Jeshi la Nigeria
Nigeria inapanga kuondoa baadhi
ya wanajeshi wake, kati ya 1,200 kutoka jeshi la kulinda amani la Umoja
wa Mataifa nchini Mali, Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara
ametangaza.
Rais Ouattara ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amesema wanajeshi hao
wanahitajika nyumbani kukabiliana na wanamgambo wa Kiislam.
Haijafahamika bado ni vikosi vingapi vya Nigeria vitabakia Mali, ambako uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai.
Wanajeshi wa Nigeria ni sehemu ya
jeshi la Afrika lenye askari 12,600 ambao walichukua jukumu la kulinda
amani kutoka kwa Ufaransa Julai mosi mwaka huu.
Vikosi vya Ufaransa na Afrika viliwatimua wanamgambo wa Kiislam kutoka kaskazini mwa Mali Februari mwaka huu.
Jeshi la Umoja wa Mataifa sasa linashirikiana na
jeshi la Mali kulinda usalama kwa ajili ya uchaguzi. Linatarajiwa
kuongezeka hadi kufikia askari 11,200, pamoja na polisi 1,400 ifikapo
mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa
mataifa ya Afrika Magharibi, katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Rais
Ouattara amesema kuondolewa kwa wanajeshi hao kunatokana na matatizo ya
ndani nchini Nigeria.
“Hawataondoa wanajeshi wote. Sehemu muhimu ya vikosi hivyo itabakia Mali,” amesema.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu wanamgambo wa
Kiislam wa kundi la Boko Haram walipoanzisha uasi mwaka 2009 ili kuunda
taifa la Kiislam katika eneo lenye Waislam wengi la Kaskazini mwa
Nigeria.
Hali ya hatari ilitangazwa tarehe 14 Mei katika
majimbo ya kaskazini mashariki ya Adamawa, Borno na Yobe, huku zaidi ya
wanajeshi 2,000 wakipelekwa kuvunja kambi za Boko Haram na operesheni za
uasi.
Uchaguzi mkuu wa mwezi huu nchini Mali una lengo
la kumaliza miezi ya mtafaruku wa kisiasa ulioanza baada ya wanajeshi
kumpindua Rais Amadou Toumani Toure mnamo Machi 2012, na kuruhusu waasi
na wanamgambo wa Kiislam kudhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Ufaransa ambayo ilikuwa mkoloni wa zamani wa
mali ilipeleka zaidi ya askari 4,000 Januari mwaka huu baada ya waasi
kutishia kuuteka mji mkuu wa Mali, Bamako.
Nchi za Magharibi zimeahidi kutoa msaada wa dola
za Kimarekani bilioni 43 kusaidia kufufua uchumi wa Mali, ukiwa
unahusishwa na utekelezaji wa mpango wa maridhiano ya kisiasa na
kufanyika kwa uchaguzi mkuu.