Thursday, July 18, 2013

SAKATA LA SISTA WA KANISA KATOLIKI ALIYEBAKWA NA KUNDI LA WANAUME WATATU


Sista aliye mafunzoni ametekwa na kubakwa kwa wiki nzima na kundi la wanaume watatu katika kile kinachohisiwa kuwa ni shambulio la kulipiza kisasi, vyombo vya habari nchini India vimeripoti.

Sista huyo mwenye miaka 22 alidaiwa kutekwa kwenye stesheni ya treni na binamu zake na kisha kushikiliwa mateka na kubakwa kwa zaidi ya siku kadhaa sababu waliishutumu familia yake kwa kifo cha baba yao.


Ni tukio la karibu kabisa katika mfululizo wa mashambulio ya ubakaji nchini India mwaka huu tangu mwanafunzi alipobakwa na kundi la wanaume na kufa kutokana na majeraha yake ya kutisha ndani ya basi la Delhi Desemba mwaka jana.
 

Sista huyo aliwaeleza polisi alikuwa akutane na binamu zake kwenye stesheni ya treni karibu na Chennai, huko Tamil Nadu, kusini mwa India, baada ya kudai kwamba mama yao alikuwa anaumwa.
 

Hatahivyo, anasema alichukuliwa hadi kijiji cha jirani ambako alishambuliwa mara kadhaa.
 

Watuhumiwa hao baadaye walimrejesha kwenye stesheni hiyo na kumwonya asiripoti tukio hilo.
 

Binamu wa mwanamke huyo, Jotindra Sobhasundar mwenye miaka 30, na Tukuna Sobhasundar mwenye miaka 28, walikamatwa Jumapili, kwa mujibu wa ripoti.
 

Mtuhumiwa wa tatu alikamatwa Jumatatu baada ya mfululizo wa makimbizano katika wilaya ya Kandhamal.
Vyombo vya habari za mjini humo vilisema kaka wa Sista huyo alihojiwa kuhusiana na mauaji ya mmoja wa watuhumiwa. 

 
Shambulio hilo lilidaiwa kutokea kati ya Julai 5 na 11 lakini likatangazwa hadharani wiki hii.

Tukio hilo limelaaniwa vikali na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini India.

Kardinali Oswald Gracias, alinukuliwa akisema: "Ubakaji huu wa makundi ni ugaidi wa kimwili na kihisia.

Pia alizishutumu wakala za serikali kwa 'kukwepa wajibu wao'.

HABARI ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA "TANZANIA DAIMA" KUHUSU UDINI WA LIPUMBA YAWACHEFUA CUF

Habari iliyoandikwa na Gazeti la Tanzania Daima ikimhusisha Prof. Lipumba na udini  imewachefua  CUF  na  kuwafanya  watoe  waraka mkali wakiita Serikali kulichukulia hatua gazeti la Tanzania Daima kwa uchochezi wa kidini..
Chama    hicho  kimedai kuwa  Lengo la Gazeti la Tanzania Daima na Mwandishi wake ni kupandisha hasira za Waislam
--------------------------------------------------------------------
HUU  NI  WARAKA  WA  CUF:
CUF TUNASHANGAZWA NA JINSI SERIKALI INAVYOSHINDWA KULICHUKULIA HATUA GAZETI LA TANZANIA DAIMA KWA KUENDELEZA UCHOCHEZI WA KIDINI.

CUF-Chama cha Wananchi, kinasikitishwa sana na kitendo cha uchochezi wa Kidini unaofanywa na Gazeti la Tanzania Daima chini ya Muandishi George Maziku, kufuatia habari iliondikwa leo Tarehe 18/07/2013 toleo na 3149 . Aina hii ya uchochezi na Chuki ya Kidini anayoiendeleza bw, Maziku chini ya usimamizi wa Mmiliki wa Gazeti la Tanzania Daima na Mhariri wake, kwa maslahi ya Kisiasa tu, yatatupeleka mahala pabaya sana kama Taifa.

CUF-Chama cha Chama Wananchi tunashangazwa na tuna hoji juu ya lengo na Dhamira ya Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi wake nini juu ya muendelezo wa habari wanayoitoa kwa muda wa miezi miwili sasa ? Habari hii ina lenga nini ? Kwamba Viongozi wa Kisiasa wanaotokana na Dini ya Kiislam hapaswi kujumuika na Waislam wenzao kwenye Nyumba za Ibada ? Au waislam hawapaswi kujadili Maendeleo ya Taifa lao ?

