Saturday, May 25, 2013

RIPOTI MAALUMU KUHUSU KUACHIWA HURU KWA "RAMA MLA WATU'


Mama na mtoto wake Waachiwa

Ramadhani Suleiman 'Rama mla kichwa' (kulia) na mama yake mzazi, Khadija (katikati) walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.
------------
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemuachiwa huru Ramadhani Suleiman (Rama mla kichwa) aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, baada ya kubaini hana akili timamu.
Jaji Rose Temba alitoa hukumu hiyo jana kutokana na ripoti ya Dk Mdeme Erasto iliyowasilishwa mahakamani hapo kuonesha kuwa, wakati mshitakiwa huyo anatenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
Ramadhani, ambaye alishitakiwa pamoja na mama yake Khadija Suleiman, alidaiwa kukutwa na kichwa cha mtoto Salome Yohana (3) katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili kikiwa katika mfuko wa plastiki maarufu kama rambo.
Jaji Temba alisema mshitakiwa alitenda kosa la mauaji, lakini kwa kuzingatia ripoti ya uchunguzi wa akili, mahakama haiwezi kumtia hatiani hivyo aliamuru mshitakiwa huyo awe chini ya uangalizi wa madaktari wa Hospitali za magonjwa ya akili na watatakiwa kuripoti maendeleo ya afya yake kwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Aidha mahakama ilimwachia huru mama mzazi wa mshitakiwa huyo, Khadija, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hakuwa na haja ya kuendelea kumshitaki.
Awali Wakili wa utetezi, Yusuph Shehe alidai kuwa mahakama ilitoa amri ya mshitakiwa kwenda hospitali kuchunguzwa kama ana akili na ripoti ya daktari iliwasilishwa mahakamani hapo na kubainisha kuwa hakuwa na akili timamu, hivyo aliomba mahakama imfutie mashitaka.
Akiwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao, Wakili wa Serikali Cecilia Mkonongo alidai kuwa Aprili 25 mwaka 2008 saa 2:25 usiku, Salome (marehemu) alikuwa anacheza na Ramadhan pamoja na mtoto Paschal Lucas lakini baadaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Alidai saa 2:30 usiku baba wa Salome, Yohana Mussa alikwenda kwa dada yake aitwaye Furaha ambapo Salome alikuwa akiishi, alipohoji mtoto wake yupo wapi ndipo wakaanza kumtafuta bila mafanikio, wakaamua kutoa taarifa kwa balozi.
Aliendelea kudai kuwa, asubuhi ya Aprili 26 mwaka 2008, wakiwa  njiani kwenda kituo cha polisi walipewa taarifa kuwa kuna kiwiliwili cha mtoto kimeonekana katika choo cha nyumba ya washitakiwa, walipokwenda walikuta mwili wa Salome ukiwa chini bila kichwa.
Mkonongo alidai wakiwa katika eneo la tukio, polisi walipata taarifa kuwa kuna mtu amekamatwa na kichwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walikwenda wakiwa na askari na ndugu wengine na kukitambua kichwa hicho.
Ilidaiwa kuwa, Ramadhani alikamatwa na mlinzi wa Hospitali hiyo akiwa na kichwa hicho na kudai anakipeleka kwa shangazi yake anayefanya kazi ya usafi katika hospitali hiyo.
Aprili 29 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na ripoti ya daktari ilionesha,  chanzo cha kifo chake hakikujulikana lakini, ilidai Salome alikatwa na kitu chenye ncha kali na alikuwa na michubuko mwilini.
Rama alipohojiwa na askari, alikiri kukutwa na kichwa hicho na kudai mama yake ndiye aliyemuua Salome kwa kutumia shoka na alikuwa anapeleka kichwa kwa shangazi yake.
Mama wa mshitakiwa huyo (Khadija)  alipohojiwa alikiri mwili wa marehemu kukutwa kwenye choo chake na ukiwa umefungwa na shati la Ramadhani.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, ndugu wa marehemu waliangua kilio, na walipotoka Upendo Dunstan (mama wa marehemu) na shangazi yake Furaha Mussa walikuwa wakiangua kilio huku baba wa mtoto akilia huku ameshika kiuno nje ya mahakama hiyo. 
Washitakiwa walirudishwa rumande kwa ajili ya kukamilisha taratibu, baada ya kusota rumande kwa zaidi ya miaka mitano.

JWTZ YAKANUSHA TAARIFA ZA ASKARI WAKE KUJIHUSISHA NA "BIASHARA YA KUKUNUA MALAYA " HUKO CONGO



Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, limekanusha taarifa zilizotapakaa kwenye mitandao kuwa askari wa jeshi hilo waliokwenda huko kwa ajili ya kulinda amani,wameanza kujihusisha na makahaba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Mtandao wa www.congodrcnews.com umedai wanajeshi wa Tanzania wameanza kujihusisha na ubakaji wanawake katika Mji wa Sake ulioko Goma.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa askari mmoja wa JWTZ alihitaji kujamiiana na mwanamke mmoja(Kahaba) kwa ujira wa Dola 50. Baada ya kumaliza shida zake ambazo ilielezwa alizifanya bila kinga yoyote,askari huyo alikataa kumlipa ujira wake,hali iliyoleta tafrani na mwanamke huyo kupiga kelele.

