
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad akipokea nakala
ya rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa
Makamu wa Rais Muungano Dkt Gharib Bilal, huku Jaji Mstaafu Joseph
Warioba akishuhudia
KAMA kuna wakati ambao Wazanzibari wamepata nafasi nzuri zaidi ya
kueleza hisia zao kuhusu mustakbali wa Muungano wa Tanzania, basi ni
kipindi kilichoanzia tangazo la Rais Jakaya Kikwete la kuleta fursa kwa
Watanzania kuandika katiba wanayoitaka.
Kwanza hiyo ni fursa ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza kwao kujadili
kwa uwazi suala hili ambalo limekuwa likiwasumbua kwa muda wote huo
tangu dola yao huru ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilipounganishwa na
Jamhuri ya Tanganyika Aprili 26, miaka karibu 50 iliyopita.
Ni fursa pia kwa Watanzania wa upande wa Tanganyika (nchi waliyojitia
kuiita Tanzania Bara) kujadili muungano wao kwa kuwa nao, kama walivyo
ndugu zao wa Zanzibar, wana maslahi makubwa kutokana na mfumo wa
Muungano huo ulioasisiwa kwa nguvu kubwa na aliyekuwa kiongozi wao mkuu
baada ya dola yao kupata uhuru Desemba 9 mwaka 1961, Mwalimu Julius
Nyerere.
Sababu ya pili ya kujitokeza kwa fursa ya kujadili suala la muungano kwa
uwazi ni ule ukweli kwamba Wazanzibari wanazo kumbukumbu nyingi za
namna walivyopoteza viongozi wake wakuu kwa sababu ya hatua za viongozi
hao kusimama kidete kutetea maslahi ya nchi yao, Zanzibar.
Alisumbuliwa Mzee Abeid Amani Karume kila alipotaka kubadilisha mwelekeo
wa Muungano. Mzee Karume aligundua mapema sana kwamba alilaghaiwa na
muasisi mwenzake wa muungano, Mwalimu Nyerere. Aligundua kuwa kumbe
mwalimu hakuwa na nia njema katika kutaka Muungano.
Ndio maana Mzee Karume mara tu alipotanabahi kuwa alizungukwa, aliamua
kila wakati kuchukua msimamo imara wa kuibakisha dola ya Zanzibar katika
mstari wa kuwa nchi inayojitegemea. Kwa bahati mbaya, alimudu mambo
machache tu lakini mengi yalimshinda kutokana na kubanwa na sheria
iliyokuwepo ya mamlaka kuvikwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Wazanzibari wangali wanakumbuka kauli mbalimbali za ukakamavu alizokuwa
akizitoa Mzee Karume kuonesha kupinga kuporwa mamlaka na Serikali hiyo.
Aliposema “Muungano ni kama koti likikubana livuwe,” aliposema “Muungano
mwisho Chumbe,” alipofukuza mawaziri kadhaa wa Mwalimu Nyerere
waliotumwa kuja kumwambia hili na lile, alipozuia safari ya wanajeshi wa
Kizanzibari kwenda Msumbiji kwa kuwa hakushauriwa wala kujulishwa na
muasisi mwenzake wa Muungano, Mwalimu Nyerere kuhusu safari hiyo,
alikuwa anadhihirisha kupinga mfumo wa muungano.
Alipokuwa ameandaa sarafu mahsusi ya Zanzibar huku akimkatalia Waziri wa
Fedha wa Mwalimu Nyerere, Mzee Amir Jamal aliyetumwa kuja kumshawishi
Mzee Karume kupeleka au kusalimisha hazina yake ya fedha Tanganyika, na
alipopeleka ujumbe wa kabineti yake kuwasilisha mapendekezo ya
mabadiliko ya mfumo wa muungano, yote hayo ni kudhihirisha alivyopinga
mapema muungano wa kinafiki.
