Friday, July 12, 2013

Maelfu wa raia Congo watorokea Uganda


Ramani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Maelfu ya watu wamekimbia makaazi yao nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya waasi kutoka Uganda kushambulia mji mmoja wa Mpakani.
Kwa mujibu wa mashirika ya kutoa misaada wapiganaji wa Allied Democratic Forces ADF, walivamia mji wa Kamango siku ya Alhamisi na kuanza kupora mali.
Msemaji wa jeshi la Uganda, Luteni Kanali Paddy Ankunda amethibitisha tukio hilo.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa takriban watu elfu kumi na nane wamevuka mpaka na kuingia nchini Uganda.
Kundi hilo la waasi wa ADF, lina makao yake katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini Mashariki wa Congo, eneo ambalo makundi mengine ya waasi yamesababisha maafa makubwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Msemaji huyo wa Jeshi Uganda Luteni Kanali Paddy Ankunda, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu kadhaa waliuawa kwenye shambulio hilo.
Ripoti zinasema waasi hao waliwateka nyara watu kadhaa akiwemo chifu mmoja wakati walipokuwa wakaitoroka kutoka mji huo
Kundi la ADF liliundwa miaka ya tisini, katika eneo la Magharibi mwa Uganda, lililazimika kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani baada ya kushambuliwa na jeshi la Serikali ya Uganda.

Hali ya Mandela imeimarika asema Bi. Machel

 
Picha ya Nelson Mandela na maua iliyoachwa nje ya hospitali na watu waliofika kumfariji
Mke wa Nelson Mandela, Graca Machel amesema kwa sasa hana wasi wasi sana kuhusu afya ya rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini kama ilivyokuwa wiki chache zilizopita.
Bi Machel amesema hali ya Mandela inaendelea kuimarika kila uchao.
Mandela ambaye ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mwenye umri wa miaka tisini na nne, anasemekana kuwa katika hali mahututi.
Mandela alilazwa hospitalini wiki tano zilizopita na hapo jana rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa mwanaharakati huyo wa uhuru amesalia kuwa mpiganiaji mkubwa kama alivyokuwa miaka hasmini iliyopita.
Mandela alilazwa hospitalini tarehe nane mwezi Juni, kutokana na maambukizi ya mapafu.
Wiki iliyopita, rais Zuma alipuuzilia mbali madai kuwa afya ya Bwana Mandela imezorota kiasi kwamba hawezi kupona tena.
Watu kadhaa ambao wamemtembela hospitalini wamesema kuwa Bwana Mandela angali ana ufahamu na anaweza kujibu na kuitikia salamu.
Mwandishi wa BBC Mjini Johannesburg, amesema kuwa Bi. Machel amekuwa kando ya mumewe tangu alipolazwa hospitalini na amejiepusha na mzozo unaokumba familia ya Bwana Mandela kwa wiki kadhaa zilizopita.
Maafisa wa serikali ya Afrika Kusini wametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kujiandaa kwa sherehe za kuadhimisha miaka tisini na tano ya kuzaliwa kwa Bwana Mandela wiki ijayo.
Mandela anaenziwa kote duniani kutokana na juhudi zake za kumaliza utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Alifungwa miaka 27 gerezani kabla ya kuachiliwa huru mwaka wa 1990 na kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka wa 1994.

Watu watano wauawa Mogadishu


Ramani ya Somalia
Watu watano wameuawa kwenye shambulio la bomu la kujilipua, lililolenga wanajeshi wa kutunza amani wa Muungano wa Afrika mjini Mogadishu, Somalia.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, ameiambia BBC kuwa ameona miili ya raia watano, ambao walikufa baada ya bomu hilo lililokuwa ndani ya gari kulipuka.
Muungano wa Afrika umethibitisha kuwa wanajeshi wake wawili walijeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo la Bomu, lakini kundi la Al shabaab lililo na uhusiano na kundi la kigaidi ya Al-Qaeda limewahi kufanya mashambulio kama hayo mjini Mogadishu.
Kundi hilo la Al-Shabab, linataka kuundwa kwa taifa la Kiislamu la Somalia, licha ya kuwa wapiganaji wake wametimuliwa kutoka mji mkuu wa nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Al Shabaab bado linadhibiti maeneo kadhaa ya Somalia.
Zaidi ya wanajeshi elfu kumi na nane wa Muungano wa Afrika wako nchini Somalia, kuisaidia serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na rais Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alichaguliwa na wabunge September mwaka uliopita

Maandamano zaidi kufanyika Misri leo


Wafuasi wa rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi
Wafuasi na wapinzani wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi wanajiandaa kwa maandamano makubwa mjini Cairo, huku waumini wa dini ya Kiislamu wakiadhimisha Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadan.
Wafuasi wa Bwana Morsi wanatarajia kuwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo, wataendelea kuunga mkono wito wao wa kutaka Bwana Morsi kurejeshwa madarakani.
Wapinzani wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.
Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema vuguvugu la Muslim Brotherhood huenda liliwatenga raia wengi wakati wa utawala wa Morsi, lakini bado raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi kuingilia masuala ya siasa.

Marekani kutuma ndege za kivita Misri

Siku ya Alhamisi serikali ya Marekani, ilitoa wito kwa utawala mpya wa Misri, kusitisha harakati zake za kuwakamata wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood na kuonya dhidi ya kulenga kundi lolote.
Wanajeshi wakishika doria mjini Cairo
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.
Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri.
Marekani inatarajiwa kupeleka ndege nne za kivita aina ya F-16 nchini Misri, lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini.
Serikali ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia mapinduzi.
Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa madarakani.

