Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
imesisitiza kuwa itaendeleza utaratibu wa kuwafukuza wanafunzi wa vyuo
vikuu ambao watakuwa na tabia za utovu wa nidhamu na migomo isiyokuwa na
lazima.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo.
Alisema Serikali haina kigugumizi cha kuona ni kwa
nini isiwafukuze wanafunzi wa aina hiyo ambao wanakuwa ni kichocheo cha
migogoro.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza
la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ambaye alitaka kujua
mkakati wa Serikali kuwarudisha wanafunzi wa vyuo vikuu ambao
walifukuzwa masomo yao kutokana na migogoro iliyoibuliwa vyuoni mwao.
Katika swali la msingi Mnyika alitaka kujua hatua
za Serikali katika kuwarudisha wanafunzi hao kutoka vyuo vya Dodoma
(Udom), Dar es Salaam na Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi (MUHAS).
Mbali na hilo, aliomba ripoti ya Tume ya Rais
iliyoundwa mwaka 2011 kwa ajili ya kuangalia migogoro hiyo kwa wanafunzi
ambayo imedumu kwa muda mrefu ili ipelekwe bungeni na kujadiliwa kabla
ya kumshauri Rais jambo la kufanya.
Naibu Waziri alisema katika migogoro hiyo, kuna
maeneo ambayo wanafunzi walisimamishwa masomo na baadhi walirudishwa
masomoni, lakini wengine bado hawajarudishwa.
“Mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanafunzi
waliosimamishwa ni 99, lakini 78 walirudishwa na 21 hawajarudishwa, kwa
Udom walisimamishwa 570 lakini 563 walirudishwa masomoni na 7
wamefukuzwa kabisa, kingine ni MUHAS ambapo walisimamishwa wanafunzi 115
wengine wamerudi na wengine watarudi Desemba mwaka huu wakati wanafunzi
wawili wamefukuzwa kabisa,” alisema Mulugo.
Kuhusu ripoti ya Rais, Mulugo alisema ilikuwa ni
tume maalumu kwa ajili ya kumsaidia Rais, hivyo siyo lazima ripoti yake
kupelekwa bungeni kama ambavyo wabunge wanataka.