Watu wengi wanahofiwa kukwama ndani ya vifusi
Vikosi vya uokoaji vinasema,
watu wapatao 30 wamefariki dunia na mamia wengine wanahofiwa kukwama
baada ya jingo la ghorofa nane kuporomoka katika mji mkuu wa Bangladesh,
Dhaka.
Juhudi za ziada zinaendelea kuwaokoa watu
walionaswa kwenye kifusi. Watu wapatao 200 wamejeruhiwa kufuatia ajali
hiyo. Jeshi linasaidia shughuli za uokoaji katika eneo la tukio nje
kidogo ya jiji la Dhaka.
Matukio ya majengo kuporomoka nchini
Bangladesh ni ya kawaida kutokana na majengo mengi marefu kujengwa
kinyume na sheria za ujenzi.
Jengo lililoporomoka lilikuwa na kiwanda cha nguo, benki na maduka kadhaa. Liliporomoka asubuhi wakati watu wakielekea makazini.
Watu wengi wamekusanyika karibu na eneo la tukio
wakiwatafuta ndugu na marafiki. Mwandishi wa BBC mjini Dhaka anasema
haijafahamika kilichosababisha jengo hilo kuporomoka, lakini vyombo vya
habari nchini humo vimearifu kwamba, nyufa zilionekana kwenye jengo hilo
siku ya Jumanne.
Polisi wameviambia vyombo vya habari kwamba,
waliona ghafla sehemu ya nyuma ya jengo hilo ikianguka Jumatano asubuhi
na baada ya muda mfupi jengo lote likafuatia isipokua nguzo kuu na
sehemu ya ukuta wa mbele hali iliyosababisha taharuki.
Maafisa wanasema, ni sehemu ya chini pekee ya
jengo hilo la Rana Plaza ndio ilibakia imara baada ya kuporomoka, wakati
wanajeshi na waokoaji wa idara ya zimamoto wakiwa na vifaa vya kukatia
vyuma na matingatinga wakifukua kifusi ili kuwaokoa watu walionaswa .
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Mohammed Asaduzzaman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, hali ilikua mbaya sana.
Novemba
mwaka jana, moto uliounguza kiwanda cha nguo nje ya jiji la Dhaka uliua
watu 110 na kusababisha wananchi kupigia kelele kuhusu viwango vya
usalama kwenye viwanda husika.
Mara mwisho jengo la ghorofa nne
liliporomoka jijini Dhaka mnamo mwaka 2010 na kusababisha vifo vya watu
25 na wengine kadhaa kujeruhiwa.