18 Aprili, 2013 - Saa 12:06 GMT
Mwanawe rais wa zamani wa zamani
wa Senegal Abdoulaye Wade amezuiliwa na polisi baada ya kushtakiwa kwa
kosa la ufisadi ambalo limehusishwa na mali anayomiliki.
Karim Wade amekanusha madai kuwa alijipatia takriban dola bilioni 1.4 kinyume na sheria wakati wa utawala wa babake.Bwana Wade anadaiwa kumiliki makampuni ya kigeni kwa njia haramu.
Alikamatwa Jumatatu, saa chache kabla ya mawakili wake kutoa stakabadhi za umiliki wa mali yake mahakamani.
'Waziri wa ardhi na anga'
Wendesha mashtaka walitangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya bwana Wade na mawaziri wengine watano wa zamani mwaka jana.Hali hii ilianza kujitokeza baada ya Abdoulaye Wade kushindwa na rais Macky Sall katika uchaguzi wa Machi mwaka 2012 ambaye aliahidi kuangamiza ufisadi.
Wakati wa utawala wa miaka 12 wa Abdoulaye Wade, Karim Wade alishikilia nyadhifa kadhaa za waziri ikiwemo waziri wa miundo mbinu na usafiri wa angani.
Nyadhifa hizi zote alizoshikilia zilisababisha watu kumuita waziri wa anga na ardhi na pia ilimwezesha kusimamia kiwango kikubwa cha bajeti ya serikali