CUF-Chama cha Wananchi tunaona Lengo la Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi wake ni kupandisha hasira za Waislam kwa mtazamo wa Ubaguzi wa Kidini kupitia tasnia ya Habari na hivyo kuleta machafuko yasiokuwa ya lazima.

Hata hivyo ikiwa lengo ni kuondosha Dalili za Udini kwenye mambo ya Siasa, hivi Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi wake hawakuona Waraka wa Uchaguzi wa Mwaka 2010 uliotolewa na Kanisa Katoliki na kupewa jina la IIani ya Uchaguzi wa Kanisa Katoliki ? Waraka ambao uliwataka Wakristo kuichagua Chadema na wagombea wake, Sio hivyo tu Waraka huo ulikwenda mbali zaidi na kuwatahadharisha Wakristo wasichague CUF na CCM na kuvifananisha Vyama vya CUF na CCM ni sawa na Chui waliovaa Ngozi ya Kondoo kwa Kanisa.

Waraka huo ulipingwa vikali sana na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru. Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi wake walikuwa wapi ? Mbona hatukuona waandike KANISA LA CHOCHEA UDINI ? Kama hiyo haitoshi, hivi Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi wake mbona hawakumkemea wala kuandika kuhusu Askofu Kakobe alipokua anampigia debe Mgombea wa Urais kupitia Chadema 2010 tendo ambalo lilikuwa linaonyeshwa wazi wazi kupitia Star Tv.

Kama hiyo haitoshi katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika jijini Arusha na Chadema kushinda wafuasi na viongozi wake kutuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) kuwa YESU AMESHINDA hilo nalo hukuliona?

Kama hiyo pia haitoshi ? Mwaka huu Mery Nagu amekwenda kusali Kanisani na kuwataka Wakristo wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya na kuwataka waumini hao wapinge mambo yote yanayotakiwa na kikundi kidogo cha baadhi ya watu kwa maslahi ya Kanisa, je huu haukuwa UDINI ? Lowasa kila kukicha yupo Makanisani na Misikiti na anatoa Fedha anatoa je hilo sio tatizo ?

Kwa mkusanyiko wa hoja zote hizi , CUF –Chama cha Wanainchi kinashindwa kuelewa kwanini Serikali haioni hatari inayofanywa na Gazeti la Tanzania Daima na Muandishi kwa tendo hili la Uchochezi wa Kidini ? Ikiwa Serikali iliweza kuzifungia Radio Imani na Radio Maria zote zikiwa zinarusha matangazo yake kwa Malengo ya Kuendeleza Dini zao, inashindwaje kulitazama Gazeti hili la Tanzania Daima ? Hivi Serikali inasubiri nini ? mpaka hao Waislam wanaotumiwa kuwa wadini waje juu na kuleta vurugu ? Ni busara kwa Serikali kulitazama jambo hili kabla halijalet madhara.

CUF-Chama cha Wananchi kinaishauri Serikali kulitazama kwa makini jambo hili, kabla halijaleta madhara, uandishi wa aina hii ndio uliosababisha Mauaji ya Kimbali. Uandishi wa Uchochezi unaolenga kuligawa Taifa kwa misingi ya Ukabila au Udini ni uandishi hatari sana kwa Taifa letu.

Bahati mbaya Tanzania Daima hawajui au wamesahau kwamba kwa chuki ya Kidini wanayojitahitahidi kuipandikiza ndani ya Taifa letu kwa nguvu ya Tasnia ya Habari, haitawaacha SALAMA wao kama Gazeti wala Muandishi wa Habari hiyo ya Uchochezi na wanapaswa kutambua kwamba kwa kufanya hivyo tu, basi wanainunua hatari ya Taifa letu kwa gharama kubwa.

Malengo ya Kisiasa yasije kulisambaratisha Taifa letu eti kwa sababu tu Chadema ichukue Nchi. Mnaweza kufikia Lengo la kuchukua Nchi kwa Mtazamo na Mkakati huo wa Kidini, kama ambavyo mnaendlea kufanya, lakini mjue kwamba mtachukua Nchi isokuwa salama. Maana mtakuwa mmeigawa Nchi kwa Matabaka ya Udini.

