Monday, May 13, 2013

MTOTO WA MIEZI MIWILI ANAJISIWA...


Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimeendelea kutokea nchini licha ya kupigwa vita kwa kampeni mbalimbali

Baadhi ya ukatili huo ni pamoja na kubakwa na ule wa kukatwa viungo vya mwili kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino).


Licha ya kupigiwa kelele, hata kampeni mbalimbali za kupinga kufanyika, unyama huo umeendelea kufanyika na tukio la hivi karibuni limemhusisha mtoto Erisia Tito mwenye miezi miwili anayedaiwa kunajisiwa wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.


Tukio hilo limekuwa gumzo katika mitaa mbalimbali wilayani humo, huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa linahusiana na imani za kishirikina.


Unaweza kujiuliza maswali mengi, hata inakuwaje mtoto wa miezi miwili kunajisiwa?

 

Katika vijiwe vya kahawa wilayani Mpwapwa, hii ni habari kubwa zilizokuwa zikizungumzwa kuhusu kunajisiwa kwa mtoto huyo swali likibaki; Je, yule mtu alimnajisi mtoto ameishia wapi?

Naingia chumba cha Mganga Mkuu Wilaya ya Mpwapwa kupata maelezo ya mtoto huyo tangu alipofikishwa katika hospitali ya wilaya hiyo, maendeleo yaliyofikiwa na utaratibu wa kiuchunguzi unavyoendelea.


Kauli ya Mganga Mkuu

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Lunemo Sakafu anasema kuwa tangu alipolazwa, mtoto huyo alikuwa akipelekwa kliniki kwa ajili ya kupatiwa chanzo mbalimbali na kupima afya yake, kwamba alikuwa na afya nzuri.

“Hakuzaliwa katika hospitali hii ila alikuwa akihudhuria kliniki, alizaliwa kwa wakunga wa jadi na mara ya mwisho kuja hapa hospitali ilikuwa Aprili 15, mwaka huu na alikuwa na afya nzuri,” alisema


Ashangazwa

Alisema kuwa alishangazwa na hali aliyokuwa nayo mtoto huyo alipofikishwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo kwani alikuwa akitokwa haja zote bila kikomo.

“Tunampatia matibabu ya kina ili kujua tatizo ni nini. Kwa sasa tuna utaratibu wa kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ili akafanyiwe vipimo vya kina kwa kuwa mtoto huyu anatoa haja zote bila kikomo,” anasema Sakafu.


Sakafu anasema hata wazazi wa mtoto huyo walipoulizwa juu ya hali aliyonayo mtoto wao, walipishana kauli katika maelezo yao na kwamba jambo hilo liliwatia shaka.


Kauli za wazazi

Baba wa mtoto huyo, Silvani Msemakweli anasema kuwa tangu mtoto wake alipozaliwa alikuwa na maumivu wakati wa kupata haja kubwa.

“Tangu alipozaliwa hali hii ilikuwapo hasa wakati wa kujisaidia haja kubwa mtoto analia, kwani husikia maumivu makali. Katika ukoo wetu yupo mmoja wa ndugu zetu aliyewahi kuwa na mtoto aliyekumbwa na hali kama hii ya mtoto wangu,” anasema na kuongeza:


“Yeye alipona baada ya kutumia dawa za kienyeji na alipona kabisa, siyo kweli kuwa mtoto alinajisiwa.”


Msemakweli anaongeza kuwa ni vigumu kuamini kama mtoto huyo amenajisiwa kutokana na mazingira ya familia hizo mbili, yaani familia yake na ya mke wake.


“Japo sikuwapo siku hiyo, lakini bado siamini kama mtoto wangu atakuwa amenajisiwa. Kwa sasa mama yangu ndiyo anayeshikiliwa na polisi na kufunguliwa kesi,” anasema Msemakweli.


Mama wa mtoto huyo, Rejina Msemakweli anasema kuwa yeye alijifungua kwa mkunga wa jadi aliyemtaja kwa jina la Hilda Maderemo na kwamba mtoto alikuwa mzima na hakuwa na tatizo lolote.


Anasema kuwa baada ya kujifungua alianza kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya kupata chanjo mbalimbali.


