25 Mei, 2013
Takriban watu laki tatu
wamekimbia makaazi yao katika jimbo la Darfur nchini Sudan, kufuatia
mapigano makali, katika miezi mitano ya kwanza mwaka huu.
Hii ni kwa mujibu wa afisaa mkuu wa UN kuhusu hali ya kibinadamu Valerie Amos."hatuwezi kuacha Darfur kuanguka kutoka kwa upeo wa jamii ya kimataifa,'' alionya Bi Amos, huku akiitaja hali kuwa yenye kutia wasiwasi
Watu milioni 1.4, wanasalia kuwa bila makaazi baada ya vita hivyo vya mwongo mmoja.
Takriban watu 300,000 wanakadiriwa kufariki tangu mwaka 2003, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Ingawa mzozo katika eneo hilo , umeshuka kwa kiwango kidogo, bado kumekuwa na maneo ambayo yamekuwa yakishuhudia vita tangu mwezi Januari, huku wanajeshi wa serikali wakikabiliana na waasi pamoja na makundi ya kikabila.
Bi Amos alisema kuwa wakimbizi wanalazimika kuishi katika mazingira mabaya huku wakikumbwa na uhaba wa chakula.
Aidha Bi Amos aliyatoa matamshi yake wakati wa ziara yake ya siku nne katika jimbo hilo kutizama hali ya kibindamu ilivyo na kukutana na rais wa Sudan Omar al-Bashir.
"wakati huu wa msimu wa jua, hawana chochote," alisema Bi Amos,wakati alipozuru kambi ya watu walioachwa bila makao iliyo nje ya mji wa El Fasher Kaskazini mwa Darfur.
"wangali hawana maji."
Maelfu ya watoto wanazaliwa nje ya kambi hizi na hawajahi kujua maisha mengine kuliko ya hapo kambini.
Bi Amos alisema kuwa mashirika ya kutoa misaada yanakabiliwa na wakati mgumu katika kuwasaidia watu milioni 1.4 wanaoishi kambini bila huduma za afya ,elimu na huduma nyinginezo muhimu.
Juhudi za kupeleka msaada huko, zimekuwa zikitatizwa na ukosefu mkubwa wa ufadhili pamoja na waasi kuzuia msaada kufikishwa katika maeneo yanayoiihitaji.