Sunday, May 12, 2013

MAMA AMCHOMA MOTO MTOTO WA WIFI YAKE SEHEMU ZA SIRI KWA KOSA LA KUNYWA UJI WA MTOTO



ELIZABETH Bureko (26), mkazi wa Kata ya Nyamatare, Manispaa ya Musoma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma, kwa tuhuma za kumchoma na moto sehemu za siri mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane.
 



Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Baraka Maganga, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Sajini Stephano Mgaya, kuwa mwanamke huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 24 mwaka huu, saa 3 asubuhi.


Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, mshitakiwa alikiuka kifungu cha sheria namba 169 cha mwenendo wa makosa ya jinai kama sheria hiyo ilivyofanyiwa marekebisho na kuwa namba 16, mwaka 2002.


Alidai kwamba, mshitakiwa huyo alimchoma katika sehemu zake za siri na mdomoni baada ya kumtuhumu mtoto huyo wa wifi yake, kwamba alikuwa akinywa uji wa mtoto aliyekuwa akimnywesha.


Mshitakiwa alikana shitaka na kurudishwa mahabusu hadi Mei 25 mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.

Nawaz Sharif afikiria kuunda serikali

 12 Mei, 2013 - Saa 09:44 GMT

Kiongozi wa chama cha Pakistan cha Muslim League, Nawaz Sharif, amezungumza na wenzake chamani kuhusu namna ya kuunda serikali yake mpya baada ya uchaguzi mkuu wa Jumamosi.
Nawaz Sharif kwenye kampeni
Matokeo yasiyo rasmi yanaonesha kuwa Muslim League itakuwa na viti vya kutosha bungeni kuunda serikali, lakini huenda kikahitaji kuungwa mkono na vyama vengine.
Bwana Sharif, ambaye amewahi kuwa waziri mkuu mara mbili kabla, alisema kuwa watu wameonesha wanaamini kuwa chama chake kinaweza kuleta mabadiliko.
Mcheza kriketi maarufu wa zamani, Imran Khan, ambaye huenda akawa kiongozi wa upinzani, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi; lakini alisema taarifa za udanganyifu kwenye kura zinavunja moyo.
Chama tawala cha PPP inaelekea kuwa kimeshindwa vibaya.

Syria yarejesha lawama zote kwa Uturuki

 12 Mei, 2013 - Saa 14:41 GMT

Syria imekanusha vikali tuhuma kutoka Uturuki kwamba ilihusika na miripuko miwili ya mabomu yaliyotegwa ndani ya magari Jumamosi katika mji wa wa mpakani wa Reyhanli, ambayo iliuwa watu 46.
Mji wa Reyhanli baada ya miripuko wa mabomu Jumamosi
Waziri wa Habari wa Syria, alisema serikali ya Uturuki ndio ya kubeba lawama kwa sababu imeruhusu eneo lake kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa.

Ilikuwa jawabu kali kutoka kwa serikali mjini Damascus ambayo imekanusha kabisa kuwa idara yake ya ujasusi ndio iliyofanya mashambulio ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari, na imewatupia lawama zote wakuu wa Uturuki.
Waziri wa Habari, Omran Zoabi, alisema serikali ya Uturuki ndiyo iliruhusu na kuwezesha silaha, mabomu, magari, wapiganaji na fedha kuvuka mpaka wake na kuingizwa Syria.
Hayo yamelifanya eneo la mpakani kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa; na viongozi wa Uturuki lazima wabebe dhamana ya kisiasa na kiutu.
Na upinzani wa Syria nao piya umeilaumu serikali ya Syria kwa mashambulio ya jana ukisema hilo ni jaribio la kuleta mzozo baina ya Uturuki na maelfu ya wakimbizi wa Syria waliopewa hifadhi na Uturuki.
Kuna hasira kati ya Waturuki kuwa vita vya Syria vimetapakaa na kuleta umwagaji damu nchini mwao.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kukutana na Rais Obama mjini Washington, hapo Alhamisi.

WHO yasema coronavirus yaambukiza

 12 Mei, 2013 
Shirika la Afya Duniani, WHO, linasema inaelekea sana kuwa aina mpya ya virusi vinavouwa, vya coronavirus, vinaweza kuambukizwa baina ya watu walio karibu sana.
Coronavirus
Virusi hivyo ni sawa na vile vya homa ya SARS (Severe Acute Respiratory Syndrome) na vinamfanya mgonjwa kuwa na shida sana ya kuvuta pumzi.
Nchini Ufaransa mwanamume mwengine hivi sasa ni mahtuti baada ya kuambukizwa na mgonjwa wa mwanzo nchini humo, ambaye walilazwa chumba kimoja hospitali.
Hadi sasa watu 34 wanajulikana kupata ugonjwa huo duniani tangu mwaka wa 2012, 18 kati yao walikufa Saudi Arabia.
WHO inasema ni muhimu kujulisha watu kuhusu virusi hivyo kwa sababu kuna wasi-wasi mkubwa kuwa vinaweza kusambaa.