“Mwanangu nilimzaa akiwa mzima nilishangaa siku moja analia sana wakati huo alikuwa amepakatwa na bibi yake,” anasema na anaongeza:


“Nilimwacha na bibi yake kwa kuwa nilikwenda shambani ila niliporudi nilimkuta akiwa analia kupita kiasi. Nilimchukua na kumwogesha, lakini kabla sijamaliza niligundua kuwa ameumia sehemu zake za siri na alikuwa akitoka kinyesi mfululizo, yaani mbele na nyuma.”


Regina anaeleza kuwa familia yake ina watoto wawili ambao wote ni wasichana, mume wake pamoja na mdogo wake wa kike, kwamba pia wanaishi kwa ukaribu mkubwa na familia ya mume wake.


“Katika maisha yetu nimekuwa nikiishi na wakwe zangu bila maelewano mazuri, familia imekuwa ni yenye kugombana kila wakati, hata kama kitu ni kidogo. Lakini yataibuka mambo makubwa kiasi kwamba utadhani ni watu wasio familia moja inaniuma sana,” alisikitisha.


“Naongea kwa kuvumilia tu, lakini moyoni ninaumia kwa kiasi kikubwa kuona mwanangu amekuwa katika hali kama hii sielewi. Tukijaribu kumwuliza mama mkwe wangu hasemi ukweli kuwa mtoto amekuwaje,” anasimulia Regina huku akilia machozi.


Anasema kuwa aligundua kwamba sehemu za siri za mtoto wake zimevimba na kuonyesha kukwaruzika huku akitokwa na kinyesi bila kikomo.


Kauli ya mkunga

Mkunga Hilda Mademo anakiri kuwa alimzalisha Regina na kwamba mtoto huyo alikuwa mzima bila kuwa na kasoro yoyote.

“Mimi ndiye niliyemzalisha mama huyo na mtoto alizaliwa akiwa mzima kabisa. Suala la kupatikana kwa tatizo hilo, ukweli wanao wazazi wenyewe. Huduma zangu nilizitoa hata hospitali ya wilaya inalifahamu, walinitembelea hadi hapa kuona mazingira ninayofanyia kazi na kunisaidia baadhi ya vifaa kwa mfano haya mabakuli,” anasema Hilda.


Polisi yatoa tamko

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi David Misime anakiri kupokea taarifa za kunajisiwa kwa mtoto wa miezi miwili katika Kijiji cha Ising’u wilayani Mpwapwa.

“Sisi tulipokea taarifa hiyo na kuanza kuifanyia kazi za awali, hadi sasa bibi wa mtoto huyo yuko mikononi mwa polisi. Tunasubiri jibu la kitaalamu kutoka kwa daktari kwa kuwa wakati mtoto amepelekwa katika hospitali,”alisema Misime na kuongeza:



“Katika Kituo cha Polisi hapakuwa na ushahidi wa kujitosheleza kwa kuwa mtoto huyo tayari alikwishasafishwa siku tatu zilizopita.”

Viongozi wa Serikali wakemea

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, Ryoba Kangoye amekemea vikali tukio hilo na kuliita ni la ugaidi kwa kuwa mtu huyo hakuwa na nia ya kubaka bali ni kuua.

“Hii hali siyo ya kawaida ni mstuko mkubwa kusikia hili kama hiyo kujitokeza katika mazingira hayo. Hivi, Mtanzania wa leo kufikia kufanya jambo kama hilo ni ajabu kubwa, hata hiyo familia kukaa kimya ni kunyima haki vyombo vya sheria kufanya kazi zake na kupoteza ushahidi uliokamika,“ anasema Kangoye.


Mtendaji wa kijiji hicho, Emmanuel Mamba anasema kuwa waliposikia tukio hilo walijikuta ni kama wamemwagiwa maji au tindikali wakilifananisha na mauaji.


“Tulioposikia tuliishiwa na nguvu kwa kuwa hata kama matendo kama hayo hufanyika, basi isingekuwa kwa mtoto mdogo kama huyo, asiye na uwezo wowote ule. Tulijiuliza maswali mengi hata kuhisi huenda walitaka kumfanyia ukeketaji,” anasema Mamba


Viongozi wa dini

Kwa niaba ya madhebu ya dini, Padiri Masasi Deo kutoka Kanisa la Katoliki Mpwapwa, amekemea vikali tabia hiyo akisema:

“Nionavyo sasa umefika wakati wa watu wenye dhamana na jamii kukaa pamoja na kufanya ibada na kujua mbinu mpya ya kufundisha maadili kutokana na hali ya maadili ilivyobadilika nchini.”


