Takriban watu kumi na saba waliuawa katika makabiliano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.
Hii ni kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu, Red Cross.
Mapigano yalizuka baada ya waasi wa zamani waliokuwa wanashika doria katika Ikulu ya rais aliyeondolewa mamlakani
Francois Bozize kushambuliwa.
Msemaji wa serikali mpya alisema kuwa kiongozi wa waasi, Michel Djotodia alitangazwa kuwa rais wa mpito mnamo Jumamosi.
Kundi lake la waasi lilichukua mamlaka wiki tatu zilizopita.
Mapambano yaliyotokea Jumamosi na Jumapili yalikuwa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa mjini
Bangui tangu kung'olewa mamlakani kwa bwana Bozize.
Kombora liliangukia kanisa la Baptist siku ya Jumapili na kuwaua watu watatu.
Kasisi wa kanisa hilo alikatwa mkono wake baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye shambulio hilo.
Kundi la waasi la Seleka lililoipindua serikali ya Rais Fracois Bozize
Kaimu msemaji wa serikali ,generali Moussa
Dhaffane, alisema kuwa makabiliano yalizuka wakati vijana
waliwashambulia wanajeshi waasi, katika eneo Boy-Rabe, eneo
linalosemekana kuwa ngome ya bwana Bozize.
Maafisa wa shirika la Red Cross walisema kuwa watu 17 waliuawa katika sehemu mbali mbali za mji mkuu.
Wenyeji walisema kuwa vijana wengi wanataabika kufuatia hali mbaya ya usalama mjini Bangui.
Baadhi wakiwatuhumu waasi hao kwa uporaji.
Baraza la kitaifa la mpito, lililoundwa baada ya
kupinduliwa kwa rais Bozize lilimteua bwana Djotodia kama rais wa muda
siku ya Jumapili.
Taarifa iliyotiwa saini na Francois Bozize kutoka kwa idara ya mawasiliano ililaani vikali mapinduzi hayo.
Aidha bwana Bozize alikimbilia Cameroon wakati waasi walipowasili Bangui.
Bwana Djotodia alisema kuwa ataandaa uchaguzi katika kipindi cha miezi 18
Kundi la waasi la Seleka, lilitwaa mamlaka, baada ya mkataba wa amani waliotia saini na rais Bozize kusambaratika.