Tuesday, July 23, 2013

Kiwanda cha kienyeji cha kutengeneza silaha chagundulika DSM

Kiwanda cha kienyeji cha kutengeneza vifaa na silaha mbalimbali,kimegundulika kuwepo jijini Dar es Salaam,ambapo wahusika wa kiwanda hicho wamekiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya unyang'anyi wa kutumia silaha ambayo yamesababisha mauaji mengi sehemu mbalimbali.
 
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam,kamishna msaidizi wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam DCP Ally Mlege,amesema katika hali ya kushangaza baada ya kukamatwa kwa baadhi ya watuhumiwa waliokuwa wakijihusisha na matukio ya ujambazi,hatimaye baada ya kubanwa na jeshi la polisi walikubali na kusema kiwanda hicho kilichopo maeneo ya Kawe Mzimuni kinatumika katika kutengeneza na kukarabati vifaa na silaha mbalimbali zinazotumika katika matukio ya uporaji na unyang'anyi ambavyo vilitumika na kusabisha mauaji mengi sehemu mbalimbali.
 
Aidha tapeli hatari bwana Mfaume Omary maarufu kwa jina la Mau(29)mkazi wa Magomeni Kagera,ameshikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kutumia namba tofauti za mitandao ya simu na majina ya watu maarufu ikiwemo viongozi wa serikali na viongozi wa dini kwa lengo la kujipatia fedha kwa kuvaa uhusika wa mtu husika bila wanaombwa fedha hizo kugundua.
 
Jeshi la polisi limekanusha vikali kuhusu habari zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuwa mbunge wa jimbo la Ubungo Mh John Mnyika amekoswa na bomu na kumjeruhi moja ya wafuasi wake kuwa ni la huzushi,na ukweli ni kwamba bomu hilo lililipuka ndani ya gari la polisi Pt .1902 wakati askari dcp Julius alipokuwa ndani ya gari akisogeza box lenye mabomu ya machozi na kwa bahati mbaya bomu hilo lililipuka ndani ya gari hilo lakini halikuleta madhara kwa askari polisi yeyote wala raia waliokuwa katika eneo hilo.
 
 