Haki za binadamu

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu (AFNET)Mkoa wa Dodoma, Sara Mwanga amesema kuwa kitendo hiko ni unyama na kwamba jamii bado haina elimu ya kujitambua kuhusu ukatili unaofanywa hasa katika kushughulikia kesi za aina hiyo.

“Watoto wengi wamekuwa wakiumizwa, lakini mwishowe hakuna linalofanyika katika kumtetea mtoto huyo kutokana na wahalifu huachiwa huru kwa kile kinachodaiwa ushahidi haujakamilika. Kwa kweli kuna utata mkubwa katika suala hilo,” alisisitiza.


Aliitaka Serikali kupitia vyombo vya dola kuwa makini katika kuangalia namna ya kupatikana kwa ushahidi ili kutenda haki kwa watoto wanapoumizwa, badala ya watuhumiwa kuachiwa huru kwa madai kuwa ushahidi haujakamilika.

Wataka waruhusiwe kujiua Uingereza

 13 Mei, 2013 

Marehemu Tony Nicklinson naye aliwahi kutaka mahakama imruhusu auawe kwa usaidizi wa daktari kwa sababu ya ulemavu wake

Wanaume wawili wenye ulemavu mbaya zaidi wanakwenda mahakamani kukata rufaa katika kesi inayoonekana kuwa moja ya kesi inayotaka mageuzi makubwa ikitaka kubadilisha sheria za serikali kuhusu haki ya mtu kufa.
Mmoja wa watu hao, Pail Lamb amekuwa na ulemavu mbaya kwa miaka mingi pamoja na kupitia uchungu mwingi, hawezi kujitoa uhai wake na anataka madaktari waruhusiwe kumuua bila ya kukabiliwa na kosa la mauaji baadaye.
Mwanamume mwingine anayejulikana kama Martin, anataka uamuzi utakaowaruhusu madaktari wamsaidie kujiua ingawa waweze kulindwa kutokana na sheria za kuweza kuwashtaki kwa kufanya kitendo cha mauaji.
Wakosoaji wanasema kuwa ikiwa mahakama itaruhusu wawili hao wajiue, itakuwa na athari kubwa kwa watu wazee na wenye ulemavu kutaka kujinyonga ili kuzuia kuwahangaisha jamaa zao kuwahudumia.

Wagonjwa wa kiakili watoroka hospitalini Kenya

 13 Mei, 2013 

Wagonjwa wa kiakili
Polisi wanawatafuta wagonjwa karibia arobaini waliotoroka kutoka hospitali ya watu wenye matatizo ya kiakili, mjini Nairobi ya Mathare. Wagonjwa hao wanasemekana waliwashinda nguvu walinzi wao na kutoroka.
Zogo hilo lilizuka katika hospitali ya Mathare baada ya kutokea hali ya sintofahamu iliyowahusisha wafungwa arobaini wanaume.
Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuwa wagonjwa hao walikuwa wanateta kuhusu hali mbaya na kibinadamu katika hospitali hiyo.

Sunday, May 12, 2013

MAMA AMCHOMA MOTO MTOTO WA WIFI YAKE SEHEMU ZA SIRI KWA KOSA LA KUNYWA UJI WA MTOTO



ELIZABETH Bureko (26), mkazi wa Kata ya Nyamatare, Manispaa ya Musoma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma, kwa tuhuma za kumchoma na moto sehemu za siri mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane.
 



Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Baraka Maganga, ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Sajini Stephano Mgaya, kuwa mwanamke huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 24 mwaka huu, saa 3 asubuhi.


Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, mshitakiwa alikiuka kifungu cha sheria namba 169 cha mwenendo wa makosa ya jinai kama sheria hiyo ilivyofanyiwa marekebisho na kuwa namba 16, mwaka 2002.


