Katika kijiji kimoja Kaskazini mwa Tanzania,
ndege aina ya Boeing 747 zinatua kwenye kiwanja binafsi, magari yenye
nambari za usajili za milki za kiarabu, zikiendeshwa katika eneo hilo na
yeyote mwenye simu ya mkononi anapotua hapo hupokea ujumbe ambao
haukutarajiwa
''Hujambo mgeni na karibu UAE.''
Kwa karne nyingi, (Savanna) katika eneo la
Arusha lilikuwa makao kwa watu wa jamii ya wamaasai lakini siku hizi mtu
sasa anaweza kudhania yuko Dubai moja ya nchi za milki za kiarabu.
Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya ardhi mjini
Arusha hasa katika eneo la Loliondo karibu na mbuga ya kitaifa ya
wanyama ya Serengeti imekodishwa kwa kampuni ya uwindaji ya Emirati
iitwayo Ortello
Tangu mwaka 1992, kampuni hiyo imekuwa
ikiwapeleka kwa ndege watalii matajiri zaidi kuwinda simba na wanyama
wengine hali iliyowaghadhabisha wenyeji wa eneo hilo ambao ni wamaasai
ambao wamezuiwa kuwalisha mifugo wao katika maeneo ya kuwinda.
Sasa serikali ya Tanzania inataka kutoa ardhi
zaidi kwa wawindaji hao kwa lengo la kujenga barabara ya umbali wa
kilomita 1,500 ambako wanyamapori watakuwa wakipita kwa manufaa ya
kampuni hiyo ya uwandaji.
Mpango huo utawaathiri takriban watu 30,000
watakaoachwa bila makao na pia kuwaathiri maelfu ya wengine, ambao
huwalisha mifugo wao katika maeneo hayo wakati wa msimu wa kiangazi.
Wamaasai wameghadhabishwa mno na hata kufanya maandamano, wakisema kuwa maisha yao yataathirika pakubwa.
Zaidi ya asilimia ya 90 ya wakaazi wa Loliondo
ni wa Maasai ambao hutegemea kuwalisha mifugo wao nyasi kutoka eneo
ambalo serikali inanuia kuwakodishia waarabu.
"bila Ardhi hatuwezi kuishi,'' anasema mama Naishirita Tenemeri, mwenye watoto watatu.
Bi Tenemeri anafuga Ng'ombe na Mbuzi eneo la Loliondo, ili kuwanunulia chakula na kuwalipia karo ya shule wanawe.
Wa Maasai wana historia ya kupoteza ardhi yao
nchini Tanzania tangu wazungu walipowahamisha kutoka mbuga ya Serengeti
mwaka 1959.
Mapema mwezi huu, Bi Tenemeri, akiwa amejifunga
shuka yake nyekundu, alijiunga na watu 1,000 wengi wao wakiwa wanawake
chini ya miti ya mivule, katika kijiji cha Olorien kupinga mipango ya
serikali kuuza ardhi yao.
Wengine walitembea kwa siku nyingi kuonyesha ghadhabu yao kwa kujiondoa katika chama tawala cha CCM kama wanachama.
"ikiwa sina ardhi, sina mahala pa kujifungulia
watoto wangu,'' alisema Bi Morkelekei Gume,akitupa kadi yake ya
uwanachama wa CCM chini .
"mwanangu yuko katika shule ya upili, kwa sababu ya nyasi zinazotoka hapa.''
''Ikiwa wanataka ardhi yangu wanaweza kuniua.''
Mwanamke mmasaai anashikia bango linalosema
"tutapigania ardhi yetu hadi mwisho wake.'' Wanawake hapa ndio wamekuwa
wakisikika zaidi katika maandamano yao.
Wanawake wamekuwa wakisikika zaidi, wameathirika
zaidi kutokana na hatua ya serikali kuwafukuza, wakiachwa bila kazi
kuwalea watoto wao kwa hali ngumu wakati wanaume wakienda katika sehemu
za miji ambako wanapata kazi kama walinzi.
Pia wameongoza maandamano tangu viongozi wao wa
kisiasa waliopinga mpango wa ujenzi wa barabara waliokuwa wamesema
wataondoka katika chama tawala kukosa kutimiza ahadi zao.
Eneo la Loliondo lina wanyama wengi wa porini na
hivyo kuvutia watalii ingawa sio wengi. Linapakana na mbuga ya wanyama
ya Maasai Mara iliyoko Kenya pamoja na hifadhi ya wanyama ya Ngorongoro.
Waziri wa utalii Khamis Kagasheki anatetea hatua
ya serikali kutaka kuwaondoa wamasaai katika eneo hilo akisema kuwa
mradi huo utasaidia katika kuendeleza uhifadhi kwani Maasai wametumia
ardhi hiyo vibaya.
Lakini wasomi wanasema kuwa jamii ya wamaasai kawaida hawaathiri wanyamapori.
"nina swali moja kubwa kwa wanaosema kuwa
wamaasai ni tisho kubwa kwa wanyamapori kuliko kampuni hiyo ya kiarabu
ya OBC," alisema Benjamin Gardner wa chuo kikuu cha Washington na ambaye
amesomea maswala ya ardhi miongoni mwa wamaasai kwa miongo miwili.
Wamaasai hutegemea sana mifugo wao kwa chakula
Ni nadra kwa wamaasai kuwinda wanyama na hutumia ardhi kuzuia baadhi ya wanyama kujifungulia huko kwani ni tisho kwa mifugo wao.
Mashirika 13 ya kijamii kutoka kote nchini
Tanzania, yamesema kuwa wamaasai, wana vibali vichache sana vya kumiliki
ardhi, na kuwa serikali inawapotosha watu
Viongozi wa jamii hiyo wanapanga kwenda
mahakamani kuishtaki serikali, lakini wanahofia kuwa huenda swala hilo
likakosa kutatuliwa haraka kwani kuna kesi moja iliyowasilishwa mwaka
2009 na haijapata ufumbuzi hadi wa leo.