
Ashton alikutana na Morsi ingawa anasema hajui aliko
Mwakilishi wa mambo ya nje
katika Muungano wa Ulaya Catherine Ashton amekutana na Rais
aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohammed Morsi katika eneo
lisilojulikana. Morsi amekuwa akizuiliwa na jeshi tangu kuondolewa
madarakani mapema mwezi huu.
Ashton amewaambia waandishi wa habari mjini
Cairo kwamba Bw. Morsi alikua salama na kwamba alikubaliwa kutazama
habari kwenye runinga na kusoma gazeti.
Alisema walijadili haja ya Misri
kuganga yajayo na kuweka amani.Baroness Ashton amesema mchakato wa
utawala mpya sharti ushirikishe pande zote
Msemaji wa Bi Catherene Ashton, alisema kuwa
mkutano ulifanyika katika eneo lisilojulikana ambako Morsi anazuiliwa na
kuwa ulidumu kwa masaa mawili.
Hakutoa maelezo kuhusu walichokijadili.
Hata hivyo tayari ameshakutana na maafisa kadhaa
wa serikali akiwemo rais wa muda Adly Mansour, mkuu wa majeshi,
Generali Abdel-Fattah al-Sisi na makamu wa rais wa maswala ya
kigeni,Mohamed ElBaradei.
Alisema kuwa atatoa wito kwa pande zote mbili
kushirikishwa katika serikali. Ziara ya Ashton ambayo ni ya pili nchini
Misri inakuja baada ya wafuasi zaidi ya sabini wa Morsi kuuawa kwenye
makabiliano na vikosi vya usalama nchini Misri.
Wafuasi wa kiongozi huyo wamesema kuwa wanapanga
kufanya maandamano Jumanne huku serikali ya muda ikiwatahadharisha
dhidi ya kuhusika na ghasia na kuwa watakaovunja sheria watachukuliwa
hatua.
Maafisa wa usalama pia wametishia kuvunja
maandamano ya wafuasi hao waliopiga kambi nje ya medani iliyo karibu na
msikiti wa Rabaa al-Adawiya mjini Cairo.