Alidai kwamba, mshitakiwa huyo alimchoma katika sehemu zake za siri na mdomoni baada ya kumtuhumu mtoto huyo wa wifi yake, kwamba alikuwa akinywa uji wa mtoto aliyekuwa akimnywesha.


Mshitakiwa alikana shitaka na kurudishwa mahabusu hadi Mei 25 mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.

Nawaz Sharif afikiria kuunda serikali

 12 Mei, 2013 - Saa 09:44 GMT

Kiongozi wa chama cha Pakistan cha Muslim League, Nawaz Sharif, amezungumza na wenzake chamani kuhusu namna ya kuunda serikali yake mpya baada ya uchaguzi mkuu wa Jumamosi.
Nawaz Sharif kwenye kampeni
Matokeo yasiyo rasmi yanaonesha kuwa Muslim League itakuwa na viti vya kutosha bungeni kuunda serikali, lakini huenda kikahitaji kuungwa mkono na vyama vengine.
Bwana Sharif, ambaye amewahi kuwa waziri mkuu mara mbili kabla, alisema kuwa watu wameonesha wanaamini kuwa chama chake kinaweza kuleta mabadiliko.
Mcheza kriketi maarufu wa zamani, Imran Khan, ambaye huenda akawa kiongozi wa upinzani, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi; lakini alisema taarifa za udanganyifu kwenye kura zinavunja moyo.
Chama tawala cha PPP inaelekea kuwa kimeshindwa vibaya.

Syria yarejesha lawama zote kwa Uturuki

 12 Mei, 2013 - Saa 14:41 GMT

Syria imekanusha vikali tuhuma kutoka Uturuki kwamba ilihusika na miripuko miwili ya mabomu yaliyotegwa ndani ya magari Jumamosi katika mji wa wa mpakani wa Reyhanli, ambayo iliuwa watu 46.
Mji wa Reyhanli baada ya miripuko wa mabomu Jumamosi
Waziri wa Habari wa Syria, alisema serikali ya Uturuki ndio ya kubeba lawama kwa sababu imeruhusu eneo lake kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa.

Ilikuwa jawabu kali kutoka kwa serikali mjini Damascus ambayo imekanusha kabisa kuwa idara yake ya ujasusi ndio iliyofanya mashambulio ya mabomu yaliyotegwa ndani ya gari, na imewatupia lawama zote wakuu wa Uturuki.
Waziri wa Habari, Omran Zoabi, alisema serikali ya Uturuki ndiyo iliruhusu na kuwezesha silaha, mabomu, magari, wapiganaji na fedha kuvuka mpaka wake na kuingizwa Syria.
Hayo yamelifanya eneo la mpakani kuwa kituo cha ugaidi wa kimataifa; na viongozi wa Uturuki lazima wabebe dhamana ya kisiasa na kiutu.
Na upinzani wa Syria nao piya umeilaumu serikali ya Syria kwa mashambulio ya jana ukisema hilo ni jaribio la kuleta mzozo baina ya Uturuki na maelfu ya wakimbizi wa Syria waliopewa hifadhi na Uturuki.
Kuna hasira kati ya Waturuki kuwa vita vya Syria vimetapakaa na kuleta umwagaji damu nchini mwao.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anatarajiwa kukutana na Rais Obama mjini Washington, hapo Alhamisi.

WHO yasema coronavirus yaambukiza

 12 Mei, 2013 
Shirika la Afya Duniani, WHO, linasema inaelekea sana kuwa aina mpya ya virusi vinavouwa, vya coronavirus, vinaweza kuambukizwa baina ya watu walio karibu sana.
Coronavirus
Virusi hivyo ni sawa na vile vya homa ya SARS (Severe Acute Respiratory Syndrome) na vinamfanya mgonjwa kuwa na shida sana ya kuvuta pumzi.
Nchini Ufaransa mwanamume mwengine hivi sasa ni mahtuti baada ya kuambukizwa na mgonjwa wa mwanzo nchini humo, ambaye walilazwa chumba kimoja hospitali.
Hadi sasa watu 34 wanajulikana kupata ugonjwa huo duniani tangu mwaka wa 2012, 18 kati yao walikufa Saudi Arabia.
WHO inasema ni muhimu kujulisha watu kuhusu virusi hivyo kwa sababu kuna wasi-wasi mkubwa kuwa vinaweza kusambaa.