Maelfu wamlaki Papa Rio De Janeiro


Baba Mtakatifu Francis amelakiwa na maelfu ya mahujaji wa Brazil wakati akianza ziara yake ya kwanza ya nje tangu achaguliwe kuwa mkuu wa Kanisa Katoliki.
Baba Mtakatifu huyo wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini alitembelea jiji la Rio De Janeiro, akiwa kwenye gari la wazi na kisha kukutana na Rais Dilma Rousseff , katika kasri la taifa la gavana.
Baada ya kuondoka, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi, kuwatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali na gharama kubwa za ziara hiyo.
Yuko Brazil kuhudhuria Sherehe za Siku ya Vijana Wakatoliki Duniani.
Katika hotuba yake mara baada ya kuwasili, Baba Mtakatifu alitoa wito kwa vijana Wakatoliki kuwa manabii wa mataifa yote.
“Nimekuja kukutana na vijana kutoka sehemu zote duniani, waliovutika kwenye mikono ya Yesu Kristo Mwokozi,” amesema akiimanisha sanamu maarufu ya Yesu iliyopo katika jiji la Rio.
“Wanataka kutafuta hifadhi katika mikono yake, karibu kabisa na moyo wake ili wasikie wito wake kwa nguvu na wazi.”
Takriban saa moja mara baada ya sherehe za kumkaribisha, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na yale ya kushtua dhidi ya waandamanaji nje ya kasri.
Yalikuwa ni maandamano ya hivi karibuni ambayo waandamanaji wanasema ni ya kupinga vitendo vilivyokithri vya rushwa ndani ya serikali na nchi nzima.
Lakini baadhi yao wamechukizwa na dola za Kimarekani milioni 53 zilizotumika kuandaa ziara ya Baba Mtakatifu.
Kulikuwa na uharibifu kiasi na watu kadhaa kukamatwa, lakini ilikuwa kama ishara kwamba, upo uwezekano wa ziara hiyo ya kihistoria ya Baba Mtakatifu ikagubikwa na matukio yasiyo ya kawaida ya kisiasa.
Katika hatua nyingine, jeshi la Brazil limesema, bomu la kutengeneza nyumbani limegunduliwa karibu na eneo moja takatifu kati ya Rio na Sao Paulo ambalo kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki anatarajiwa kulitembelea siku ya Jumatano.
Bomu hilo lilikowa na nguvu kidogo, lilidhibitiwa baada ye.
Wakati Baba Mtakatifu Francis akiteremka kutoka kwenye ndege ya shirika la Alitalia, kwenye uwanja wa ndege wa Rio, mapema Jumatatu, alilakiwa na Rais Rousseff huku umati wa watu ukishangilia na alikabidhiwa shada la maua, huku kwaya ya vijana ikiimba wimbo unaohusu siku ya vijana.
Aliwapungia mkono watu na msafara wake kuelekea katikati ya Rio ambako maelfu ya mahujaji walikuwa wamekusanyika.
Baba Mtakatifu Francis alionekana mwenye furaha na kutulia wakati akielekea jijini Rio akiwa ndani ya gari la kawaida huku dirisha likiwa limefunguliwa na maafisa usalama wakihangaika kuudhibiti umati.
Kulikuwa na matukio ya fujo wakati gari lake lilipokwama kwenye moja ya msongamano wa magari katika jiji la Rio, baada ya dereva wake kukosea njia na kuzikosa zile zilioandaliwa kwa ajili ya msafara wa Papa. Mara umati ulizingira gari lake ukiwa na matumaini ya kumuona kwa karibu ama kumgusa. Mwanamke mmoja alimpitisha mtoto wake kwenye dirisha la gari ili Baba Mtakatifu ambusu.
Alipofika katikati ya jiji Papa alipanda gari la wazi lililoandaliwa maalum kwa ajili yake, huku akipunga mkono kwa maelfu ya watu waliojipanga pembezoni mwa barabara.
“Siwezi kusafiri kwenda Rome, lakini amekuja kuifanya nchi yangu kuwa njema na kuimarisha imani yetu,” alisema mzee mmoja wa miaka 73, Idaclea Rangel, huku akibubujikwa na machozi.
Mamlaka imeimarisha ulinzi wakati wa ziara ya siku saba ya Papa, kufuatia wiki kadhaa za maandamano nchi nzima kupinga rushwa na utawala mbovu.
Papa Francis alikataa kutumia gari maalum lisilopenyeza risasi, licha ya maombi kutoka kwa maafisa wa Brazil, maafisa wa usalama wapatao 30,000, jeshi na polisi wataimarisha ulinzi wakati wa ziara hiyo.
Zaidi ya vijana Wakatoliki milioni moja wanatarajiwa kukusanyika Rio kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani, ambyo huadhimishwa kila baada ya miaka miwili, ni sherehe za waumini Wakatoliki.
Papa huyo mzaliwa wa Argentina, ambaye alishika wadhifa huo Machi mwaka huu, anatarajiwa kuongoza ibada katika ufukwe wa pwani ya Copacabana siku ya Alhamisi na pia kutembelea moja ya vitongoji masikini.

9 wauawa kwenye ghasia nchini Misri


Watu tisa wameuawa mjini Cairo, Misri katika makabiliano yaliyodumu usiku kucha kati ya wafuasi na wapinzani wa rais aliyengo'lewa mamlakani Mohammed Morsi.
Maafisa wanasema kuwa , ghasia zilitokea wakati wa maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Morsi.
Familia ya Bwana Morsi imetuhumu jeshi kwa kumteka nyara kiongozi huyo wa zamani.
Rais huyo wa zamani amezuiliwa na jeshi katika sehemu isiyojulikana bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote, tangu mkuu wa majeshi Generali Abdul Fattah al-Sisi, kutangaza kung'olewa mamlakani kwa Morsi tarehe 3 Julai.
Chama cha Bwana Morsi cha Muslim Brotherhood kimekataa kutambua serikali ya kijeshi huku kikifanya maandamano karibu kila siku kote nchini Misri.
Ghasia hizo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 60 tangu kuondolewa mamlakani kwa Morsi.
Siku ya Jumatatu mtu mmoja alifariki na wengine wengi wakijeruhiwa wakati wa maandamano mjini Cairo, kwa mujibu wa maafisa wa afya.
Televisheni ya taifa iliripoti kuwa wafuasi wa Morsi waliokuwa wanaandamana walikamatwa kwa umiliki haramu wa silaha.
Vifo zaidi vimeripotiwa katika makabiliano mengine tofauti katika mkoa wa Qalyubiya Kaskazini mwa Cairo.
Wakati huohuo, familia ya Morsi ilisema hawajawasiliana kamwe na Morsi, na ikathibitisha kuwa wanaitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuanzisha uchunguzi juu ya kupinduliwa kwake.
Nchi kadhaa ikiwemo Marekani zimetaka Morsi aachiliwe.
Lakini maafisa wa kijeshi wanasisitiza kuwa anazuiliwa katika eneo salama.