Mapema kabisa, Mzee Karume alishuhudia namna muasisi mwenzake
alivyohalifu miadi kwa kuandaa sheria zisizokubaliwa na wote wawili –
badala ya zile zilizokubaliwa – ikiwemo ya kuwageuza watumishi wa
Tanganyika kuwa ni watumishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
kuzibadilisha sheria za Tanganyika kuwa ni sheria za Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kuunda Mahakama Maalum ya Kikatiba kwa ajili ya
kushughulikia mivutano ya kimuungano – na hivyo naye kuamua kwenda
kulingana na matakwa ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Mzee Karume alishuhudia vilevile, kuondolewa kwa sheria iliyoweka muda
maalum wa kudumu kwa muungano huo na kutathminiwa kama una maslahi kwa
washirika wake muda huo utakapokuwa umefika. Muda ulikuwa ni wa miaka
10, kwa maana ya kwamba ilikubaliwa itakapofika mwaka 1974, pande mbili
zilizoungana, Tanganyika na Zanzibar, zijadili kama muungano unakidhi
maslahi ya pande hizo.
Mzee Karume alipouliwa Aprili 7 mwaka 1972, miaka miwili kabla ya kufika
kwa muda wa kutathmini mwenendo wa Muungano, ikaonekana kama vile
ingekuwa mwisho wa harakati za Wazanzibari kudai haki ya mamlaka yao.
Sivyo.
Mauaji hayo yalikuwa machungu mengine kwa Zanzibar ambayo tayari
ilishashuhudia umwagikaji mkubwa wa damu ya wananchi waliodhulumiwa kwa
sababu tu ya kupigania nchi yao iliyoingizwa katika muungano wa
kilaghai.
Historia inaonesha viongozi wengi wa kisiasa hasa waliokuwa wasomi wa
hali ya juu pamoja na maulamaa katika Uislam, waliuliwa kwa siri na kwa
dhahiri kwa sababu ya misimamo yao hiyo ya kuisimamia haki ya Zanzibar
na Wazanzibari.
Hapo ndipo yanakuja majina makubwa na maarufu ya kina Jaha Ubwa, Othman
Sharif, Mdungi Ussi, Ibrahim Saadalla, Abdalla Kassim Hanga na wengineo
waliouliwa katika matukio ya kusikitisha wengine wakiwa hawakuzikwa na
jamaa zao.
Madai ya Zanzibar yaliendelezwa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aliyefuata
baada ya hapo, alisimama barabara kuitakia Zanzibar mamlaka yake. Kwa
kuwa mfumo wa kudhoofisha yeyote ambaye angeutilia shaka muungano
ulishajengwa na kuimarika kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda, juhudi
zake ziligonga mwamba.
Ilikuwa mwaka 1984 alipojikuta akihojiwa na Mwalimu Nyerere mbele ya
wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano, kwanini aliandaa waraka wa kutaka Muungano ubadilishwe ili
kuirudishia Zanzibar mamlaka yake.
Ilikuwa ni bahati mbaya kwamba Mzee Jumbe aliandaa waraka wa kuitetea
Zanzibar akiwa peke yake – hakumshauri au kumshirikisha yeyote kati ya
mawaziri wake wakati huo. Hili ni jambo lililoleta utata mkubwa kiasi
cha kusababisha mawaziri wa Serikali ya Zanzibar kumkana ilipotokea
kuulizwa kama walikuwa wanajua lolote kuhusu waraka aliouandaa Mzee
Jumbe.
Taarifa za ndani ya serikali zilieleza kwa umakini jambo hilo kuwa
ukweli Mzee Jumbe hakushirikisha kiongozi yeyote katika kuandaa waraka
huo na kwamba kwa vile wenzake hawakujua ni kitu gani hasa alichokusudia
kukipata – tena labda ilikuwa ni jambo la maslahi yake binafsi kuliko
nchi – wao waliona wangekumbwa wote na fagio.
Wakaukana waraka na kumtosa Mzee Jumbe. Ilikuwa ni bahati mbaya sana kwa
hakika kwa sababu hata kama ilikuja kudhihirika kuwa alichokiandaa
kilikuwa na maslahi makubwa ya kuikomboa nchi kutoka minyororo ya
kumong’onyolewa mamlaka yake, alilenga pia kujijenga kisiasa kwa nia ya
kutwaa madaraka ikitokea Mwalimu Nyerere kung’atuka.
Kilichomfika Mzee Jumbe baada ya hapo ni kulazimishwa kujiuzulu baada ya
kujitetea kwa ujasiri mkubwa, huku akitaka aachiwe arudi Zanzibar
ambako ndio angetangaza kujiuzulu kwa kuwa ndiko kwenye mamlaka yake.