“JWTZ linapenda kuwaeleza wananchi kuwa taarifa hizo ni za uongo mtupu wenye nia ya kulipaka matope JWTZ na Tanzania kwa ujumla. “Picha iliyotolewa kwenye tovuti hiyo ya www.congodrcnews.com ni ya wanajeshi wa Tanzania walipokuwa katika Operesheni ya huko Comoro mwaka 2008.


Mtu anayeonekana kuwa chini ya Ulinzi alikuwa ni mshiriki wa Kanali Mohamed Bacar ambaye aliondolewa madarakani.

“Vilevile picha hiyo ilitolewa vile vile katika tovuti za www.apc.net.au/news/stories ya Machi 26, 2008 na ww.Seattletimes.com. na pia picha hiyo ipo pia kwenye tovuti ya Jamii Forum baada ya kufanya ‘link’ kutoka kwenye Mtando wa www.google.com.”

Taarifa hiyo ilisema kuwa JWTZ inapenda kueleza wananchi na dunia kwa ujumla kwamba wanaoneza taarifa hizo wana lengo la kukatisha tamaa juhudi zinazofanywa na nchi za Maziwa Makuu na SADC kuleta amani nchini DRC kwani JWTZ wako DRC kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji za Umoja wa Mataifa.  

Friday, May 24, 2013

WAASI WA M23 WATISHIA KUTUVAMIA MUDA WOWOTE....SERIKALI YA MKOA WA KAGERA YATOA TAHADHARI KWA WANANCHI

Serikali ya Mkoa wa Kagera imewatahadharisha wananchi wake kuepukana na wageni wasiowafahamu kwenye maeneo yao kutokana na tishio la kikosi chaM 23 cha nchini Congo DRC kinachotishia kuivamia Tanzania...
Kumekuwa na mapigano  makali  kati  ya waasi wa M23  na  vikosi vya serikali  nchini  Congo ambako jeshi letu lipo huko...
Waasi  hao  wametishia  kuivamia  Tanzania  muda  wowote  ili  kulipiza  kisasi.Miongoni mwa mipaka ambayo iko wazi  ni Kagera, na hii ndo sababu iliyopelekea  serikali ya Mkoa huo kutoa tahadhari kwa wananchi wake na watanzania kwa ujumla....
Credit: ITV

AIBU: MUME WA MTU ANASWA NA MWANAFUNZI WA KIDATO CHA PILI GESTI


INAUMA sana! Wakati wazazi wakihenyeka na wakati mwingine kujinyima ili mabinti zao waweze kupata elimu bora itakayowasaidia maishani mwao wapo wapuuzi wanaokatisha jitihada hizo.

Mwanaume mmoja aitwaye Taliki Juma mkazi wa Temeke – Wailesi jijini Dar es Salaam ameingia  katika  dimbwi la AIBU baada ya kunaswa akiwa na mwanafunzi wa kidato cha pili wakifanya mchezo mchafu.

 

Mbaya zaidi, bila haya wala soni, Taliki alimwingiza binti huyo (jina na shule anayosoma vinahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) katika chumba anachoishi na mwanamke anayedaiwa ni mke wake ambaye alikuwa safarini.

Chanzo chetu cha habari kilipiga simu chumba cha habari na kueleza juu ya tabia ya Taliki ya kwenda na denti huyo chumbani kwake tena akiwa kwenye sare za shule.

Kikao cha dharura kiliitishwa haraka baada ya sosi wetu kutoa maelekezo juu ya habari hiyo ambapo kwa muda huo na foleni za jiji la Dar usafiri uliopendekezwa ukawa ni pikipiki.

Haraka timu ya waandishi  wetu ilielekea eneo la tukio lakini kwa bahati mbaya walikwama.
 
Taarifa iliyopatikana kutoka kwa mtoa habari wetu ni kwamba, muda mfupi kabla timu haijaingia eneo la tukio, Taliki alifanikiwa kukwepa mtego baada ya kumuondoa denti huyo.

Wikiendi iliyopita Mei 18, mwaka huu chanzo chetu kilekile kilipiga tena simu kwa mwandishi yuleyule na kueleza kuwa jamaa kwa mara nyingine amemwingiza yule denti chumbani kwake.

Timu A iliondoka na kwenda moja kwa moja hadi eneo la tukio na kuliweka chini ya uangalizi huku timu B ikielekea katika Kituo cha Polisi cha Wailesi na kuomba ushirikiano wao.
Timu ya maaskari wa kituo hicho wakiwa tayari kwa lolote, waliungana na waandishi wetu kwenda eneo la tukio.
Waandishi wetu, maaskari na wazee wachache wa mtaani hapo walivamia katika chumba hicho na kufanikiwa kumnasa laivu Taliki akiwa na denti huyo kama walivyozaliwa akimfanyisha mambo ya kikubwa muda ambao alitakiwa kuwa darasani.