Marekani kutoa ndege za kivita Misri


Ndege ya kivita F-16
Marekani inaendelea na mpango wake wa kutoa ndege za kivita kwa jeshi la Misri licha ya msukosuko wa kisiasa unaokumba nchi hiyo. Hatua hii inajiri wakati Marekani ikiendelea kutathmini matukio ya wiki jana ambapo jeshi lilimuondoa madarakani Rais Mohammed Morsi.
Msaada wa kijeshi kwa Misri ungesitishwa endapo Marekani ingelitaja matukio ya wiki jana kama mapinduzi ya kijeshi. Kundi la Muslim Brotherhood linalomuunga mkono Morsi linasisitiza arejeshwe madarakani.
Wafuasi wake wamekua wakiandamana karibu na kambi kuu ya jeshi ambapo anaaminika kuuzuiliwa. Hapo Jumatatu,wafuasi wa Brotherhood 51 waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi wakati wanakabiliano.
Utawala wa mpito umesema kwamba Bw. Morsi anazuiliwa eneo salama na kwamba haki zake zinazingatiwa.Maafisa wa Marekani wamesema ndege mpya za kivita aina ya F-16 zitawasilishwa katika wiki chache zijazo.
Mpango wa kufadhili jeshi ulianza kutekelezwa mapema mwaka huu na jeshi inatarajia kupokea ndege 20 za kivita. Msemaji wa ikulu ya Rais amesema Marekani haitabadilisha mpango wa kufadhili jeshi la Misri, japo inaendelea kutathmini kuhusu matukio ya kisiasa. Msaada wa kijeshi nchini Misri ambao hutolewa na Marekani hufikia dola bilioni 1.3 kila mwaka.
Hapo Jumanne, kibali cha kumkamata kiongozi wa Muslim Brotherhood Mohamed Badie kilitolewa pamoja na wakuu wengine tisa wa kundi hilo. Viongiozi hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia mjini Cairo ambapo zaidi ya watu 50 waliuawa na mamia kujeruhiwa.

Dola Bilioni 1.1 kujenga upya Nigeria

 
Viongozi wa Nigeria na China mjini Beijing
China imekubali kutoa mkopo wa dola bilioni 1.1 kwa Nigeria ili kufadhili ukarabati wa miundo msingi.Mkataba huu umeafaikiwa wakati wa ziara ya Rais Goodluck Jonathan mjini Beijing,ambapo alikutana na mwenyeji wake Xi Jinping.
Fedha hizi zitasaidia ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na kujenga miji minne na njia mpya ya reli.China inawekeza kwa kiwango kikubwa Barani Afrika ambapo pia imekua ikipata raslimali za mafuta na madini.
Nigeria inaongoza kwa kuzalisha mafuta Afrika lakini kwa miaka imekua na miundo msingi mibovu, huku mamilioni ya raia wake wakiishi kwa umasikini. Bw. Xi amesema nchi mbili zinashirikiana kwa minajili ya kuboresha maisha ya watu wake.
Rais Jonathan anaongoza ujumbe wa wawekezaji wa Nigeria huko China na ziara ya siku nne itasaidia kuleta mshikamano wa karibu wa kibiashara.
Kampuni za ujenzi za Ki-China zimeanza kujenga barabara nchini Nigeria, kwa kandarasi ya dola bilioni 1.7.China kwa upande wake inatarajia kupata mapipa laki mbili ya matufa ghafi kutoka Nigeria ifikapo mwaka 2015.

Brotherhood kuendelea na maandamano


Wafuasi wa Brotherhood
Kundi la Muslim Brotherhood limeapa kuendelea na maandamano ya amani kupinga kuondolewa madarakani kwa Rais Mohammed Morsi na jeshi la nchi. Wafuasi wa Mosri wamekua wakiandamana mjini Cairo karibu na kambi kuu ya jeshi anakoaminika amezuiliwa.
Taarifa ya Brotherhood inajiri wakati kumetolewa kibali kuwakamata viongozi wake wakuu. Hapo Jumatatu wiki hii wafuasi wa kundi hilo zaidi ya 50 waliuawa katika makabiliano na jeshi.
Huku haya yakiarifiwa Marekani imetangaza kwamba itatoa ndege za kivita aina ya F-16 kwa jeshi la Misri katika majuma yajayo. Utawala wa Rais Barack Obama inaendelea kutafakari matukio yaliyotokea Misri wiki jana.
Ufadhili wa jeshi ungesitishwa mara moja endapo mwingilio huo wa jeshi ungelionekana kuwa mapinduzi. Hapo Jumatano maafisa wa Misri walitoa kibali cha kukamatwa viongozi wa Muslim Brotherhood akiwemo kiongozi mkuu Mohammed Badie.
Viongozi hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia ambapo wafuasi wao waliuawa pamoja na maafisa watatu wa usalama. Tayari ratiba ya uchaguzi mpya imetangazwa na Rais mpya anatarajiwa kuchaguliwa mwakani sawa na bunge.
Katiba itafanyiwa marekebisho na kupigiwa kura ya maoni kabla ya mwisho wa mwaka huu.Kundi la Brotherhood limepinga mpango mpya na kuapa halitashiriki mchakato wowote bila Mohammed Morsi kurejeshwa madarakani.