Kama kweli wewe ni mwandishi mahiri na mpenda amani katika nchi, tafadhali soma kitabu cha KANISA KATOLIKI NA SIASA YA TANZANIA BARA KUANZIA MWAKA 1953 HADI 1985 kilichoandikwa na Dr. John C. Sivalon na uje na uchambuzi wa dini uliomo katika kitabu hicho.

CUF- Chama cha Wananchi kinalitaka Gazeti la Tanzania Daima , kuanzia Mmiliki wake, Mhariri wake na Muandishi wa Habari hizi, ambae mara huandika kwa mtindo wa Makala , mara huzipa uzito mkubwa kadri anavyoona inafaa kwa utashi wa Kisiasa au Udini wake, kujitazama upya juu ya hili wanalolitengeneza kama litaiweka Nchi yetu katika eneo salama.

Mwisho CUF-Chama cha Wananchi kinaitaka Serikali kuchukua hatua juu ya Uchochozi huu.

Imetolewa na
Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Haki za Bainaadam na Mahusiano ya Umma
0719 566 567

--------------------

Ghana kuongeza umri wa kuolewa

 
Mtakwimu Mkuu wa serikali ya Ghana, Bi Philomena Nyarko, amesema umri halali wa mwanamke kuolewa unapaswa kuongezwa kutoka miaka 18 hadi 23.
Bi. Nyarko amesema, hatua hiyo itawafanya wanawake kujiandaa vyema kiakili na kimwili kuzaa watoto, na kwamba, itapunguza ongezeko la idadi ya watu nchini Ghana kwa kati ya 15% hadi 20%.
Mapendekezo yake yamekuja wakati Wabunge nchini Nigeria wanajadili kuhusu kupunguza umri wa kuolewa kutoka miaka 18 ya sasa ili watu waweze kuoa na kuolewa katika umri mdogo zaidi.
Baadhi ya Wabunge Waislam, wametoa hoja kwamba, kuzuia watu kuolewa kabla ya miaka 18, unakiuka sheria za Kiislam ambazo zinaruhusu ndoa katika umri mdogo.
Nigeria ambayo inaongoza kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, imegawanyika kati ya Waislam na Wakristo.
Bi. Nyarko amesema kwamba, wanawake wanaochelewa kuolewa ama kuzaa hadi umri wa miaka 23 wanakuwa na afya njema.
“Inafahamika vizuri kwamba, matokeo ya afya njema kwa mama na mtoto, endapo atachelewa kuzaa hadi msichana anapokuwa amekomaa vya kutosha kwa ajili ya kuolewa na kubeba mimba ili kuokoa maisha ya mama na mtoto”, amesema Bi. Nyarko.
Watu wengi nchini Ghana ambayo ina watu takriban milioni 25.5 ni Wakristo.

Munyenyezi ahukumiwa kifungo gerezani

Beatrice Munyenyezi
Mama mmoja ambaye alidanganya kuhusu majukumu yake katika mauaji ya halaiki nchini Rwanda, ili kupata hifadhi ya ukimbizi nchini Marekani, amekuhumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani.
Viongozi wa mashtaka wanasema kuwa Beatrice Munyenyezi, 43, ambaye alikwenda nchini Marekani mwaka wa 1998, kwa wakati mmoja alisimamia kituo kimoja cha ukaguzi ambako waathiriwa walichaguliwa ili kwenda kunyongwa.
Mama huyo amepewa kifungo hicho kwa kutoa habari za uongo kwa maafisa wa serikali.
Baada ya kukamilisha hukumu yake, Bi Munyenyezi atarejeshwa nchini Rwanda ambako anatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya halaiki.
Zaidi wa watu laki nane, wengi wao kutoka kwa kabila la Watusti, ambao ndio wachache nchini Rwanda, waliuawa mwaka wa 1994.
Munyenyezi ni mshukiwa wa kwanza kuhukumiwa nchini Marekani kuhusiana na mauaji hayo yaliyotokea nchini Rwanda.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mama huyo alilia mbele ya mahakama, mjini Concord katika jimbo la New Hampshire.
Wakati wa kesi hiyo, Jaji Judge Stephen McAuliffe alisema Munyenyezi alikuwa amepata uraia wa Marekani kwa njia ya ulaghai na udanganyifu.
Baada ya mauaji hayo kumalizika, alitorokea nchini Kenya ambako alifanikiwa kupata watoto wawili.
Baaadaye alikwenda nchini Marekani kama mkimbizi na alipata makao katika jimbo la Kaskazini Mashariki la New Hampshire, baada ya kusaidiwa na mashirika ya kutoa misaada.
Kisha alijiunga na chuo kikuu huku akifanya kazi katika ofisi moja ya serikali.
Lakini mashahidi waliliambia mahakama hiyo kuwa mama huyo alikuwa kamanda wa kituo kimoja cha ukaguzi mjini Butare Kusini mwa Rwanda, ambako Watutsi wengi waliuawa.
Mawakili wake wanasema wanapanga kukata rufaa.
Mume wake Arsene Shalom Ntahobali na mamake wanatumikia kifungo cha maisha nchini Rwanda baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda.