Binti huyo ambaye alionekana kushtuka sana baada ya kukutwa chumbani hapo, alieleza kuwa amekuwa katika uhusiano na Taliki kwa muda mrefu baada ya kumrubuni kwa fedha na zawadi mbalimbali.
“Ni kweli huyu hapa ni mpenzi wangu, huwa ananipa pesa. Nyumbani kwetu ni Mwananyamala na nimetoka nyumbani nikienda tuisheni lakini Taliki aliniambia nije kwake.
 
“Naombeni mnisamehe jamani. Mama akijua atanipiga sana. Nisameheni tafadhali na ninaahidi mbele yenu kuwa nitaachana kabisa na huyu mbaba (Taliki),” alisema denti huyo.
 

Denti huyo alitoa namba ya simu ya mama yake mzazi ambapo alipigiwa na kufika eneo la tukio na kujionea jinsi mtoto wake anavyoharibiwa wakati yeye akiwa kwenye juhudi za kumtengenezea maisha. 

Mama wa binti huyo, hakuamini alichokiona na alijikuta akimwaga machozi muda wote, watu wazima wakapata kazi ya kumtuliza.
UPUUZI WA TALIKI
“Ni kweli nakubali huyu ni mpenzi wangu na nipo naye muda mrefu ila naombeni sana mnisamehe, kwa kweli ni shetani tu alinipitia (Mh! Huyu shetani anasingiziwa mengi sana).
 
“Ndugu zangu wakijua hili jambo watanitenga, naombeni muwe na roho ya huruma (utadhani na yeye ana huruma), maisha yangu yataharibika (sijui alikuwa anamtengenezea yule binti  wa watu maisha?).”
 
Utetezi wake haukusaidia na badala yake alifikishwa katika Kituo cha Polisi Wailesi na kufunguliwa mashitaka katika Jalada namba WS/RB/585/2013 – KUFANYA MAPENZI NA MWANAFUNZI.

Thursday, May 23, 2013

ASKARI ALIYENASWA NA MAGUNIA 18 YA BANGI HUKO HIMO AWATOROKA POLISI

ASKARI Polisi Koplo Edward, anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya (bangi) gunia 18 huko Himo, Kilimanjaro tarehe 18, Mei 2013, ametoroka chini ya ulinzi wa askari polisi saba na kutokomea kusikojulikana.

Mtuhumiwa huyo alikuwa dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser namba PT. 2025 la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema askari huyo akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi saba, walikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya ukaguzi, na walipofika nyumbani kwa  mtuhumiwa, walimwamini na kumwacha kuingia ndani peke yake nao waliingia ndani ili kuendelea na upekuzi, na ndipo mtuhumiwa alipofungua mlango wa nyuma ya nyumba yake na kukimbia bila ya wao kufanikiwa kumkamata
 

Alisema polisi imemkamata Inspekta wa Polisi Izaack Manoni aliyekuwa anasimamia upekuzi huo: “Inspekta Manoni yupo chini ya ulinzi na hatua za kinidhamu dhidi yake zitachukuliwa,” alisema ACP Sabas na kuongeza:  
“Mtuhumiwa Edward, anayetafutwa kwa sasa alishafukuzwa kazi, akipatikana atafikishwa mahakama ya kiraia kusomewa mashitaka ya kufanya biashara ya dawa za kulevya,” alisema.

Alisema tayari mtuhumiwa mwenzake ambaye ni askari polisi mwenye namba G. 2434 PC George, amesomewa mashitaka yake jana.


Mbali na mtuhumiwa huyo, watuhumiwa wengine waliokamatwa na magunia 30 ya bangi wilayani Arumeru nao wamepandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yao.

HALI BADO NI MBAYA MTWARA....WANAFUNZI WAWILI WAMETANDIKWA RISASI, MMOJA AMEFARIKI HAPOHAPO

Mwandishi wetu aliyepo Mtwara ametueleza kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wa eneo la magomeni mkoani mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo..

Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari magereza . Mwanafunzi wa CHUNO amefikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.  
Mwanamke mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 mjamzito ameuawa kwa kupigwa risasi maiti ipo Ligula.




Kwa sasa ( jioni  hii) inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokua eneo la magomeni ambako mbomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule

PICHA ZA SHEHA WA TOMONDO- ZANZIBAR ALIYEMWAGIWA TINDIKALI JANA USIKU

\
Sheha Mohammed Omary Said aliyemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana akiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja akipatiwa matibabu, Sheikh Mohammed amepata maumivu makali sehemu za kifuwa na jicho kuumia

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,Mukhadam Khamis,amesema chombo kilichotumika kumwagia tindikali Sheha huyo kilipatikana eneo la tukio na kwamba polisi imekichukua kwa kukichunguza kitaalam ili kugundua aliyekuwa akikitumia kwa kuangalia alama za vidole.

Sheha huyo alimwagiwa tindikali jana usiku wakati alipotoka nje ya nyumba yake kuchota maji na ndipo mhalifu huyo alipomwagia tindikali na kwamba hakuweza kumtambua.

Sheha Mohammed Kidevu akiwa katika wodi ya Hospitali kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja akipata matibabu ya majaraha ya kitu kinachosadikiwa kwa Tindi Kali,akipata matibabu hayo katika hospitali hiyo.