Kwa miaka 75, kina mama
wajawazito wamekuwa wakipewa na serikali visanduku vya karatasi.
Visanduku hivyo vimekuwa vikitolewa kama sehemu ya vitu muhimu vya
mwanzo kwa mtoto atakapozaliwa, kama vile vile nguo, mashuka na midori,
ambavyo pia vinaweza kutumika kama kitanda. Na baadhi ya watu wanasema
vitu hivyo vimeisaidia Finland kufanikiwa kuwa moja ya nchi ambayo ina
viwango vya chini kabisa vya vifo vya watoto duniani.
Imekuwa ni desturi iliyojengekea ambapo
visanduku vya karatasi hutolewa kwa mama wajawazito tangu miaka ya 1930
na imepangwa na serikali kutolewa kwa watoto wote nchini Finland, bila
kujali hali ya familia wanazotoka, ni mwanzo wenye usawa katika maisha
ya watoto.Vifaa vya uzazi - ni zawadi kutoka serikalini na ipo kwa mama wote wajawazito.
Vifaa hivyo ni pamoja na nguo za mtoto, mfuko wa kulalia, vifaa vya kumbebea nje ya nyumba, sabuni za kuogea na mafuta ya mtoto, pamoja na nepi, matandiko na godoro dogo.
Godoro likiwa ndani ya kisanduku cha karatasi linakuwa kitanda cha kwanza cha mtoto. Watoto wengi kutoka familia zenye hali tofauti za maisha, kwanza wanalala katika sanduku salama la karatasi la pembe nne.
Utamaduni huuu umedumu tangu mwaka 1938. Kwa kuanzia, mpango huu uliwahusu tu familia zenye vipato vya chini, lakini ukabadilika mwaka 1949.
"Si tu kwamba uliwalenga wanawake wanaotarajia kujifungua lakini sheria mpya ilimaanisha, ili kupata ruzuku hiyo, au sanduku la mzazi, walitakiwa kumwona daktari au muuguzi wa zahanati ya manispaa kabla ya kufikisha miezi minne ya ujauzito," anasema Heidi Liesivesi, ambaye anafanya kazi Kela - Taasisi ya Bima ya Jamii ya Finland.
Kwa hiyo sanduku hilo linakuwa na vitu muhimu ambavyo mama wazazi wanatakiwa kuwa navyo kwa ajili ya watoto wao wachanga, lakini pia inasaidia wanawake wajawazito kuwa katika uangalizi wa madaktari na wauguzi wa serikali ya Finland.
Katika miaka ya 1930 Finland ilikuwa nchi maskini na kiwango cha vifo vya watoto kilikuwa cha juu ambapo katika kila watoto 1,000 waliozaliwa, 65 walifariki dunia. Lakini hali hiyo ilibadilika haraka katika miongo iliyofuata.