Shule zafungwa nchini Kenya


Wanafunzi Kenya
Wanafunzi nchini Kenya wakiwa darasani

Serikali nchini Kenya imetangaza kufungwa kwa shule zote za msingi za umma huku walimu wa shule za umma za msingi na sekondari wakisitisha mgomo wao.
Waziri wa elimu prof Profesa Jacob Kaimenyi amesema kuwa shule hizo zitabakia kufungwa kwa muda usiojulikana. Ameshutumu walimu akisema kuwa mgomo wao ulikuwa kinyume cha sheria.
Zaidi ya walimu laki mbili na arobaini wamesusia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wakidai nyongeza ya asili mia mia tano ya mishahara waliyoahidiwa na serikali mwaka wa 2007.
Pia wanataka kuongezewa marupurupu ya usafiri, ya nyumba na matibabu. Serikali imesema kuwa wazazi wataarifiwa juu ya siku ya kufunguliwa tena shule.
Waziri huyo wa elimu amesema kuwa wizara yake itafanya mipango maalum kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nane wanaotarajiwa kufanya mtihani wao wa kitaifa chini ya miezi minne ijayo.

Mzee Nelson Mandela afikisha miaka 95


Leo ni siku ya kimataifa ya shujaa wa kupinga Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela pia anaadhimisha siku ya kuzaliwa leo akitimiza miaka 95 akiwa bado amelazwa hospitalini.
Mandela amelazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.
Serikali ya Afrika Kusini imewaomba wananchi wake kusaidia watu wasiojiweza na kutenda mema kama heshima kwa Madiba.
Rais Barack Obama alimtakia kila la heri Mandela anayetambulika kama shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Madiba anasalia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wake wamethibitisha kuwa afya yake inaendelea kuimarika.
Naye rais Jacob Zuma amemtakia kila la heri Mandela katika sherehe za siku ya kuzaliwa kwake.
Watoto kwenye shule kote nchini humo walitarajiwa kuanzisha sherehe hizo kwa kumuimbia Mandela wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake katika siku ambayo pia iliadhimishwa miaka kumi na mitano ya ndoa yake kwa mke wake wa tatu Graca Machel.
Mwanawe Mandela wa kike, Zindzi, alisema Jumatano kuwa afya ya Mandela imeimarika pakubwa na kwamba alimpata akiwa anatazama televisheni huku akiwasiliana kwa macho yake na mikono alipomzuru wiki jana.
''Nina matumaini kuwa atarejea nyumbani wakati wowote sasa'' Zinzi aliambia shirika la habari la Uingereza Sky News.
Siku ya kimataifa ya Mandela iliwekwa na umoja wa mataifa kama njia ya kumkumbuka mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel kwa juhudi zake za kupatanisha watu.
Mandela anasifika kote duniani kwa juhudi zake za kumaliza vita vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Baadaye alichaguliwa kama rais wa kwanza mwafrika wa nchi hiyo mwaka 1994.
Chama cha kitaifa cha (ANC) kimesema kuwa katika siku hii ya kusherehekea siki ya kimataifa ya Mandela, ni heshima kwa miaka yake 95 kwa maisha yake aliyoishi vyema na ambayo ameitumia kupigania wananchi wa Afrika Kusini.