Migogoro ya ardhi yaathiri uchumi Afrika


Nchini Zambia kuna wakulima wengi wa Ngano
Ukuwaji wa uchumi katika bara la Afrika unakwamishwa na migogoro ya umiliki wa ardhi kubwa ya kilimo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na benki ya dunia.
Bara hilo ni makao kwa nusu ya ardhi ya kilimo duniani ingawa inakabiliwa na viwango vikubwa vya umaskini.
Lakini benki ilisema kuwa ukosefu wa wakulima kuthibitisha umiliki wa ardhi , matatizo ya kisheria na watu kupokonywa mashamba yao, zimekuwa changamoto kwa kilimo.
Sheria za ardhi zinapaswa kuboreshwa barani Afrika ikiwa bara hilo litaweza kufanikiwa kutumia rasilimali zake vyema na kubuni nafasi za kazi.
Makamu wa rais wa benki hiyo barani Afrika , Makhtar Diop, amesema kuwa licha ya kuwa na ardhi kubwa na madini bado ni bara maskini zaidi.
Wanawake ni asilimia sabini ya wakulima Afrika ingawa wananyimwa ardhi kutokana na mila za kitamaduni.
''Hali halisi, haikubaliki na lazima ibadilike, ili waafrika wote wanufaike na ardhi zao,'' alisema bwana Diop.
Ripoti hiyo inapendekeza kuwa serikali ziweze kuhakikisha jamii na watu binafsi kumiliki ardhi na hata kutumia teknolojia mpya kuweza kufanya utafiti na uchunguzi wa umiliki wa ardhi.
Mwandishi wa BBC Mark Doyle, anasema kuwa migogoro ya kisheria kuhusu umiliki wa ardhi, ni kawaida barani Afrika.
"ni kawaida katika maeneo ya vijijini kuwa mashamba hugawanywa miongoni mwa familia, na kusababisha hali ya mvutano kuhusu nani anamiliki nini.''
Benki hiyo imesema kuwa huu ndio wakati mwafaka kuweka vizuri sheria ya umiliki wa radhi ili waafrika wafaidike zaidi na kupanda kwa bai ya bidhaa na kuimarisha uekezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa usimamizi mzuri wa ardhi, pia utazuia wizi na unyang'anyi wa mashamba
Katika miaka ya hivi karibuni, waekezaji kutoka nchi tajiri zaidi wamenunua mamilioni ya hekari za mashamba na wao hudai kuwa mashamba hayo hayana wamiliki.

M23 wadaiwa kubaka na kuua DRC

 
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch limesema kuwa kundi la wapiganaji la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrsia ya Congo limewaua zaidi ya watu arobaini na kuwabaka zaidi ya wanawake na wasichana sitini tangu Machi mwaka huu.
Baada ya kuwahoji zaidi ya watu mia moja eneo hilo, shirika hilo lilisema kuwa waasi hao wanawasajili kwa nguvu vijana huko DRC na wengine kutoka nchi jirani ya Rwanda.
Kundi hilo limeongeza kuwa Jeshi la Rwanda bado linawasadia moja kwa moja waasi hao licha ya serikali ya Kigali kupinga hilo mara kwa mara.
Wakati huohuo, jeshi la DRC hapo jana lilishambulia ngome za waasi hao karibu na mji wa Goma Mashariki mwa DRC.
Haya yalikuwa mashambulizi ya kwanza tangu vita kati ya pande hizo mbili kuanza Jumatatu asubuhi na kusitishwa siku hiyo mchana.
Kundi hilo limesema liko umbali wa kilomita nne kutoka mji wa Goma, ingawa limesema lengo lake ni kulazimisha serikali kufanya mazungumzo nao wala sio kuteka mji wa Goma.
M23 liliuteka mji wa Goma, kwa siku kumi mwezi Novemba kabla ya kuondoka mjini humo kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa kufanya mazungumzo na serikali ya rais Joseph Kabila.
Mazungumzo na serikali yalianza mjini Kampala mwezi Disemba ingawa baada ya miezi miwili jeshi likaanza tena mapigano na waasi hao mwezi Julai tarehe 14.
Kulingana na Umoja wa Mataifa mapigano hayo yamesababisha takriban watu 4,200 kutoroka makwao.