baa la njaa.
Waandamanaji wachoma magurudumu kupinga hatua ya jeshi kuingia mji wa Kidal Kaskazini mwa Mali
Hata kabla ya kampeni ya kuwatimua wanamgambo wa kiislamu iliyoongozwa na Ufaransa kuanza, takriban asilimia themanini ya chakula cha eneo hilo kilitoka maeneo ya kusini yenye rutuba nyingi au kutoka mataifa jirani ya Algeria na Libya.
Nyingi ya barabara za kufanyia biashara kuelekea kaskazini zimefungwa kutokana na hali duni ya usalama na masoko kuahirishwa. Shirika la Islamic Relief linasema vita vimesababisha uharibifu wa mfumo wa usambazaji maji huku mabomba pamoja na visima vya maji vikiharibiwa kabisa.
Shirika hilo linasema kiwango cha mateso wanayokumbana nao wakaasi wa kaskazini mwa Mali kinafumbiwa macho. Limetowa wito kwa jamii ya kimataifa kufadhili mpango wa dharura wa kutoa msaada pamoja na miradi ya maendeleo ya kudumu.
Islamic Relief limesema kuwa kwa upande wake, limetowa chakula cha msaada pamoja na mbegu kwa wakulima.