Hakuruhusiwa, badala yake alijiuzulu palepale na kuanza kutengwa
kiulinzi huku akiwa amezuiliwa haki zake za kibinadamu.
Hizi ni pamoja na haki ya kuwasiliana na familia yake, haki ya kwenda
atakapo, haki ya kushirikiana na watu atakao na kadhalika. Simu
zilikatwa kwenye nyumba zake mbili, Unguja na Pemba.
Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyefuata hakuwa na makubwa zaidi ya kujitahidi
kuleta sera ya kuregeza masharti ya biashara hivyo kuchochea uingiaji wa
bidhaa nyingi nchini zilizosaidia kuinua uchumi wa nchi na mapato ya
wananchi. Alikaa kwa mwaka mmoja tu kupandishwa kwenda kuongoza Serikali
ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1985.
Katika awamu hizo mbili, Zanzibar ilianza kufunguka kidunia. Misingi ya
nchi ya kidemokrasia ilianza kujengwa. Ndipo Zanzibar ikapata katiba
yake huru baada ya ile iliyofutwa mara tu ilipoingia Serikali ya
Mapinduzi ambapo ilipindua katiba na sheria na kuweka mahakama za
wananchi badala ya zilizofuata sheria.
Paliandikwa Katiba ya 1984 ambayo ilikuwa na ruhusa ya haki zote za
kibinadamu – Bill of Rights – wakati tayari likiwepo na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar, mfano wa Bunge kwa nchi nyingine.
Mzee Idris Abdulwakil hakuwa na makubwa ingawa alikuwa na msimamo wa
dhati wa kuitetea Zanzibar kama ilivyodhihirika wakati fulani
alipoyaeleza baadhi ya mambo yanayopaswa kutizamwa upya kwa lengo la
kuiwezesha Zanzibar kukuza uchumi wake.
Hapo ikaja zama ya Dk. Salimin Amour Juma ambaye alikuwa akiuma na
kupuliza katika kutetea maslahi ya Zanzibar. Mara kadhaa alisikika akiwa
mkakamavu lakini akisalimu amri baada ya kutishiwa na uongozi wa juu.
Hili lilidhihirika alipoingiza Zanzibar katika Jumuiya ya Nchi za
Kiislam – Organisation for Islamic Conference (OIC) – mwaka 1994, na
kuitoa haraka baada ya Mwalimu Nyerere kutumia rungu la Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, Wazanzibari hawasahau jinsi serikali yake ilivyoandaa waraka
maalum wa kuyahoji masuala kadhaa yaliyo chini ya Muungano na kutaka
majadiliano. Kuna tume ya Amina Salum Ali iliyokuja na mapendekezo ya
kurekebisha masuala yanayoweza kuisaidia Zanzibar kiuchumi hasa kwa kuwa
eneo hilo halikuwa moja na mambo ya Muungano ndio maana Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) mpaka leo haitizami uchumi wa Zanzibar inapoandaa sera za
kifedha.
Ila inafurahisha kukuta kwamba pamoja na hasara zote hizo zikiandamana
na vitisho vya dola kubwa ya Tanganyika iliyojigeuza kinyemela na kuvaa
koti la Muungano, Wazanzibari hawakutetereka. Waliendelea kudai haki yao
ya kuondokana na utawala wa Waafrika wenzao.
Katika harakati zao paliandikwa vitabu na mashairi mengi kuelezea ubaya
wa kuikandamiza Zanzibar. Miongoni mwa vitabu hivi ni kile alichoandika
Abdulrahman Mohamed Babu kiitwacho I Saw The Future And It Works, Mzee
Jumbe kiitwacho The Partnership: 30 Years of Turbulent Zanzibar na
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru alichoandika Dk. Harith Ghassany,
Mzanzibari aliyelewea Uarabuni.
Hatua za sasa ni mfululizo wa jitihada za Wazanzibari kudai haki ya
kurudisha mamlaka yao ya kujitawala. Kama si sasa basi hakika ni halafu
hakutakuwa na namna ya kuzuia madai yao. Italazimu haki iachiwe
kusimama.
Chanzo: Fahamu – Kalamu ya Mzanzibari