Maalim Seif ameeleza hayo
nyumbani kwake mbweni alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa Uingereza
ulioongozwa na Naibu Waziri anayehusika na Mambo ya Nje na Jumuiya ya
Madola, Mark Simmonds ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzi juu
mchakato wa katiba na maendeleo ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na
gesi asilia Zanzibar.
Amesema wakati Zanzibar
imeshaamua kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano, bado
inasubiri taratibu za kisheria ambazo zinaweza kupatikana baada ya
kukamilika kwa mchakato wa katiba.
Amesema mara baada ya
kukamilika kwa mchakato huo na suala la mafuta na gesi asilia kuondolewa
katika mambo ya Muungano, Zanzibar itatangaza zabuni za uchimbaji wa
mafuta na gesi asilia ambapo makampuni mbali mbali yataruhusiwa kuomba
zabuni hizo, na hatimaye kuanza rasmi kwa kazi ya uchimbaji.
Amefahamisha kuwa mchakato wa
katiba umefikia hatua nzuri baada ya kuanza kwa mabaraza ya katiba
tarehe 12/07/2013, ambayo itafuatiwa na bunge la katiba na baadaye
wananchi wataamua katiba hiyo kupitia kura ya maoni.
Kuhusu nishati ya umeme ambapo
Uingereza ni mshirika wa karibu wa nishati hiyo nchini, Maalim Seif
amesema Zanzibar imo katika mchakato wa kutafuta nishati mbadala
itokanayo na jua pamoja na upepo, ambapo tayari imeonesha mwelekeo
mzuri.
Amesema nishati hiyo
itakapopatikana itaondosha usumbufu unaojitokeza mara kwa mara na
kupunguza utegemezi wa upatikanaji wa umeme kutoka Tanzania Bara,
sambamba na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Aidha Maalim Seif ameelezea
mazingira ya uwekezaji Zanzibar, na kuuomba ujumbe huo kuhamasisha
wawekezaji kuja kuwekeza hasa katika sekta za utalii na uvuvi wa bahari
kuu.
Amesema Zanzibar ambayo kwa
sasa imetoa kipaumbelele katika sekta ya utalii, inakaribisha wawekezaji
katika ujenzi wa hoteli za nyota tano katika visiwa vya Unguja na
Pemba.
Ameongeza kuwa Zanzibar pia
ina mpango wa kujenga bandari ya kibiashara katika eneo la mpigaduni,
pamoja kuvifanyia matengenezo makubwa viwanja vya ndege, ili kuweka
mazingira bora zaidi ya uwekezaji.
Naye Bwana Simmonds amesema Uingereza itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo nishati.
Ameahidi kuwasiliana na
makampuni ya utalii, uvuvi na ujenzi ili kuangalia uwezekeno wa kuja
kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbali mbali nchini.